Showing posts with label MICHEZO. Show all posts
Showing posts with label MICHEZO. Show all posts

Tuesday, 28 November 2017

BEYONCE 'NDANI' HARUSI YA BALE

Gareth Bale na mpenzi wake.
NYOTA wa soka wa klabu ya Real Madrid ya Hispania na timu ya taifa ya Wales, Uingereza, Gareth Bale, ameripotiwa kumtaka staa wa muziki Mmarekani, Beyonce, kutumbuiza siku ya harusi yake mwaka kesho.
Hata hivyo, itambidi Bale zimtoke Paundi milioni l.5 (Sh. bilioni 4.4) ili kupata burudani ya nyota huyo maarufu duniani.
Bale anategemea kumwoa mpenzi wake wa siku nyingi, Emma Rhys-Jones, ambapo anataka mwanamuziki huyo wa kundi lililokuwa linajulikana kama Destiny’s Child, awaburudishe waalikwa.
Beyonce.
Ndoa hiyo iliyotakiwa kufanyika nchini Italia mapema, ilichelewa kutokana na baba wa Rhys-Jones kufungwa kutokana na utapeli nchini Marekani.
Wawili hao wamefahamiana tangu utotoni na wanaishi jijini Madrid na watoto wao wa kike wawili. Baada ya sherehe hiyo huko Italia, wamepanga kufanya sherehe nyingine huko Wales.
Bale ana mkataba na Real Madrid ambapo analipwa Sh. milioni 894 kwa wiki (Paundi 300,000) na anasemekana anaweza kuhama kwenda Manchester United ya Uingereza. Beyonce, aliyeoana na nyota wa muziki wa hip-hop, Jay-Z mwaka 2008, ameuza rekodi zipatazo milioni 100 akiwa msanii anayejitegemea.
Share:

Trioni 1.8 kumuondoa Mess Barcelona


Mshambuliaji wa FC Barcelona ambaye pia ni nahodha wa timu ya taifa ya Argentina Lionel Messi hivi karibuni ameripotiwa kuamua kuongeza mkataba mpya wa kuendelea kusalia FC Barcelona.

Barcelona ni timu ambayo imemlea Lionel Messi toka akiwa katika kituo cha kukuzia vipaji cha Barcelona kinachojulikana kwa jina la La Masia.

Messi ameamua kuongeza mkataba mpya na FC Barcelona utakaomuweka Nou Camp hadi mwaka 2021 kubwa lililochukua headlines katika mkataba wa Lionel na kuzua mijadala ni kipengele kilichopo katika mkataba wake, kama kuna club itakayofikiria kumuondoa Lionel Messi FC Barcelona kama PSG walivyofanya kwa Neymar.

Watahitaji kutoa dau la pound milioni 626 ambazo ni zaidi ya Tsh Trioni 1.8, Lionel Messi hadi anasaini mkataba mpya wa kuendelea kuitumikia FC Barcelona, alikuwa ameichezea game 602, akifunga jumla ya magoli 523 na ametwaa mataji 30 akiwa na FC Barcelona na bado historia inaendelea hadi 2021.
Share:

Friday, 13 October 2017

MANENO YA NIYONZIMA YANGA


Kiungo wa Simba, Mnyarwanda, Haruna Niyonzima.
KIUNGO wa Simba, Mnyarwanda, Haruna Niyonzima, ameweka wazi kuwa endapo timu yake hiyo itaibuka na ushindi kwenye mchezo wao dhidi ya Yanga, basi atashangilia.

Niyonzima ambaye ali­jiunga na Simba mwanzoni mwa msimu huu akitokea Yanga, amebainisha hilo ikiwa ni siku chache kabla timu hizo hazijakutana.
Oktoba 28, mwaka huu ni siku ambayo Yanga na Simba zina­tarajiwa kupambana kwenye mchezo wa Ligi Kuu Bara utakaopigwa katika Uwanja wa Uhuru jijini Dar.

Akizungumza na moja ya vyombo vya habari hapa nchini, Niyonzima alisema mchezo baina ya Simba na Yan­ga siku zote huwa ni mgumu, lakini ameonyesha dhamira yake ya kushangilia bila ya kuhofia chochote ikitokea wao wamepata ushindi na kama yeye akifunga.

“Hakuna asiyejua ugumu wa mechi baina ya Simba na Yanga, katika mechi zinazokuwa na kukamiana kwingi ni hizo, hivyo nitafurahi kama tukipata pointi tatu dhidi yao au nikifunga nitashangilia japokuwa itakuwa kiungwana siyo kwa nyodo na dharau.

