Jidenna Theodore Mobisson.
“I’M a classic man, you can be mean when you look this clean, I’m a
classic man…” (Mimi ni mwanaume wa kiwango cha juu, utakuwa na maana
kama ukiwa msafi kama hivi…) hicho ni kibwagizo cha wimbo wa Classic Man,
uliomtambulisha Jidenna Theodore Mobisson katika ulimwengu wa muziki wa
Hip Hop, mwanzoni mwa mwaka 2015.
Kabla ya hapo, hakuna aliyekuwa anamjua Jidenna na baada ya kuachia
ngoma yake hiyo ya kwanza, alifanikiwa kutinga kwenye nafasi ya 49
kwenye chati kubwa ya muziki ya Billboard na kumpatia tuzo ya
mwanamuziki bora anayechipukia ya Soul Train Music Awards nchini
Marekani.
Aliteuliwa pia kuwania tuzo ya msanii bora chipukizi kwenye Grammy
Awards ingawa hakushinda, baadaye mwaka huu, 2017 akaachia ngoma
nyingine ambayo inakimbiza sana kwa sasa, Bambi (My Dear). Baada ya
kuachia Classic Man, Jidenna alianza ku-make headlines, hasa kutokana na
utanashati wa hali ya juu aliouonesha kwenye video ya wimbo huo na
kilichokuja kuwashangaza wengi, ni pale mwenyewe alipofunguka kwamba
chimbuko lake ni nchini Nigeria.
Jidenna Theodore Mobisson.
Licha ya kueleza kwamba asili yake ni Nigeria, kuna kitu kilionekana
kutokuwa sawa kwa Jidenna kwani mara kwa mara alikuwa akiizungumzia
vibaya nchi yake kwenye mitandao ya kijamii, akitoa matamshi ambayo
yalionesha kuwakera sana mashabiki wake wa nchini Nigeria, na hapo ndipo
alipoamua kumwaga nyongo.
Katika mahojiano na VLAD TV, Jidenna ambaye baba yake, Oliver
Mobisson alikuwa Mnigeria mweusi kutoka kabila la Igbo, akiwa ni Profesa
wa Sayansi ya Kompyuta katika Chuo Kikuu cha Enugu, Nigeria, na mama
yake, Tama Mobisson akiwa ni Mmarekani mweupe, alifunguka kwamba
kutokana na rangi ya ngozi yake (chotara wa Kizungu na Kinigeria),
amewahi kupigwa risasi ya mguu akiwa na umri wa miaka mitano.
Si kupigwa risasi tu bali pia mama yake alipigwa vibaya mbele ya
macho yake na baba yake akaporwa kiwango kikubwa cha fedha na majambazi,
kipindi hicho wakiwa wanaishi nchini Nigeria. Shambulio hilo,
lilisababisha baba yake kuamua kuhamishia makazi yake nchini Marekani,
katika Mji wa Norwood, Massachusetts kwa ajili ya usalama wa familia
yake na huko ndiko alikokulia na baadaye alipoanza kujitegemea, alihamia
Brooklyn, New York anakoishi hadi leo.
Jidenna Theodore Mobisson.
“Rangi yangu nyeupe, na asili ya Kizungu ya mama yangu, vilisababisha
tunusurike kuuawa. Ukiwa mweupe Nigeria, unaonekana una fedha, na kwa
sababu watu wengi ni maskini, unakuwa kwenye hatari ya kuvamiwa, kutekwa
na kuuawa muda wowote na majambazi na makundi ya kigaidi, hicho ndicho
kilichotokea kwangu,” alikaririwa Jidenna.
Akaendelea kufunguka kwamba, hata baada ya baba yake mzazi kufariki
nchini Marekani kwa ugonjwa wa shambulio la moyo, suala la kurudi
kumzika nchini Nigeria, lilikuwa mtihani mkubwa kwa wanafamilia. “Kwa
kuwa familia yetu wote ni weupe isipokuwa baba, wakati wa kwenda kumzika
baba nyumbani, tulilazimika kukodi bunduki nyingi za AK-47 na makomando
kwa ajili ya ulinzi wakati wote wa mazishi, walitulinda kuanzia mwanzo
mpaka tulipomaliza na kurejea nchini Marekani,” alisema.
Jidenna mwenye umri wa miaka 31, anasema licha ya yote yaliyotokea,
bado anajivunia asili yake ya Nigeria na mashabiki wake wanapaswa
kumuelewa kwamba kuna muda huwa kumbukumbu za kuumiza zinamjia ndani ya
kichwa chake na kusababisha atoe maneno makali kuhusu nchi hiyo.
Jidenna Theodore Mobisson.
Katika video ya Bambi iliyopo kwenye albamu yake ya kwanza ya The
Chief, Jidenna amemtumia mwanadada wa Nigeria, Megalyn Echikunwoke
ambaye amecheza nafasi ya mpenzi wake aliyeamua kumsaliti na kwenda
kuolewa na mwanaume mwingine, tena mweusi, Jay Ellis ambaye pia ni
Mnigeria.
“Sina kinyongo na Nigeria na ndiyo maana hata kwenye video zangu
nawatumia Wanigeria,” alisema Jidenna ambaye utanashati wake kwenye
video zake na maisha ya kila siku, umempa umaarufu mkubwa.
0 comments:
Post a Comment