MWENYEKITI wa zamani wa Simba, Mzee Hassan Dalali ameibuka na
kufunguka kuwa kamati ya usajili ya timu hiyo haikukosea kumsajili tena
mshambuliaji Mganda, Emmanuel Okwi kutokana na kuonyesha bado ni mashine
hatari licha ya kubezwa na wapinzani wao Yanga kwa kumuita mhenga.
Okwi amejiunga na Simba kwa mkataba wa miaka miwili akitokea SC Villa
ya Uganda, kabla ya hapo alikuwa akiitumikia Klabu ya Sonderjysk ya
nchini Denmark.
Tayari mshambuliaji huyo ameshafikisha mabao sita katika mechi mbili
za ligi alizocheza mpaka sasa ikiwa ni wastani wa mabao matatu kwa kila
mechi huku akijinyakulia Tuzo ya Mchezaji Bora wa Agosti.
Akizungumza na Championi Jumatano, Mzee Dalali
alisema kwa upande wake bado anaona Okwi bado ni hatari kutokana na
kufunga mabao sita hivyo hafanani na kuitwa mhenga kwa kuwa ubora wake
umekuwa ukionekana.
“Simba ya msimu huu kiukweli ni nzuri, nawapongeza kamati ya usajili
kwa kujaribu kuleta uwiano ambao mashabiki na wanachama wa Simba
walikuwa wakiuhitaji siku nyingi na suala la Okwi kuitwa mhenga hilo
haliwezi kutupa shida kwa sababu kitu cha msingi ni kwamba bado mashine.
“Unajua wakati nilipokuwa mwenyekiti ndiyo tulimsajili Okwi mwaka
2009 akiwa kijana mdogo sasa huo uzee wanaousema wapinzani wetu umeanza
lini labda kwa kuwa amecheza ligi ya hapa kwa muda mrefu.
“Lakini bado ni mchezaji hatari kwa sababu hata wao ukiangalia safari
hii timu yao haitishi kabisa ipo kama tunda la shokishoki yaani lina
miba mingi lakini haichomi,” alisema Mzee Dalali.
0 comments:
Post a Comment