“Zaidi naomba siku tukikutana tupate pointi tatu tu maana ndiyo kitu cha muhimu kwetu, ili tuweze kufikia mafanikio yetu ya kutwaa ubingwa wa ligi msimu huu, ni lazima tupate pointi tukicheza na Yanga, Azam na Singida United.

“Hizi ndizo timu kubwa kwa sasa na ndiyo ambazo naona zina upinzani mkubwa kwetu, hivyo ili upate ubingwa kwa sasa ni muhimu pia uhakik­ishe unapata pointi katika timu hizo,” alisema Niyonzima.
Share:

Tuesday, 10 October 2017

ROBERTO LEWANDOSKI ADHIHIRISHIA UMMA KUWA YEYE SI MPIRA TU

Kama kuna mwanadamu mwenye bahati wiki hii baasi atakuwa ni Roberto Lewandoski, mshambuliaji huyo wa Poland mambo yake yanaonekana kumnyookea sana kuanzia ndani hadi nje ya uwanja.
Wakati Poland wakikipiga na Montenegro katikati ya wiki hi Lewandoski alifikisha idadi ya mabao 16 katika mechi za kufuzu kombe la dunia, idadi hiyo haijawahi kufikiwa na mchezaji yoyote katika mechi hizo.

Pia hattrick dhidi ya Almernia ilimfanya kufikisha mabao 50 katika timu yake ya taifa katika michezo 90, idadi hii ya mabao imevunja rekodi ya ufungaji Poland iliyokuwa ikishikiliwa na Wlodek Lubanski amabaye alifunga mabao 48 katika michezo 75.

Kama hiyo haitoshi lakini idadi hiyo ya mabao iliwafanya Poland kufudhu kwa ajili ya kombe la dunia litakalopigwa mwakani, safari ya Poland kwenda Urusi inakuja ikiwa ni baada ya kuikosa michuano hiyo mwaka 2010 na 2014.

Lakini jana Jumatatu jina la Roberto Lewandoski lilikuwepo kati ya majina 30 ya mwanzo ya wachezaji ambao wanagombania tuzo kubwa kabisa ya Ballon D’Or, Lewandoski jina lake limekuja baada ya msimu mzuri sana na Bayern Munich.

Ila hayo ni mambo ya kisoka, nje ya soka Roberto Lewandoski alikuwa na wakati mzuri sana kielimu, mshambuliaji huyu ametunukiwa degree yake ya kwanza ihusianayo na masuala ya elimu ya michezo.
Share:

Sunday, 8 October 2017

INIESTA ASAINI MKATABA WA MAISHA BARCELONA


Kiungo na nyota machachari wa klabu ya FC Barcelona Andres Iniesta  ameongeza mkataba wake na timu hiyo maisha yake yote.

Timu hiyo ya Catalonia imetangaza Ijumaa katika jarida lake rasmi kuwa imeafikiana na Iniesta kusalia katika timu hiyo maisha yake yote.
Jarida hilo lilifahamisha kuwa kiongozi wa timu hiyo Josep Maria Bartomeu alishiriki katika hafla ilioandaliwa kwa ajili ya kutia saini kuhusu mkataba huo.

Iniesta alijuanga na timu ya Barcelona Oktoba 29 mwaka 2002.
Share:

HII NDIYO SIKU YA OKWI KUREJEA SIMBA

Mchezaji wa Simba, Emmanuel Okwi.
Mshambuliaji nyota wa Simba na mchezaji bora wa mwezi, Emmanuel Okwi anatarajia kurejea nchini ili kuungana na klabu yake ya Simba siku ya kesho akitokea nchini Uganda.
 
Okwi aliondoka nchini kwenda Uganda ambako aliungana na kikosi cha timu ya taifa ya Uganda kwa ajili ya mechi ya kuwania kufuzu kucheza Kombe la Dunia.

Katika mechi hiyo, Uganda ilifanikiwa kupata sare ya bila kufungana, mechi ambayo ilikuwa ngumu.

Maofisa wa Simba wamesema, Okwi atangana na wenzake kesho kwa ajili ya maandalizi ya mechi zijazo.


