Mbunge
wa Kilombero, Peter Lijualikali na viongozi watatu wa Chadema wilayani
Malinyi wanashikiliwa na polisi kwa tuhuma za kufanya kusanyiko lisilo
halali.
Mbunge huyo amekamatwa leo Alhamisi saa
12:40 jioni akitoka kwenye kikao cha ndani cha chama hicho
kilichofanyika katika Kijiji cha Makerere wilayani Malinyi.
Akizungumzia kukamatwa kwa viongozi
hao, Mwenyekiti wa Chadema Kanda ya Kati, Alfonce Mbassa amesema baada
ya kumaliza kikao, mbunge huyo na viongozi wengine walipanda kwenye
magari ili kuondoka lakini ghafla lilitokea gari la polisi na askari
walimuamuru Lijualikali ashuke.
“Tulishuka wote kujua tatizo ni nini
lakini askari walimhoji Lijualikali kwa nini amekwenda kufanya siasa
Malinyi wakati yeye ni mbunge wa Kilombero,” amesema Mbassa.
Amesema walijaribu kuwaelewesha polisi
kwamba kilikuwa ni kikao cha ndani lakini askari walisisitiza kuwa
lilikuwa kusanyiko lisilo halali.
Amewataja waliokamatwa pamoja na mbunge
huyo kuwa ni Mwenyekiti wa Chadema Malinyi, Emmanuel Lukindo; Katibu
wake, Sadi Lyampawe na Katibu wa Uenezi wa wilaya, Lucas Lyambalimu.
“Lakini tulivyowabana polisi wametuambia wameelekezwa na Mkuu wa Wilaya ya Malinyi, Majura Kasika kuwakamata,” amesema Mbassa.
Alipotakiwa kuzungumzia tuhuma hizo,
mkuu wa wilaya Kasika amesema ni kweli ameagiza polisi kumkamata mbunge
huyo kwa kuwa anafanya siasa nje ya jimbo lake.
“Ndiyo, nimetoa maelekezo akamatwe
maana hakuna mbunge anayeruhusiwa kufanya siasa nje ya jimbo lake na
tunaendelea kumshikilia kwa mahojiano,” amesema Kasika.
Kaimu Kamanda wa Polisi Mkoa wa Morogoro, Leons Rwegasira amesema hajapata taarifa za kukamatwa kwa mbunge huyo.
“Nipe muda nifuatilie nitakujulisha maana bado sijapata taarifa za kukamatwa kwa mbunge huyo,” amesema Rwegasira.
0 comments:
Post a Comment