KATIBU wa
zamani wa Yanga, Abdul Sauko, ametamka wazi kwamba kinachotokea kwenye
klabu hiyo kwa sasa, ni matokeo ya kukosa watu wenye mapenzi ya dhati ya
kujitolea kwa moyo kama tofauti na zamani na ndio maana timu inayumba
nje ya uwanja.
Sauko aliyeshikilia nafasi mbalimbali za
ukatibu klabu hapo miaka ya nyuma, alisema katika uongozi wao
waliwatafuta matajiri na kuwajengea moyo wa kujitolea, jambo
lililoisaidia Yanga kiasi cha kutisha Afrika Mashariki na Kati mpaka
kupachikwa jina la Yanga Afrika Umoja wa Mataifa.
Alisema
bado kuna watu ambao wanaweza kutoa michango yao kwa timu, lakini
akadai baadhi ya viongozi hawajajiweka karibu na watu hao ili kuonyesha
umuhimu wao ndani ya timu na kusaidia kujitoa kwa hali na mali.
“Sisi
tuliwatafuta na kuwaweka karibu, ndiyo maana wakati ule hata pesa za
usajili tulichangishana kuhakikisha timu inafanya vizuri,” alisema Sauko
ambaye alikuwa miongoni mwa waasisi wa kundi la Yanga Family ambalo
lilikuwa mhimili wa usajili mwanzoni mwa miaka ya 2000.
“Wachezaji na wafanyakazi kwa ujumla wakitimiziwa mahitaji yao, watajituma kikamilifu.
“Mipango
ya timu ilikuwa wazi kwao, ndicho kilichokuwa kinawafanya wawe na
uchungu wa kuona inapotokea timu ikatetereka kwa masuala ya fedha,
inakuwa aibu kwao, hilo linapaswa kufanywa kwa sasa. Hata nafasi za
ujumbe ndani ya klabu zilishikwa na watu ambao walikuwa tayari kujitolea
kutatua shida ndogo ndogo. Hilo pia lilikuwa msaada kwa timu kiasi cha
kuwa na mafanikio ya hali ya juu.”
Sauko aliwataka
viongozi waliopo madarakani Yanga kwa sasa, wawasake wadhamini ambao
watabeba gharama za klabu kwa asilimia 80, watafanya wachezaji wapate
mishahara kwa wakati, wasafiri kwenda mikoani, huku asilimia 20 ya
gharama, ziwe za wanachama kujitolea, uuzwaji wa jezi pamoja na pesa za
viingilio vya timu inapofanya mazoezi.
“Ni kutengeza
mipango madhubuti, wanachama wanapenda timu zao, wapo tayari kutoa
viingilio vya mazoezi, hivyo wanaweza kupata pesa ndogo ndogo za kukidhi
mahitaji yao, naamini hilo litawapa hatua.
“Tulikuwa
tunatangaza viingilio pindi timu ikifanya mazoezi Uwanja wa Kaunda,
mashabiki walikuwa wanakuja, tena wengine kutoka mbali, hasa kipindi cha
usajili ndipo tulipata pesa zaidi kutokana na mashabiki kuwa na hamu ya
kuwaona wachezaji wapya.
“Lazima unapopanga bajeti ya
mwezi kwa klabu kama Yanga, uwe na miradi ama vyanzo vya kupata pesa,
lasivyo mipango itakuwa inaingia doa na kushindwa kufikia pale
panapotakiwa.
“Najua maneno haya hayatawafurahisha wengi lakini ndiyo ukweli.”
0 comments:
Post a Comment