Simba inatarajia kuivaa Mtibwa Sugar katika mechi ijayo ya Ligi Kuu Bara, mechi itakayopigwa Jumapili ijayo.
Share:

Friday, 6 October 2017

KESHO SIMBA KUIJUA MBIVU NA MBICHI

Klabu ya Simba huenda kesho ikaingia kwenye ukurasa mpya wa uendeshaji wa timu ambapo kamati maalum ya kusimamia mchakato wa zabuni ya kumpata mwekezaji kwenye muundo mpya wa klabu ya hiyo kesho Saa 5:00 asubuhi inatarajiwa kukutana na Waandishi.
Taarifa ya Simba SC kwa vyombo vya Habari iliyotolewa na Mkuu wa Idara ya Habari na Mawasiliano wa klabu, Hajji Sunday Manara imesema kwamba mkutano huo utafanyika kwenye ukumbi wa Kivukoni 3 uliopo ndani ya hoteli ya Serena mjini Dar es Salaam.

Kamati hiyo iliyoundwa mapema mwezi uliopita, ipo chini ya Mwenyekitil, Jaji Mstaafu wa Mahakama Kuu Thomas Mihayo na Wajumbe wengine wanne, ambao ni Mbunge wa Ilala, Mussa Azzan ‘Zungu’, Mkurugenzi wa Bodi ya Mikopo ya Elimu ya Juu, Abdul-Razaq Badru, Wakili Dk. Damas Ndumbaro na Yusuph Maggid Nassor.

Agosti 20, mwaka huu wanachama 1,216 wa klabu ya Simba waliridhia mfumo wa klabu yao kuuza Hisa baada ya Mkutano uliofanyika Ukumbi wa Kituo cha Kimataifa cha Mikutano cha Mwalimu Nyerere (MNICC), Dar es Salaam.

Katika mkutano huo uliohudhuriwa na Waziri wa Afya Jinsia na Watoto, Dk Hamisi Kigwangala, Kaimu Mwenyekiti wa klabu, Salim Abdallah 'Try Again' alisema kwamba asilimia 50 ya hisa zitauzwa kwa mwekezaji au wawekezaji watakaoungana wasiozidi watatu, kwa sharti moja tu la kuwa wanachama wa klabu hiyo.  Mwekezaji anatakiwa kuweka dau lisilopungua Sh. Bilioni 20 ili kupatiwa asilimia 50 ya hisa za klabu, wakati kwa kuanzia wanachama wote wa Simba wamepewa asilimia 10 ya hisa.
Share:

Monday, 2 October 2017

NIYONZIMA, AJIBU WAWATIBUA YANGA

Mshambuliaji wa Yanga, Ibrahim Ajibu akikabidhiwa jezi namba kumi wakati alipojiunga na klabu ya Yanga.
WAKATI kivumbi cha Ligi Kuu Bara kikizidi kupamba moto, baadhi ya mashabiki wa timu ya Simba juzi Jumamosi walijikuta wakiingia katika mvutano mkubwa na kutaka kushushiana makonde kuhusiana na mshambuliaji wa Yanga, Ibrahim Ajibu.

Mvutano huo ulitokea katika Uwanja wa Uhuru jijini Dar wakati Ajibu alipokuwa akiitumikia Yanga dhidi ya Mtibwa Sugar katika mchezo uliomalizika bila ya kufungana.

Wakati mechi hiyo ikiendelea, mmoja wa mashabiki wa Simba ambaye jina lake halikuweza kujulikana, aliyekuwa uwanjani hapo akiiunga mkono Mtibwa Sugar, alidai kuwa katika usajili bora ambao Yanga wananufaika nao msimu huu ni ule wa Ajibu.
Mnyarwanda Haruna Niyonzima.
Alisema kuwa tangu ajibu ajiunge na Yanga amebadilika na sasa anacheza soka la uhakika tofauti na alivyokuwa Simba msimu uliopita na mabao yake yameweza kuisaidia Yanga kupata pointi sita lakini wao wamepata hasara kwa kumsajili, Mnyarwanda Haruna Niyonzima akitokea Yanga kwa madai kuwa hakuna chochote alichokifanya mpaka sasa tangu ajiunge na timu hiyo.

