Mshambuliaji wa Yanga, Ibrahim Ajibu akikabidhiwa jezi namba kumi wakati alipojiunga na klabu ya Yanga.
WAKATI kivumbi cha Ligi Kuu Bara kikizidi kupamba moto, baadhi ya
mashabiki wa timu ya Simba juzi Jumamosi walijikuta wakiingia katika
mvutano mkubwa na kutaka kushushiana makonde kuhusiana na mshambuliaji
wa Yanga, Ibrahim Ajibu.
Mvutano huo ulitokea katika Uwanja wa Uhuru jijini Dar wakati Ajibu
alipokuwa akiitumikia Yanga dhidi ya Mtibwa Sugar katika mchezo
uliomalizika bila ya kufungana.
Wakati mechi hiyo ikiendelea, mmoja wa mashabiki wa Simba ambaye jina
lake halikuweza kujulikana, aliyekuwa uwanjani hapo akiiunga mkono
Mtibwa Sugar, alidai kuwa katika usajili bora ambao Yanga wananufaika
nao msimu huu ni ule wa Ajibu.
Alisema kuwa tangu ajibu ajiunge na Yanga amebadilika na sasa
anacheza soka la uhakika tofauti na alivyokuwa Simba msimu uliopita na
mabao yake yameweza kuisaidia Yanga kupata pointi sita lakini wao
wamepata hasara kwa kumsajili, Mnyarwanda Haruna Niyonzima akitokea
Yanga kwa madai kuwa hakuna chochote alichokifanya mpaka sasa tangu
ajiunge na timu hiyo.
Kauli hiyo uliungwa mkono na mashabiki wengi wa Simba waliokuwa
uwanjani hapo lakini ikapingwa vikali na wachache wakidai kuwa Niyonzima
ni mchezaji mzuri lakini kocha wao mkuu, Mcameroon, Joseph Omog bado
hajajua kumtumia, ndiyo maana anaonekana hana msaada katika timu hiyo.
Hali hiyo ilizua mzozo mkubwa uliosababisha mashabiki hao kutaka
kutwangana makonde. Hata hivyo, tangu Ajibu ajiunge na Yanga amefanikiwa
kuifungia timu hiyo mabao mawili mpaka sasa kati na manne ambayo
imefunga lakini Niyonzima hana bao lolote, ingawa yeye anacheza nafasi
ya kiungo.
0 comments:
Post a Comment