KIUNGO wa Simba, Mnyarwanda, Haruna Niyonzima, ameweka wazi kuwa
endapo timu yake hiyo itaibuka na ushindi kwenye mchezo wao dhidi ya
Yanga, basi atashangilia.
Niyonzima ambaye alijiunga na Simba mwanzoni mwa msimu huu akitokea
Yanga, amebainisha hilo ikiwa ni siku chache kabla timu hizo
hazijakutana.
Oktoba 28, mwaka huu ni siku ambayo Yanga na Simba zinatarajiwa
kupambana kwenye mchezo wa Ligi Kuu Bara utakaopigwa katika Uwanja wa
Uhuru jijini Dar.
Akizungumza na moja ya vyombo vya habari hapa nchini, Niyonzima alisema
mchezo baina ya Simba na Yanga siku zote huwa ni mgumu, lakini
ameonyesha dhamira yake ya kushangilia bila ya kuhofia chochote ikitokea
wao wamepata ushindi na kama yeye akifunga.
“Hakuna asiyejua ugumu wa mechi baina ya Simba na Yanga, katika mechi
zinazokuwa na kukamiana kwingi ni hizo, hivyo nitafurahi kama tukipata
pointi tatu dhidi yao au nikifunga nitashangilia japokuwa itakuwa
kiungwana siyo kwa nyodo na dharau.
“Zaidi naomba siku tukikutana tupate pointi tatu tu maana ndiyo kitu
cha muhimu kwetu, ili tuweze kufikia mafanikio yetu ya kutwaa ubingwa wa
ligi msimu huu, ni lazima tupate pointi tukicheza na Yanga, Azam na
Singida United.
“Hizi ndizo timu kubwa kwa sasa na ndiyo ambazo naona zina upinzani
mkubwa kwetu, hivyo ili upate ubingwa kwa sasa ni muhimu pia uhakikishe
unapata pointi katika timu hizo,” alisema Niyonzima.
0 comments:
Post a Comment