Kauli hiyo uliungwa mkono na mashabiki wengi wa Simba waliokuwa uwanjani hapo lakini ikapingwa vikali na wachache wakidai kuwa Niyonzima ni mchezaji mzuri lakini kocha wao mkuu, Mcameroon, Joseph Omog bado hajajua kumtumia, ndiyo maana anaonekana hana msaada katika timu hiyo. Hali hiyo ilizua mzozo mkubwa uliosababisha mashabiki hao kutaka kutwangana makonde. Hata hivyo, tangu Ajibu ajiunge na Yanga amefanikiwa kuifungia timu hiyo mabao mawili mpaka sasa kati na manne ambayo imefunga lakini Niyonzima hana bao lolote, ingawa yeye anacheza nafasi ya kiungo.
Share:

Sunday, 1 October 2017

BAADA YA SIMBA KUILAZA STAND MANARA, MWANJALI WASEMA HAYA

Baada ya timu ya Simba kuzima kelele na vijembe vya mashabiki wa Stand United kwa kuibuka na ushindi wa mabao 2-1 yaliyofungwa na Shiza Kichuya pamoja na Laudit Mavugo kwenye Uwanja wa Kambarage mkoani Shinyanga leo Jumapili msemaji wa timu hiyo Haji Manara atoa ya moyoni.
Ambapo kupitia ukurasa wake wa Instagram Msemaji huyo alituma ujumbe uliosoka hivi "Alhamdulilah, muhimu tumepata points tatu leo, Simba raha sana."
Kikosi hicho ambacho kimefanikiwa kuchomoka na pointi tatu muhimu, kimeleta matumaini kwa mashabiki wao baada ya mchezo uliopita kutoka sare ya mabao 2-2 na Mbao FC.
Timu hiyo imepanda kileleni ikiwa imefikisha pointi 11 ambazo zimefikiwa na Azam FC pamoja na Mtibwa huku watani zao Yanga walikwaa kisiki jana baada kutoka suluhu ya 0-0 dhidi ya Mtibwa Sugar kwenye Uwanja wa Uhuru jana Jumamosi.
Nahodha wa timu hiyo, Mwanjali alisema wanampongeza kipa wao Aishi Manula kwa kuokoa hatari nyingi, huku akisistiza kuyafanyia kazi upungufu uliyojitokea katika kikosi hicho cha leo.
Hata hivyo aliongeza kuwa awali kikosi hicho kililala jambo ambalo liliwapa nafasi wapinzani wao kufunga bao la kufutia machozi.

Share:

Saturday, 30 September 2017

PEP GURDIOLA ALIVYOSHUSHA REKODI YA CHELSEA

Haikuwa siku nzuri kwa Antonio Conte na mbinu za Pep Gurdiola zilimpoteza kabisa, ilikuwa mbaya kwa Chelsea kwani ndio mchezo wa kwanza kwa Chelsea kupiga mashuti machache.
Chelsea hawajawahi kupiga mashuti yaliyolenga bao chini ya 5 tangu Conte ajiunge nao, lakini hii leo wamepiga mashuti manne tu huku kuanzia dakika ya 26 hadi mpira unaisha walipiga mashuti mawili tu.
Manchester City walipata bao lao la kwanza na la pekee kupitia kwa Kelvin De Bruyne na kuwafanya sasa kuwa wamecheza michezo minne mfululizo wakishinda bila kuruhusu bao katika Epl.
Kule nchini Ufaransa Kylian Mbappe alifunga moja ya bao katika ushindi wa bao 6 kwa 2 dhidi ya Bordeaux na kumfanya kinda huyo kuhusika katika mabao 29 ya ligi ya Ligue 1 msimu huu akifunga 14 na kuasisst 5.
Share:

HIZI NDIYO WIKI ATAKAZOKAA NJE AGUERO

MSHAMBULIAJI Sergio Aguero anahitaji angalau wiki nne za mapumziko baada ya kuvunjika mbavu katika ajali ya gari usiku wa juzi mjini Amsterdam.
Mchezaji huyo wa Manchester City aliumia Alhamisi wakati teksi aliyokuwa amepanda yeye na rafiki yake kwenda Uwanja wa Ndege ilipoacha barabara na kugonga nguzo pembeni.

Muargentina huyo ambaye alikuwa katika siku yake mapumziko, alikwenda kushuhudia tamasha ingawa ilikuwa ndani ya saa 48 kabla ya City hauijavaana na Chelsea leo jioni katika mchezo wa Ligi Kuu ya England Uwanja wa Stamford Bridge.

Kocha wa City, Pep Guardiola alisema jana kwamba hana tatizo na mchezaji huyo mwenye umri wa miaka 29 kusafiri katika siku yake ya mapumziko ingawa pia alisema hakuwa na taarifa za safari ya Aguero.

