Jengo la Freemason liliopo Dar es Salaam, ambalo ndio la
kwanza kabisa kutumiwa na Bunge la Tanganyika.
WATU wengi wanazungumzia kuhusu
imani ya kundi la Freemason, huku baadhi wakihofu kuingia kwenye hekalu lao
lililoko mjini Posta jijini Dar es Salaam, mwandishi wa Jibu la Maisha Denis
Massawe, ameingia humo na hapa anaeleza alichokikuta.
Kama kuna jambo la kijasiri
nililowahi kufanya ambalo sitalisahau maishani ni pamoja na maamuzi ya kuingia
ndani ya hekalu la Freemason lililoko mtaa wa Ohio mjini Posta jijini Dar es
Salaam.
Nasema ni la kijasiri kwa sababu,
nilipoanza safari yangu kutoka Ubungo kuelekea kwenye jengo hilo kichwani
nilikuwa na maswali mengi yasiyo na majibu sahihi yaliyotokana na habari nyingi
mbaya zinazoandikwa na picha za kutisha zinazohusu kundi hilo.
Lengo kubwa la safari yangu ilikuwa
ni kujionea mwenyewe kwa macho yangu
shughuli zinazoendelea ndani ya jengo hilo, na kupata uhakika ili nisiwe
mtu wa kusimuliwa tu.
Safari yangu ilafanyika siku moja
baada ya kuzikwa kwa kiongozi wao mkuu mstaafu wa kundi hilo Andrew Chande
aliyefariki dunia hivi karibuni.
Pamoja na mambo mengine ya kitafiti
niliyohitaji kujua pia nilitaka kufahamu
walipokeaje pole za Viongozi wa dini mbalimbali kufuatia kifo cha
kiongozi wao Sir. Chande, ambae alifariki akiwa Nairobi nchini Kenya.
Licha ya kuwa na ujasiri mkubwa juu
ya kutaka kuyafahamu hayo yote tena nikiwa kwenye eneo husika, lakini pia nilijawa na hofu juu ya kile
nilichohisi ‘kutolewa kafara’.
Nakumbuka siku moja kabla ya kufika
katika jengo la ‘Freemason Hall’ nilipitia kwenye ofisi za Idara ya habari
Maelezo mjini Posta, ambapo waandishi huwa na kawaida ya kukutana kwa lengo la
kupeana vyanzo vya habari.
Nilichohitaji kwao ni walau nijue kama kuna
mwandishi aliyewahi kuingia katika jengo hilo.
Nilipofika Maelezo nilimkuta rafiki
yangu ambae ni mwandishi wa gazeti la Jambo leo (jina namhifadhi), nikamuuliza
hivi, ulishawahi kuingia kwenye jengo la Freemason Hall?’ Ghafla nilishangaa
kuona jinsi alivyoshitushwa na swali hilo!
Akanijibu ‘wewe, unataka kwenda huko’ nilimjibu ndiyo.
Akaniambia, wewe, ukienda huko ukirudi hapa
ukiwa mzima basi nitajua kuwa ni mwanamume kweli. Akaendelea kunijuza, na ujue
kuwa pale kuna njia ya chini kwa chini kutoka hotel ya Kilimanjaro maarufu
Kempisk, hadi katika jengo hilo.
Rafiki yangu huyo alinikanya na
kunipa angalizo akisema, angalia wasije kukupoteza. Kwakweli kwa maneno ya rafiki huyo japo yalizidi
kunitia hofu lakini hayakukata kiu yangu ya kwenda kutafiti niliyoyataka kwenye
jengo hilo.
Baada ya kusikia nasaha hizo za
rafiki huyo, ndipo nikaendelea na safari yangu lakini nilipofika katika ubalozi
wa Zambia..Itaendelea kesho
0 comments:
Post a Comment