Monday 28 August 2017

TSHISHIMBI AIINGIZA YANGA MATATANI

 
Ikiwa ni siku chache baada ya uongozi wa Yanga kumsajili Papy Tshishimbi, raia wa DR Congo, zengwe limeibuka.

Wakala wa aliyekuwa kiungo wa timu hiyo, Justine Zulu ‘Mkata Umeme’, Karin Nir raia wa Israel amepanga kupeleka mkataba wa mteja wake huyo katika Shirikisho la Soka la Tanzania (TFF), leo, lengo lake likiwa ni kuzuia Yanga kuendelea kumtumia.

Tshishimbi ndiye amechukua nafasi ya Zulu raia wa Zambia ameshindwana na Yanga.

Novemba, mwaka jana, Yanga iliingia mkataba wa mwaka mmoja na Zulu mbele ya wakala wake huyo raia wa Israel, lakini hivi karibuni ilitangaza kuachana na kiungo huyo kutokana na kiwango chake kutowaridhisha ambapo nafasi yake imechukuliwa na Tshishimbi.

Hata hivyo, wakala wa Zullu amesisitiza mkataba wa mteja wake umevunjwa kiholela, hivyo kitendo cha jina lake kung’olewa Yanga na nafasi yake kuchukuliwa na Tshishimbi ni haramu.

 Awali, Mkata Umeme inadaiwa alipanga kuishitaki Yanga katika Shirikisho la Soka la Kimataifa (Fifa) ili alipwe dola 100,000 (Sh milioni 221) endapo Yanga ingekataa kumrejesha kwenye timu hiyo kutokana na mkataba walioingia.

Wakala wa mchezaji huyo, tayari yupo hapa nchini tangu Ijumaa ya wiki iliyopita alipotua akitokea kwao Israel kwa ajili ya kulimaliza suala hilo lakini anadai viongozi wa Yanga wamekuwa wakigoma kupokea simu yake kwa lengo la kumalizana kwa amani hali linayomlazimu kuchukua maamuzi makubwa zaidi.
Nir amesema: “Yanga wamekatisha mkataba na mteja wangu kwa ujanjaujanja  kitu ambacho hakipo kisheria lakini pia hawataki tumalizane kwa usalama, hawataki kupokea simu yangu licha ya kuwa nipo hapa tangu Ijumaa, kesho (leo Jumatatu) nitakwenda TFF kupeleka mkataba wa Zullu ambao haujaisha maana najua sheria za hapa zinaruhusu wachezaji saba pekee wa kimataifa ndani ya timu moja.

“Najua wamemsajili mchezaji kutoka DR Congo kitu ambacho ni kinyume cha sheria kwa sababu Zulu mkataba haujaisha na nitaupeleka TFF ili  kuona Yanga ilivyowadanganya kwani katika mfumo wa TMS bado inaonyesha ni mchezaji wao, baada ya hapo nadhani Simba na Azam wataenda kulalamika TFF kwa kitendo cha Yanga kusajili wachezaji nane ili wakatwe pointi,” alisema  Nir.


Ikumbukwe Yanga ilishatangaza kuachana na mchezaji huyo kwa kukatisha mkataba wake wa mwaka mmoja.
Share:

0 comments:

Post a Comment

Ads

Blog Archive