Usiku wa Ijumaa, Aguero alitweet picha yake akionyesha dole gumba juu sambamba na maelezo: "Nipo nyumbani Manchester baada ya kufanyiwa vipimo na madaktari wa klabu. Nimevunjika mbavu. Nimeumia, lakini niko salama, naangalia namna ninavyopata nafuu. Asante kwa wote walionitumia ujumbe na kunisapoti,"alisema.

Baada ya kuangalia tamasha la mwanamuziki wa Colombia, Maluma, Aguero na rafiki yake walikuwa wanakwenda Uwanja wa Ndege Saa 7:00 usiku kuchukua ndege binafsi kurejea Manchester wakati teksi inaacha barabara na kugonga nguzo.

Akifafanua kilichotokea, Aguero alitweet: "Teksi niliyopanda ilikosea kugeuka ikagonga nguzo. Ulikuwa ni mshindo mkubwa, lakini mkanda wa kiti ulinisaidia kutoumia zaidi,".

Alipoulizwa kuhusu safari ya Aguero Uholanzi, Guardiola alisema: "Mimi si Polisi. Nilijua nilipoamka. Sitaki kujua wachezaji wangu wanafanya nini,".
Share:

ALICHOSEMA MANARA LEO CHAZUA GUMZO MTANDAONI

 Afisa habari wa klabu ya Simba, Haji Manara amezua gumzo mtandaoni leo baada ya kufunguka jambo lililoonekana kuwa mwiba mkali kwa mashabiki wa Yanga, Azam na Simba.

Msemaji huyo wa wekundu wa msimbazi alidai kuwa kitendo cha mchezaji, Cristiano Ronaldo kununua gari aina ya bugatti lenye thamani ya bilioni nne za kitanzania ni ukatili uliopitiliza bora pesa hizo zingetumika kulipa wachezaji wa Yanga, Simba na Azam.
Manara alieleza hayo kupitia ukurasa wake maalum wa instagram baada ya kupita siku moja tokea nyota huyo wa kimataifa anayechezea klabu ya Real Madrid kuweka hadharani gari hilo katika mtandao wake na kufanya mamia ya watu kumpongeza kwa hatua hiyo aliyofikia huku wengine wakibakia kutoamini kwa kilichotokea.

"Bugatti ya 2017 imenunuliwa na Ronaldo kwa thamani ya Dola milion 1.8, karibia na Bilioni nne za madafu. Unalipa 'salary' ya mwaka mzima kwa wachezaji wa Yanga, Simba na Azam. Huu ni ukatili uliopitiliza", ameandika Manara.
Hivyo Manara akajikuta akiwaacha mashabiki wa timu za hapa nchini katika mzozo usio na kikomo.
Share:

Friday, 29 September 2017

AJIBU APINDUA REKODI YA SIMBA

STRAIKA mpya wa Yanga, Ibrahim Ajibu, amefanikiwa kuipindua rekodi yake ya mabao kwa msimu uliopita alipokuwa akiitumikia Simba baada ya kucheza mechi nne za awali.

Ajibu ambaye ni zao la Simba, amejiunga na Yanga msimu huu baada ya kumaliza mkataba wake na Simba.

Katika msimu wake wa kwanza ndani ya Simba akicheza kikosi cha wakubwa ambao ulikuwa ni 2015/16, mshambuliaji huyo alionyesha uwezo mkubwa katika mechi nne za kwanza lakini hakuweza kufunga bao lolote ambapo mechi tatu za kwanza zote walitoka sare ya mabao 2-2 dhidi ya Costal Union, Polisi Moro(1-1), Stand United (2-2) na suluhu na Yanga.

Msimu uliopita ambao ni 2016/17, mshambuliaji huyo hakuweza kufunga bao lolote katika mechi nne za kwanza kabla ya kuibuka katika mechi yao dhidi ya Majimaji akifunga mabao matatu kwenye ushindi wa mabao 6-1.

Msimu wake wa kwanza ndani ya Yanga, tayari Ajibu ameshafunga mabao mawili kwenye mechi nne alizocheza. Mabao yake hayo yameipa Yanga pointi sita kwani kila alipofunga timu hiyo imeibuka na ushindi wa bao 1-0.

Ajibu alifunga bao la kwanza msimu huu katika mchezo dhidi ya Njombe Mji na kuweza kuipa ushindi timu yake wa bao 1-0 kabla ya kufunga tena katika mchezo dhidi ya Ndanda FC na kuibuka na ushindi kama huo, ameshindwa kufunga dhidi ya Lipuli FC na Majimaji SC.

