Monday 28 August 2017

SIMBA, YANGA ZATIKISA REKODI UHURU

 
Mzunguko wa kwanza wa Ligi Kuu umemalizika jana Jumapili na kushudia mabao 19 yakifungwa katika viwanja wa nane huku Uwanja wa Uhuru pekee ukizalisha mabao tisa.
Uwanja wa Uhuru umezalisha mabao tisa sawa na asilimia 47 ya magoli yaliyofungwa kwenye viwanja vyote. Uwanja huo ulitumika kwa mechi mbili ambapo Simba ilichakaza Ruvu Shooting, Jumamosi iliyopita kwa mabao 7-0, wakati Jumapili Yanga ilibanwa mbavu na Lipuli kwa kutoka sare ya bao 1-1.
Uwanja wa Sabasaba ulizalisha mabao matatu sawa na asilimia 15, wakati Prisons ikiichapa Njombe Mji kwa mabao 2-1 na Mwadui Complex pia ulizalisha magoli matatu sawa na asilimia 15 ya magoli yote yaliyofungwa mwishoni mwa wiki wakati Mwadui ikiitandika Singida United kwa mabao 2-1.
Uwanja wa Manungu Complex ulizalisha bao moja wakati Mtibwa ikiichapa Stand United bao 1-0. Matokeo kama hayo yalipatikana katika Uwanja wa Nangwanda Sijaona pale Azam ilipoifunga Ndanda bao 1-0 na pia kwenye Uwanja wa Sokoine ambapo Mbeya City iliilaza Majimaji kwa bao 1-0.
Maoni ya wadau
Kocha Msaidi wa Mwadui, Khalid Adam alisema ni mapema kusema ligi ya msimu huu, itakuwa na mabao mengi.
“Ni mwanzo, timu zimejiandaa lakini unapoingia uwanjani inategemea unakutana na mpinzani wa namna gani. Usipokuwa makini utafungwa mabao mengi,”alisema Khalid.
Katibu Mkuu wa Prisons, Havinitishi Abdallah alisema uzoefu una nafasi kubwa ya kuamua matokeo ya baadhi ya timu zinazoshiriki Ligi Kuu.
“Ukiangalia Simba na Yanga zina wachezaji wazuri mfano Okwi na Ngoma ambao wanaweza kukufunga muda wowote, kikibwa ni timu kujiandaa na kutoa ushindani,”alisema Abdallah aliyewahi kuwa mchezaji wa Prisons.
Share:

0 comments:

Post a Comment

Ads

Blog Archive