KAMA unafikiri kupata
shahada (digrii) ni kazi ngumu, tangu sasa fahamu kwamba Profesa V.N.
Parthiban anayefundisha jijini Chennai, India, ana shahada 145
alizozipata katika kipindi cha miaka 30!
Si hivyo tu, jamaa huyo
bado ana mipango ya kujiendeleza kielimu. Safari ya Parthiban ilianza
wakati anasomea shahada yake ya kwanza ambapo alikuwa anachanganya mambo
katika masomo yake ya majaribio, na hivyo kujikuta akifanya vibaya
katika mitihani na miradi muhimu chuoni.
Baada ya kuhitimu,
alipata kazi katika Idara ya Mahakama, lakini dhamira ya kujiendeleza
ilibakia palepale. Akiwa amevutiwa na masomo ya fani mbalimbali za
masomo chuoni, Parthiban aliamua kurejea chuoni ambako alipata shahada
ya pili, ya tatu na kisha akaongeza zingine 142.
Katika mahojiano yake na
jarida la Sunday Indian, msomi huyo anasema: “Nilianza kutuma maombi
katika vyuo ambavyo havikuhitaji cheti cha uhamisho katika usajili ili
niweze kusoma kozi mbalimbali wakati mmoja. Katika miaka thelathini
iliyopita nimekuwa najiandaa mfululizo kufanya mitihani na kutuma maombi
ya kozi za shahada na stashahada (diploma).”
Orodha ya mafanikio ya
Parthiban inajumuisha shahada za uzamili (master) katika masomo
yafuatayo: shahada tatu za sayansi, shahada nane za sheria, shahada nane
za biashara, shahada tisa za utawala katika biashara, shahada 10 za
sanaa, na shahada 12 za utafiti mbalimbali. Alipoulizwa iwapo kuna somo
ambalo hapendi kulisomea, Parthiban alijibu moja kwa moja kwamba ni
“hisabati”.
Kwa bahati mbaya,
kumekuweko na athari kadhaa za kusoma kwa muda mrefu kwa upande wa
Parthiban. Kusoma sana kumeathiri kumbukumbu za Parthiban kwani hivi
sasa ana matatizo ya kukumbuka sura za watu na njia ambazo amezipita kwa
muda mrefu.
Hata hivyo, matatizo
hayo hayajamkatisha tamaa mtu huyo msomi mwenye umri wa miaka 56 bado
anafanya uhadhiri katika masomo mbalimbali katika vyuo. Mbali na
shughuli zake za kisomi, Parthiban ana familia – mke na watoto wawili —
ambapo nao wamejikita katika masomo kama alivyofanya.
Mke wake hadi sasa ana
shahada tisa, hivyo anahitaji zingine 136 ili amfikie mumewe. Dhamira ya
V.N. Parthiban inawakumbusha walimwengu jina la Luciano Baietti, ambaye
anashikilia rekodi ya dunia ya kuwa mtu mwenye idadi kubwa zaidi ya
shahada za vyuo vikuu.
0 comments:
Post a Comment