Wakati huohuo, beki kisiki wa Yanga, Nadir Haroub ‘Cannavaro’ ameibuka na kusema kuwa kiwango kinachoonyeshwa na Ajib ni habari nyingine katika kikosi chao na kudai kuwa ana matumaini makubwa ya mchezaji huyo kuwa tegemeo katika kikosi chao.

Akizungumza na gazeti hili, Cannavaro amesema kuwa, hakuna asiyefahamu uwezo wa Ajibu, hivyo mabao anayoyafunga ni mwanzo mzuri kwao kuona atakuwa tegemeo katika kikosi hicho msimu huu.

“Ajibu ni mshambuliaji mzuri na ameonyesha kasi nzuri hivyo naamini ushirikiano wake pamoja na washambuliaji wengine utasaidia kuifanya timu yetu iweze kufanya vizuri kwenye ligi,” alisema Cannavaro.
Share:

KATIBU ABAINISHA KINACHOISULUBU YANGA SASA

Lwandamina na Nsajigwa wakimfunda Mwashiuya
Lwandamina na Nsajigwa wakimfunda Mwashiuya wakati tizi likiendelea kwenye manyunyu jijini Dar es Salaam. 
KATIBU wa zamani wa Yanga, Abdul Sauko, ametamka wazi kwamba kinachotokea kwenye klabu hiyo kwa sasa, ni matokeo ya kukosa watu wenye mapenzi ya dhati ya kujitolea kwa moyo kama tofauti na zamani na ndio maana timu inayumba nje ya uwanja.
Sauko aliyeshikilia nafasi mbalimbali za ukatibu klabu hapo miaka ya nyuma, alisema katika uongozi wao waliwatafuta matajiri na kuwajengea moyo wa kujitolea, jambo lililoisaidia Yanga kiasi cha kutisha Afrika Mashariki na Kati mpaka kupachikwa jina la Yanga Afrika Umoja wa Mataifa.
Alisema bado kuna watu ambao  wanaweza kutoa michango yao kwa timu, lakini akadai baadhi ya viongozi hawajajiweka karibu na watu hao ili kuonyesha umuhimu wao ndani ya timu na kusaidia kujitoa kwa hali na mali.
“Sisi tuliwatafuta na kuwaweka karibu, ndiyo maana wakati ule hata pesa za usajili tulichangishana kuhakikisha timu inafanya vizuri,” alisema Sauko ambaye alikuwa miongoni mwa waasisi wa kundi la Yanga Family ambalo lilikuwa mhimili wa usajili mwanzoni mwa miaka ya 2000.
“Wachezaji na wafanyakazi kwa ujumla wakitimiziwa mahitaji yao, watajituma kikamilifu.
“Mipango ya timu ilikuwa wazi kwao, ndicho kilichokuwa kinawafanya wawe na uchungu wa kuona inapotokea timu ikatetereka kwa masuala ya fedha, inakuwa aibu kwao, hilo linapaswa kufanywa kwa sasa. Hata nafasi za ujumbe ndani ya klabu zilishikwa na watu ambao walikuwa tayari kujitolea kutatua shida ndogo ndogo. Hilo pia lilikuwa msaada kwa timu kiasi cha kuwa na mafanikio ya hali ya juu.”
Sauko aliwataka viongozi waliopo madarakani Yanga kwa sasa, wawasake wadhamini ambao watabeba gharama za klabu kwa asilimia 80, watafanya wachezaji wapate mishahara kwa wakati, wasafiri kwenda mikoani, huku asilimia 20 ya gharama, ziwe za wanachama kujitolea, uuzwaji wa jezi pamoja na pesa za viingilio vya timu inapofanya mazoezi.
“Ni kutengeza mipango madhubuti, wanachama wanapenda timu zao, wapo tayari kutoa viingilio vya mazoezi, hivyo wanaweza kupata pesa ndogo ndogo za kukidhi mahitaji yao, naamini hilo litawapa hatua.
“Tulikuwa tunatangaza viingilio pindi timu ikifanya  mazoezi Uwanja wa Kaunda, mashabiki walikuwa wanakuja, tena wengine kutoka mbali, hasa kipindi cha usajili ndipo tulipata pesa zaidi kutokana na mashabiki kuwa na hamu ya kuwaona wachezaji wapya.
“Lazima unapopanga bajeti ya mwezi kwa klabu kama Yanga, uwe na miradi ama vyanzo vya kupata pesa,  lasivyo mipango itakuwa inaingia doa na kushindwa kufikia pale panapotakiwa.
“Najua maneno haya hayatawafurahisha wengi lakini ndiyo ukweli.”
Share:

