Soka mbinu,
hicho ndicho kinachosubiliwa kesho wakati makocha wa Yanga, Geogre
Lwandamina na mwenzake wa Simba, Joseph Omog jinsi watakavyowatumia
wachezaji wao kwa makini katika kuhakikisha wanaondoka na ushindi katika
mchezo huo wa Ngao ya Jamii utakaofanyika kwenye Uwanja wa Taifa, Dar
es Salaam.
Moja ya sifa ya kocha ni jinsi anavyoweza
kuwatumia wachezaji wake wa akiba kuingia kubadilisha mchezo na
kuisaidia timu kupata ushindi.
Kama wewe ni shabiki
basi ondoa shaka unapowaona wachezaji hawa wameanzia benchi kwani
wanapoingia huenda wakabadilisha taswira ya mchezo pindi wakitokea
benchi kwa timu zote mbili iwapo baadhi ya nyota watakaoanza kwenye
kikosi cha kwanza watashindwa kufanya vyema.
Donald Ngoma
Anapewa
nafasi kubwa ya kuanza katika mchezo wa kesho Jumatano dhidi ya Simba,
lakini kutokana na hazina ya washambuliaji ambayo Yanga inayo, Ngoma
anaweza kuanza kama mchezaji wa akiba.
Kutokana na
uwezo wake mkubwa wa kusoma mabeki wa timu pinzani na kazi aliyonayo, ni
wazi kuwa kama ataanzia benchi mechi ya Jumatano, anaweza kuwa tatizo
kwa Simba.
Amissi Tambwe
Uwezo
wake wa kuamua mechi akiingia kutokea benchi ulijidhihirisha msimu
uliopita katika mechi ambayo Yanga iliibuka na ushindi wa mabao 4-0
dhidi ya JKT Ruvu.
Katika mchezo huo, Tambwe aliingia na kuifungia Yanga mabao mawili huku mengine yakifungwa na Saimon Msuva na Obrey Chirwa.
Juma Abdul
Ni
beki lakini ni mmoja wa wachezaji wanaoweza vyema kubadilisha mechi
pindi wanapoingia kutokea benchi hasa pale timu inaposaka matokeo.
Msimu
uliopita, beki huyo aliingia akitokea benchi kwenye mechi dhidi ya Toto
Africans ambayo Yanga walikuwa wanahitaji ushindi ili wajiweke kwenye
mazingira mazuri ya kutwaa ubingwa.
Beki huyo sio tu aliiamsha Yanga bali ndiye aliyepiga krosi iliyozaa bao la ushindi kupitia kwa Amiss Tambwe.
Ibrahim Ajib
Uwezekano
mkubwa uliopo ni Ajib kuanzishwa kwenye mechi hiyo lakini hata akiwekwa
benchi, bado Simba hawatokuwa salama pindi akiingia.
Uwezo wake wa kupiga faulo, chenga na kumiliki mpira, inaweza chanzo kwa yeye kubadilisha mchezo iwapo atatokea benchi.
Msimu
uliopita, Ajib alitokea benchi kwenye fainali ya Kombe dhidi ya FA na
akawa chanzo kwa Simba kuibuka na ushindi wa mabao 2-1 dhidi ya Mbao FC
kwenye Uwanja wa Jamhuri.
Said Ndemla
Jina
lake lilianza kujulikana pale alipotoa mchango mkubwa kwa Simba kutoka
nyuma na kusawazisha mabao matatu dhidi ya Yanga katika mchezo wa
mzunguko wa pili wa ligi kuu msimu wa 2013/2014.
Katika
mchezo huo hadi mapumziko, Simba walikuwa nyuma kwa mabao 3-0 lakini
kuingia kwa Ndemla na William Lucian kuliiamsha Simba ambayo
ilisawazisha mabao hayo yote.
Mohammed Ibrahim
Kuna
uwezekano mkubwa akaanzishwa kwenye kikosi cha kwanza dhidi ya Yanga
lakini hata akitokea benchi, Ibrahim maarufu kama 'Cabaye' anamudu
vilivyo kubadilisha mchezo.
Mchezaji huyo atakumbukwa
kwa jinsi alivyobadilisha matokeo kwenye mechi ya mzunguko wa kwanza
msimu uliopita kati ya Yanga na Simba na hadi anaingia Simba walikuwa
nyuma kwa bao 1-0 huku wakiwa pungufu lakini aliweza kuimarisha safu ya
kiungo wakaweza kusawazisha bao hilo.
Shiza Kichuya
Mara
kwa mara amekuwa akipata nafasi kwenye kikosi kinachoanza lakini kocha
wa Simba, Joseph Omog alicheza kamali ya kutomwanzisha katika mchezo wa
mzunguko wa pili wa Ligi Kuu msimu uliopita dhidi ya Yanga.
Kichuya
aliingia wakati Simba ipo nyuma kwa bao 1-0 huku ikiwa pungufu lakini
alichangia kupatikana kwa bao la kusawazisha na kufunga la ushindi huku
timu yake ikitoka kifua mbele kwa mabao 2-1.
Jonas Mkude
Siku
hizi hana nafasi ya kudumu lakini ni mchezaji mwenye uwezo mkubwa wa
kubadilisha upepo pindi anapoingia uwanjani akitokea benchi.
0 comments:
Post a Comment