![]() |
Yusuf Manji |
MAMALAKA ya Mapato Tanzania (TRA)
imezifunga ofisi za kampuni ya mfanyabiashara Yusufu Manji kutokana na
kudaiwa Sh 12.2 bilioni.
Akizungumza leo Jumatatu jioni,
Mkurugenzi wa Huduma na Elimu kwa Mlipakodi, Richard Kayombo amesema
wamekuwa na mawasiliano na kampuni ya Farm Equpment ambayo inamilikiwa
na Manji tangu Agosti 15 mwaka huu lakini kulikuwa hakuna mrejesho
kuhusu deni hilo.
Kutokana na hilo amesema wamefunga
ofisi zake kwa sababu kampuni hiyo inadaiwa kiasi cha Sh 12.2 bilioni
lakini kampuni hiyo ina nafasi ya kuendelea kuwasiliana na TRA namna ya
kulipa deni hilo.
Tukio hilo limetokea leo Jumatatu kati
ya saa 4 hadi 7 wakati TRA na kampuni ya udalali ya Yono wakiambatana
na polisi walipokwenda katika jengo hilo lililopo barabara ya Pugu,
wilayani Temeke.
Baadhi ya mashuhuda wakiwamo walinzi
kwa masharti ya kutotaja majina yao wameiambia Mwananchi kuwa ofisi
zilizofungwa ni ya Manji na sehemu yake duka la kuuza pikipiki na
matrekta.
Wamesema baada ya kufika watu
waliingia moja kwa moja katika ofisi yake kisha kufanya majadiliano na
wahusika yaliyodumu zaidi ya saa 2.
“Nadhani hawakufikiana mwafaka kwa
sababu walivyotoka wakaamuru wafanyakazi wa ofisi hiyo kutoka nje kisha
kuweka utepe wa rangi nyekundu na nyeupe,” amesema shuhuda huyo.
Hata hivyo, mashuhuda hao wamesema
hawajui tatizo ni nini lakini waliwasikia maofisa wa TRA na kampuni hiyo
ya udalali wakizungumza kuhusu kodi.
0 comments:
Post a Comment