Thursday, 28 September 2017

CARLO ANCELOTTI KWA HERI

Kocha wa Bayern Munich Carlo Ancelotti amefutwa kazi leo kufuatia mwanzo mgumu wa msimu wa 2017/18 yakiwemo matokeo ya jana usiku ambapo timu hiyo ilikubali kichapo cha mabao 3-0 kutoka kwa PSG.
Mkurugenzi mtendaji wa Bayern Munich Karl-Heinz Rumminigge alionekana kuchukizwa na matokeo ambapo alisema Bodi ya timu itakuwa na kikao na kocha Ancelotti mchana wa leo baada ya timu kurejea kutoka Paris Ufaransa.

Mchana huu Sky Sports imethibitisha kuwa baada ya kikao Bodi imefikia maamuzi ya kusitisha kibarua cha kocha huyo raia wa Italia.

Ancelotti mwenye miaka 58 ameitumikia Bayern kwa msimu mmoja wa 2016/17 baada ya kuchukua nafasi ya Pep Gaurdiola ambaye alijiunga na Manchester City. Muitaliano huyo ameiwezesha Bayern kutwaa ubingwa wa Bundesliga msimu uliopita.
Share:

SIMBA NA YANGA WAZUA TAHARUKI

Gumzo la mechi ya watani Yanga na Simba itakayochezwa Oktoba 28 limezidi kupanda baada ya kuelezwa kuwa Uwanja wa Taifa jijini Dar es Salaam, utakuwa katika matengenezo.
Waziri wa Habari, Utamaduni, Sanaa na Michezo, Dk Harrison Mwakyembe alisema jana, uwanja huo unahitaji muda wa miezi mitatu zaidi na akaahidi utakuwa bomba ile mbaya.

Tayari kampuni ya kubashiri ya SportPesa imeanza kufanya ukarabati katika uwanja huo.

Lakini taarifa hiyo, kwamba hadi Oktoba 28 uwanja utakuwa katika matengenezo inaonekana kuwashitua mashabiki wengi.

Tayari kumezuka mijadala kuhusiana na wapi watani hao watacheza mechi yao hiyo.

Mashabiki wengi wangependa kuona timu hizo zinacheza kwenye uwanja huo kama ilivyozoeleka.

Wengi wamekuwa wakihoji kama Uwanja wa Uhuru unaweza kuibeba mechi hiyo ana wengine wameshauri mechi ihamishiwe CCM Kirumba, Mwanza.

Lakini wako wanatania kuwa hata Chamazi itatosha na wamekuwa wakishambuliwa kuwa hawako makini katika jambo muhimu.

Bado halijawa tamko rasmi au Yanga na Simba hazijapata barua baada ya maneno ya waziri, huenda zikajadiliana na kutangaza wapi zingependa kwenda.
Share:

HAYA NDIYO MANENO YA KOCHA LWANDAMINA KWA MTIBWA

George Lwandamina
KOCHA wa mabingwa watetezi wa Ligi Kuu Tanzania Bara, Yanga, George Lwandamina, amesema kuwa mechi dhidi ya Mtibwa Sugar itakayofanyika kesho kwenye Uwanja wa Uhuru "si ndogo" kama ambavyo baadhi ya wadau wanavyoiangalia.

Akizungumza na gazeti hili jana, Lwandamina, alisema kuwa matokeo mazuri waliyonayo Mtibwa Sugar yanawasaidia kuondoa wasiwasi katika mechi itakayowakutanisha na hivyo anaamini itakuwa na changamoto zaidi kwa upande wake.

Lwandamina alisema kuwa anaamini uzoefu wa mechi za kimataifa na faida ya kucheza nyumbani ndiyo vitu anavyovitegemea kumsaidia kupata ushindi katika mchezo huo.

"Mechi dhidi ya Mtibwa Sugar ni ngumu na ya ushindani, ni moja kati ya klabu zenye wachezaji wanaojua kupambana," Lwandamina alisema kwa kifupi.

Kocha huyo wa zamani wa Zesco ya Zambia aliongeza kuwa anaamini wachezaji wake watapambana, ili wapate pointi zote tatu katika mechi hiyo na kukaa katika nafasi nzuri kwenye msimamo wa ligi.

