HAKIKA vita ya wakubwa watoto wanatakiwa kukaa mbali, hivyo ndivyo
unavyoweza kusema baada ya bilionea wa Simba, Mohammed Dewji ‘Mo’,
kudaiwa kutaka kupeleka maumivu kwa mara nyingine tena makao makuu ya
Klabu ya Yanga.
Hivi karibuni, Mo aliwatibua Yanga baada ya kuikwamisha klabu hiyo kumuongezea mkataba mwingine Mnyarwanda Haruna Niyonzima na
kumshawishi kwa mamilioni ya fedha kujiunga na Simba. Inadaiwa Mo
amemwaga dola 50,000, zaidi ya Sh milioni 110 ili kumnasa Niyonzima.
Inadaiwa kuwa mbinu hiyo pia anataka kuitumia tena ili kuipora Yanga
kiungo wake mshambuliaji, Juma Mahadhi. Habari za kuaminika kutoka ndani
ya Simba ambazo Championi Jumatano limezipata zimedai
kuwa, hivi sasa uongozi wa Simba upo katika mazungumzo na Mahadhi
ukimshawishi aweze kujiunga na timu hiyo licha ya kuwa bado na mkataba
wa mwaka moja na Yanga.
“Bado tunaendelea na zoezi letu la usajili kama kawaida lakini kwa
wachezaji wa ndani tumebakiza nafasi mbili ambapo moja tunataka
kumsajili Erasto Nyoni wa Azam na tupo katika
mazungumzo naye. “Lakini pia tupo katika mazungumzo na Juma Mahadhi
wa Yanga kwani tunamtaka mchezaji huyo na mambo yakikaa sawa,
tutamsajili muda wowote kwani bosi wetu ametuambia tumuambie avunje
mkataba wake,” kilisema chanzo hicho cha habari.
Alivyoulizwa kuhusiana na suala hilo, Mahadhi alisema: “Sina chochote
cha kusema kuhusiana na hilo ila mimi bado ni mchezaji wa Yanga.”
Lakini alipotafutwa Mwenyekiti wa Kamati ya Usajili ya Simba, Zacharia
Hans Poppe ili aweze kuzungumzia usajili huo, hakupatikana kutokana na
simu yake ya mkononi kuita tu bila ya kupokelewa.
Wa kwetu huyo wadau Yanga macho yanawatoka kama nyundo.Simba oyee!
ReplyDelete