OFISI ya Bunge imesema Kiongozi wa Kambi ya Rasmi ya Upinzani Bungeni, Freeman Mbowe hajanyang’anywa gari.
Taarifa iliyotolewa na Bunge leo
Alhamisi imesema kilichotokea ni kwamba, gari hilo limerudishwa nchini
ili dereva afuate utaratibu wa kupata kibali cha kusafiri nje ya nchi.
Mbowe yuko Nairobi nchini Kenya ambako
Mbunge wa Singida Mashariki, Tundu Lissu anaendelea na matibabu baada ya
kushambuliwa na kujeruhiwa kwa risasi Septemba 7 akiwa nyumbani kwake
Area D mjini Dodoma.
Bunge limesema ni kweli gari lenye
namba ya usajili STL 4587 aina ya Toyota Prado limetengwa maalumu kwa
ajili ya kumuhudumia Kiongozi wa Kambi Rasmi ya Upinzani Bungeni katika
kutekeleza majukumu yake ya kikazi na binafsi nchini.
“Kiongozi wa Kambi Rasmi ya Upinzani
Bungeni aliomba gari ikamhudumie mjini Nairobi nchini Kenya na Ofisi ya
Bunge iliridhia ombi hilo na kuomba taratibu zizingatiwe. Hata hivyo,
ofisi iligundua kwamba gari ilikwenda Nairobi na dereva hakupata kibali
cha kusafiri nje ya nchi ambacho kila mtumishi wa umma anayesafiri nje
ya nchi lazima apate kibali hicho kutoka kwa Katibu Mkuu Kiongozi,”
imesema taarifa ya Bunge.
Bunge katika taarifa hiyo limesema kwa
kuwa utaratibu haukukamilika, dereva aliambiwa alirejeshe gari hilo
nchini na kuliegesha katika Ofisi ya Mkuu wa Mkoa wa Arusha hadi
utaratibu mwingine utakapokamilika.
“Dereva yupo Dodoma anakamilisha
taratibu ili ofisi iweze kumuombea kibali Ikulu ndipo anaweza kurejea
nchini Kenya kwa ajili ya kuendelea kumhudumia Kiongozi wa Kambi Rasmi
ya Upinzani Bungeni,” imesema taarifa.
Ofisi ya Bunge imesema inasikitishwa
kutokana na utaratibu unaotumiwa na Ofisi ya Kiongozi wa Kambi Rasmi ya
Upinzani Bungeni wa kuzungumzia masuala yanayohusu ofisi hiyo kupitia
kwa msemaji wa chama kama inavyoonekana kwenye mitandao ya kijamii
akitoa malalamiko kwa niaba ya ofisi hiyo.
“Ni vyema ikaeleweka kwamba Ofisi ya
Kiongozi wa Kambi Rasmi ya Upinzani Bungeni ni kama ofisi nyingine
zinazohudumiwa na Sekretarieti ya Bunge ambayo inapaswa kufuata kanuni
na taratibu za uendeshaji wa Ofisi na ni kosa kwa mtumishi kwenda
kinyume na masharti ya Utumishi wa Umma,” taarifa hiyo imesema.
Imeelezwa katika taarifa kuwa ni
dhamira ya Ofisi ya Bunge kuendelea kumhudumia Kiongozi wa Kambi Rasmi
ya Upinzani Bungeni kwa kufuata misingi na kanuni za utumishi wa umma na
zile za Bunge bila kuchanganya na siasa.
“Ofisi ya Bunge inauhakikishia umma
kuwa taratibu zikishakamilika Kiongozi wa Kambi Rasmi ya Upinzani
Bungeni ataendelea kuhudumiwa popote atakapokuwa,” imesema taarifa hiyo.
0 comments:
Post a Comment