Mzambia huyo alifurahi kuona mshambuliaji wake wa kimataifa, Amissi Tambwe, anaendelea vyema na uamuzi wa kumpanga utajulikana kesho baada ya kumaliza mazoezi.
Share:

Wednesday, 27 September 2017

STAND UNITED WAIGUSA PABAYA SIMBA

Stand United wametamba wataifunga Simba ili kuwaonyesha thamani ya wachezaji wa Kitanzania.
Mwenyekiti wa Stand United, Elson Maeja amesema wako tayari na wamepania kuwatwanga Simba ili kuwaonyesha wachezaji wa Simba.

Stand United imetoka nje ya mji wa Shinyanga na kwenda Wilayani Kahama katika eneo la Irogi kuweka kambi wakisubiri mechi yao ya Ligi Kuu Bara, Jumamosi.

“Hawa Simba wamekuwa wakisajili wachezaji wa kigeni kwa gharama kubwa. Utendaji wao hauna tofauti na wachezaji wa Kitanzania.

“Sasa tunataka kuwafunga ili waheshimu Wazalendo na waachane na kusajili wachezaji wa majimaji tu,” alisema.

Stand United wamesisitiza wanataka kuchukua pointi hizo tatu kutoka Simba ili wajiweke vizuri.
Share:

NIYONZIMA AWAVUNJA MOYO STAND UNITED

Kiungo wa Simba, Mnyarwanda, Haruna Hakizimana Fadhil Niyonzima, amesema kuwa watahakikisha wanafanya kila liwezekanalo ili kuondoka na alama tatu kwenye mchezo wao ujao wa Ligi Kuu Bara dhidi ya Stand United.
Niyonzima ameyasema hayo baada ya kuishuhudia timu yake ikitoka sare ya kufungana mabao 2-2 na Mbao FC katika mchezo wa ligi hiyo uliopigwa Alhamisi iliyopita kwenye Uwanja wa CCM Kirumba, jijini Mwanza.

Akizungumzia mchezo wao ujao ambao watacheza Jumapili ijayo dhidi ya Stand United kwenye Uwanja wa Kambarage, Shinyanga, Niyonzima amesema sare yao dhidi ya Mbao ilikuwa imepangwa hivyo sasa wanajipanga kurejesha wembe wa ushindi siku hiyo.

“Hata kama ukimleta Zidane au nani, kama Mungu ameandika droo inakuwa droo, timu yetu ni nzuri na tuliweza kufunga mabao mawili lakini tulishindwa kuyalinda japo tulitengeneza nafasi nyingi. Watu wanatakiwa kukumbuka kuwa, tupo ugenini japo tunafahamu tulitakiwa kushinda lakini hata kuipata hii pointi moja si mbaya"

Niyonzima aliendelea kufafanua kuwa
“Tunajipanga kufanya vizuri mechi ijayo kuhakikisha tunaondoka na pointi tatu, kuzikosa pointi tatu mechi iliyopita wala hakijaharibika kitu, tutafanya vizuri tu mechi ijayo,” amesema Niyonzima.

Simba kwa misimu kadhaa wamekuwa hawana matokeo mazuri katika dimba hilo la Kirumba ama wakipata matokeo ya ushindi kwa taabu wanapokutana na timu za jiji hilo tangu wakati huo wa enzi za Pamba, Toto Africans na sasa Mbao FC.
Share:

ALICHOFANYA CHIRWA CHAIKERA YANGA

Straika wa Yanga, Obrey Chirwa jana Jumanne jioni aligeuka kuwa bondia baada ya kumshambulia kwa kipigo mpigapicha John Dande wa New Habari kwenye mazoezi ya timu hiyo kwenye Uwanja wa Uhuru, ikidaiwa kukerwa kupigwa picha.

Beki Juma Abdul alifanya kazi ya ziada ya kuingilia kati na kumuokoa mpigapicha Dande alijeruhiwa na Mzambia huyo aliyeonekana kuwa na hasira huku pia mkononi akiwa ameshika mkasi wa kukatia nyasi aliotaka kumjeruhi nao Dande.
 

Tukio hilo limeripotiwa Kituo cha Polisi cha Chang'ombe, huku uongozi wa Yanga ukikaririwa kutofurahishwa na kilichofanywa na nyota wao huyo.
 

Chanzo cha mkasa huo kinaelezwa na Chirwa alikerwa na Dande baada ya wiki iliyopita kuwapiga picha wakati wa mgomo baridi wa kushinikiza walipwe mishahara yao.
Share:

Ads

Blog Archive