Friday, 29 September 2017

AJIBU APINDUA REKODI YA SIMBA

STRAIKA mpya wa Yanga, Ibrahim Ajibu, amefanikiwa kuipindua rekodi yake ya mabao kwa msimu uliopita alipokuwa akiitumikia Simba baada ya kucheza mechi nne za awali.

Ajibu ambaye ni zao la Simba, amejiunga na Yanga msimu huu baada ya kumaliza mkataba wake na Simba.

Katika msimu wake wa kwanza ndani ya Simba akicheza kikosi cha wakubwa ambao ulikuwa ni 2015/16, mshambuliaji huyo alionyesha uwezo mkubwa katika mechi nne za kwanza lakini hakuweza kufunga bao lolote ambapo mechi tatu za kwanza zote walitoka sare ya mabao 2-2 dhidi ya Costal Union, Polisi Moro(1-1), Stand United (2-2) na suluhu na Yanga.

Msimu uliopita ambao ni 2016/17, mshambuliaji huyo hakuweza kufunga bao lolote katika mechi nne za kwanza kabla ya kuibuka katika mechi yao dhidi ya Majimaji akifunga mabao matatu kwenye ushindi wa mabao 6-1.

Msimu wake wa kwanza ndani ya Yanga, tayari Ajibu ameshafunga mabao mawili kwenye mechi nne alizocheza. Mabao yake hayo yameipa Yanga pointi sita kwani kila alipofunga timu hiyo imeibuka na ushindi wa bao 1-0.

Ajibu alifunga bao la kwanza msimu huu katika mchezo dhidi ya Njombe Mji na kuweza kuipa ushindi timu yake wa bao 1-0 kabla ya kufunga tena katika mchezo dhidi ya Ndanda FC na kuibuka na ushindi kama huo, ameshindwa kufunga dhidi ya Lipuli FC na Majimaji SC.

Wakati huohuo, beki kisiki wa Yanga, Nadir Haroub ‘Cannavaro’ ameibuka na kusema kuwa kiwango kinachoonyeshwa na Ajib ni habari nyingine katika kikosi chao na kudai kuwa ana matumaini makubwa ya mchezaji huyo kuwa tegemeo katika kikosi chao.

Akizungumza na gazeti hili, Cannavaro amesema kuwa, hakuna asiyefahamu uwezo wa Ajibu, hivyo mabao anayoyafunga ni mwanzo mzuri kwao kuona atakuwa tegemeo katika kikosi hicho msimu huu.

“Ajibu ni mshambuliaji mzuri na ameonyesha kasi nzuri hivyo naamini ushirikiano wake pamoja na washambuliaji wengine utasaidia kuifanya timu yetu iweze kufanya vizuri kwenye ligi,” alisema Cannavaro.
Share:

0 comments:

Post a Comment

Ads

Blog Archive