WASOMI wametaja sifa za mtu anayetakiwa kuziba nafasi ya Waziri wa Nishati na Madini ambayo ipo wazi tangu Profesa Sospeter Muhongo atumbuliwe Mei 24.
Sifa zilizotajwa na wasomi hao ni kiwango cha elimu, uadilifu na uelewa mkubwa wa sekta ya nishati na madini.
Wakizungumza na Nipashe kwa njia ya simu wiki hii, wasomi hao walisema mambo hayo yanapaswa kuzingatiwa ili kuwa na watendaji wenye weledi na watakaofanya kazi kwa kutambua kuwa wanawatumikia Watanzania.
Taarifa iliyotolewa na Kurugenzi ya Mawasiliano ya Rais, Ikulu Mei 24 ilisema Rais Magufuli ametengua uteuzi wa Prof. Muhongo na kwamba nafasi hiyo itajazwa baadaye.
Muhongo alifutwa kazi baada ya kamati iliyoundwa na Rais John Magufuli na kuongozwa na Prof. Abdulkarim Mruma kuchunguza kiwango na aina ya madini yaliyomo katika makinikia kwenye makontena 277 yaliyokamatwa katika Bandari ya Dar es Salaam Machi kuonyesha uwapo wa udanganyifu mkubwa.
Tangu wakati huo nafasi hiyo imeendelea kuwa wazi.
Mhadhiri wa Chuo Kikuu cha Dar es Salaam (UDSM), Dk. Bashiru Ally, alisema hakubaliani na dhana kuwa nafasi za uongozi za uteuzi na wabunge hazitakiwi kuangalia suala la taaluma ya muhusika.
Alisema ni lazima kigezo cha elimu kikaangaliwa kwa watu wanaopewa nafasi hizo ili kuwa na watu walioelimika vya kutosha kwa muhimili muhimu wa taifa.
"Elimu ni jambo la msingi sana," alisema Dk. Ally kwa sababu "kama isingekuwa muhimu maana yake kusingekuwa na haja ya kusomesha watoto wetu wala kuweka msisitizo kwenye masuala ya kielimu."
"Wateule lazima wawe na sifa ya kielimu, pia uadilifu na uwezo wa kufanya kazi za umma bila uchoyo, ubinafsi na ubaguzi kwa kugeuza ofisi kama maeneo yao ya nyumbani ambayo wanaweza kujifanyia watakayo."
Dk. Ally alisema uzoefu unaonyesha kuwa huko nyuma viongozi hugeuza ofisi za umma kichaka cha 'kupiga dili' na kuingiza serikali kwenye hasara.
Aidha, alisema mrithi wa Prof. Muhongo atapaswa kuwa mwenye uwezo mkubwa na uelewa wa sekta hiyo; hasa kwa kuzingatia kwa sasa kuna sheria mpya za madini zilizotungwa na Bunge.
"Nafasi hii inapaswa kujazwa na mtu mwenye sifa za uelewa katika sekta husika, awe na uwezo na ujasiri wa kutekeleza masuala hayo muhimu kwenye sekta hiyo."
KASI YAKE
Mhadhiri Mwandamizi wa UDSM, Dk. Benson Bana alisema mtu atakayeteuliwa na Rais Magufuli kuwa Waziri wa Nishati na Madini ni vyema asitoke nje ya Baraza la Mawaziri la sasa kwa kuwa tayari ameshawafahamu vya kutosha jinsi wanavyoweza kuendana na kasi yake katika serikali ya awamu ya tano.
Prof. Muhongo amepotea katika hadhara tangu kutumbuliwa kwake na hakuhudhuria vikao vya Bunge la bajeti kwa wiki tano mfululizo.
Mbunge huyo wa Musoma Vijijini (CCM) aliiambia Nipashe mwezi uliopita, hata hivyo, kuwa hahudhurii vikao vya Bunge kwa kuwa yuko mapumzikoni.
Aliongeza kuwa kipindi hiki hataki malumbano na hahusiki na mikataba mibovu ya madini ambayo kwa sasa 'imeteka' vinywa vya Watanzania wengi wakiwamo wabunge.
"... Muhongo yuko mapumzikoni. Hataki malumbano na hahusiki na mikataba yote hiyo," aliandika ujumbe mfupi kwa Nipashe.
Ripoti ya kamati ya Prof. Mruma ilionyesha nchi imekuwa ikipoteza wastani wa kati ya Sh. bilioni 829 mpaka Sh. trilioni 1.44 kwa mwezi katika usafirishaji wa makinikia yaliyokuwa yakipelekwa kuchenjuliwa nje ya nchi na kampuni ya Acacia.
Rais Magufuli alilaumu Prof. Muhongo kwa kushindwa kuchukua hatua dhidi ya udanganyifu huo wa mabilioni ya fedha kupitia mchanga huo wa dhahabu.
Machi 23, Rais Magufuli alifanya ziara ya kushtukiza katika Bandari ya Dar es Salaam na kukuta makontena 20 yakiwa mbioni kusafirishwa, kinyume cha maelekezo yake ya Machi 2, ya kuzuia usafirishaji wa mchanga huo nje.
Baada ya ziara hiyo, makontena zaidi yalikamatwa yakiwa katika bandari kavu na maeneo mbalimbali nchini na kufikia 277.
0 comments:
Post a Comment