Pamoja
na mbwembwe, maneno, kejeli, tambo na yote ya aina hiyo, mwisho wa
msimu bingwa wa Ligi Kuu Bara anatakiwa kuwa mmoja tu. Ni nani ataondoka
na taji hilo lenye heshima zaidi katika soka la Tanzania? Kazi ipo.
Tathmini
inaonyesha kwamba vita kubwa ya ubingwa itakuwa kwa timu nne tu kati ya
16 zitakazoshiriki. Timu nyingine zinategemewa kukamia mechi moja moja
na kujiepusha na janga la kushuka daraja.
Timu kama
Lipuli, Ndanda, Majimaji na Stand United, zinatazamiwa kuendelea kuwa
wasindikizaji na kutumia muda mwingi katika eneo la chini badala ya
kuwania ubingwa.
Timu za Mtibwa Sugar, Mbeya City na
Mwadui zinatarajiwa kuwa katika eneo la katikati muda mwingi wa msimu
huu, kutokana na kuwa na uwekezaji wa kawaida ambao hautoshi kuwasaidia
kushinda ubingwa.
Timu zinazowania ubingwa sasa ni
zipi? Mwanaspoti inakuletea tathmini wakati huu ambapo pazia la Ligi Kuu
linakwenda kufunguliwa kesho Jumamosi.
Simba 9/10
Tathmini mpaka sasa inaonyesha kwamba Simba ndiyo timu yenye nafasi kubwa zaidi ya kushinda taji la Ligi Kuu kwa msimu huu mpya.
Simba
imesajili wachezaji 13 ambao ni makipa; Aishi Manula kutoka Azam, Said
Mohammed ‘Nduda’ kutoka Mtibwa na Emmanuel Mseja kutoka Mbao FC. Timu
hiyo imesajili pia mabeki; Yusuf Mlipili kutoka Toto Africans, Ally
Shomary na Salim Mbonde kutoka Mtibwa.
Nyota wengine
waliotua Msimbazi ni mabeki; Shomary Kapombe na Erasto Nyoni kutoka Azam
na Jamal Mwambeleko kutoka Mbao FC. Pia kuna kiungo Haruna Niyonzima
kutoka Yanga. Wengine ni washambuliaji John Bocco kutoka Azam, Emmanuel
Okwi kutoka SC Villa ya Uganda na Nicholas Gyan kutoka Ghana.
Usajili
wa Simba unaonekana kuwa na nguvu hasa katika nafasi ya ulinzi ambayo
sasa itakuwa chini ya watu 12 wa nguvu, ambapo mabeki ni tisa na makipa
ni watatu.
Eneo la kiungo nalo limeimarishwa kwa
kuongezwa Niyonzima ambaye ametamba na Yanga kwa miaka sita na kushinda
mataji tisa ya Ligi Kuu. Eneo hilo tayari lilikuwa na wakali kama Jonas
Mkude, Mzamiru Yassin na James Kotei.
Kwa namna ya upana wa kikosi cha Simba, ni wazi kwamba inaweza kupambana wakati wote wa Ligi na kushinda taji hilo.
Kitu
kingine ambacho kinaipa nguvu ni uwezo mkubwa kifedha ambao inao kwa
sasa ambapo mbali na kupata fedha za udhamini kutoka SportPesa, Vodacom
na Azam TV, pia wanafadhiliwa na bilionea Mohammed Dewji.
Yanga 8.5/10
Mabingwa
mara tatu mfululizo wa Ligi Kuu Bara, Yanga, nao wana nafasi kubwa ya
kutetea tena taji lao. Yanga bado ina kikosi imara cha kuweza kuwania
taji hilo lakini italazimika kupambana na Simba imara.
Katika
usajili wake, Yanga, imeimarisha maeneo yenye uhitaji maalumu kwenye
kikosi chake ambapo imemsajili beki wa kati, Abdallah Shaibu ‘Ninja’
kutoka Zanzibar ili kuwaongezea nguvu Nadir Haroub ‘Cannavaro’ na Kelvin
Yondani.
Timu hiyo imesajili pia viungo wawili wa
shoka ambao ni Raphael Daudi kutoka Mbeya City na Kabamba Tshishimbi
‘Papii’ kutoka Mbabane Swallows ya Swaziland huku pia ikiwaongeza Baruan
Yahya na Ibrahim Ajibu kwenye safu yao ya ushambuliaji.
Pigo
kubwa kwa Yanga ni kuondoka kwa winga wake tegemeo, Simon Msuva
aliyejiunga na El Jadida ya Morocco. Msuva ameifungia Yanga mbaao 40
Ligi Kuu katika miaka mitatu iliyopita jambo ambalo linatosha kuonyesha
umuhimu wake.
Nguvu kubwa ya Yanga itaendelea kuwa
katika safu ya ushambuliaji chini ya kinara Amissi Tambwe ambaye
atafanya kazi kwa ukaribu na Donald Ngoma na Obrey Chirwa.
Singida United 8/10
Timu
hii inarejea Ligi Kuu baada ya muda mrefu, lakini tathmini inaonyesha
kwamba ina nafasi pia ya kutwaa taji hilo. Baada ya Simba na Yanga, timu
inayopewa nafasi kubwa ya kuondoka na taji hilo ni Singida United.
Timu
hiyo imefanya usajili wa nyota zaidi ya 14 jambo linaloifanya kuwa na
ushindani mkubwa. Miongoni mwa nyota makini ambao wamejiunga nao ni,
Elisha Muroiwa na Muzdafa Kotinyu kutoka Zimbabwe pamoja na Danny
Usengimana na Michael Rushegoga kutoka Rwanda.
Singida
imesajili kikosi kipana na bila shaka kocha, Hans Van Pluijm, atakuwa na
chaguo la kutosha katika kila eneo, tofauti na timu nyingine za Ligi
Kuu.
Silaha kubwa ya Singida inatarajiwa kuwa soka la
kushambulia kwa kasi hasa kupitia pembeni, soka maarufu la Pluijm ambaye
aliipa Yanga mataji mawili mfululizo kabla ya kuhamia Singida.
Azam 8/10
Matarajio
makubwa yaliyokuwapo kwa Azam FC sasa yameondoka hasa baada ya timu
hiyo kuondokewa na mastaa wake sita wa kikosi cha kwanza ambapo wanne
kati yao wamejiunga na Simba.
Nyota walioondoka ni kipa
Aishi Manula, mabeki Erasto Nyoni na Shomary Kapombe pamoja na
mshambuliaji John Bocco waliotua Simba. Hata hivyo bado Azam inaonekana
kuwa na kikosi cha ushindani ambacho kinaweza kuwashangaza wengi na
kuondoka na taji hilo.
Usajili wa Azam si wa mbwembwe
tofauti na ilivyokuwa katika misimu michache iliyopita. Msimu huu
imemsajili kipa Benedict Haule kutoka Mbao FC, Hamimu Abdulkarim kutoka
Toto Africans, kiungo Salimin Hoza kutoka Mbao FC pamoja na
washambuliaji Waziri Junior kutoka Toto na Mbaraka Yusuf kutoka Kagera
Sugar.
Bado Azam inaendelea kuwa na timu imara, lakini
nafasi yake ya ubingwa haiwezi kuwa kubwa hasa kutokana na wapinzani
wake wa karibu, Simba na Yanga kujipanga vyema. Njia pekee ya Azam
kutwaa taji ni pale wapinzani wake watakapofanya vibaya.
0 comments:
Post a Comment