MWANASHERIA maarufu wa nchini Kenya
Miguna Miguna aliyemuapisha Raila Odinga, amefukuzwa nchini Kenya
(deported) na kupelekwa Canada, chini ya uangalizi wa serikali.
Taarifa kutoka Kenya ambazo
zimethibitishwa na mwanasheria wake zinasma kwamba Miguna aliondolewa
nchini kwa ndege ya KLM iliyoondoka na Nairobi, saa 4 usiku. Tukio hilo limetoka muda mfupi baada ya
mahakama ya juu ya nchini humo kuamrisha kufutwa kwa kesi zake zote
alizofunguliwa, baada ya waendesha mashtaka na pplisi kushindwa kufika
mahakamani, na kumpeleka Miguna.
Odinga akiapa.
Kitendo cha Miguna kuwa deported
kimelalamikiwa na baadhi ya wanaharakati, wakisema hawamtendei haki,
kwani mwanasheria huyo ni raia wa Kenya na mzaliwa wa Kenya. Ifahamike kwamba Miguna ana uraia wa
nchi mbili ikiwemo Canada na Kenya, uraia alioupata wakati akisoma na
kufanya kazi kule kama mwanasheria.
Miguna alikamatwa na Polisi Ijumaa ya
wiki iliyopita kwa kosa la kumuapisha Raila Odinga kitendo ambacho ni
kinyume na sheria, lakini aliachiwa kwa dhamana na kukamatwa tena kabla
hajatoka.
Robert Mugabe alijiuzulu Novemba 21
baada ya kuahidiwa kinga ya kutoshtakiwa, kulipwa dola za Marekani 10
milioni kwa mkupuo, mshahara wa kila mwezi, matibabu, usalama wake
pamoja na ulinzi wa mali zake, gazeti la Independent limeandika.
Uchunguzi
uliofanywa na Independent umefichua kwamba watu wa Mugabe walioshiriki
katika mazungumzo yaliyowezesha yeye kuondoka walifanikiwa kufikia
makubaliano na majenerali kuhakikisha mkongwe huyo mwenye umri wa miaka
93 haendi kuishi uhamishoni bali afurahie kustaafu kwake nchini Zimbabwe
na apate marupurupu yake. “Serikali itamlipa Mugabe dola 5
milioni kwa mkupuo na kisha kiasi kinachosalia atakuwa akilipwa kwa
mafungu,” chanzo kimoja kimesema. “Mugabe atapatiwa matibabu pamoja na
mshahara kamili kila mwezi. Na ikiwa atafariki mkewe atakuwa analipwa
nusu mshahara kila mwezi.” Mugabe alifanya majadiliano ili aweze
kuondoka salama kupitia timu ya wapatanishi ambayo ilijumuisha kasisi wa
Kikatoliki, Fidelis Mukonori na gavana wa zamani wa RBZ Gideon Gono.
Mukonori alisema katika mahojiano kwamba wajibu wake ulikuwa kuwa
mpatanishi kati ya majenerali na Mugabe.
Mwalimu wa somo la Mapishi katika shule ya Sekondari ya St. Charles High
School mjini Maryland nchini Marekani amehukumiwa kifungo cha mwaka
mmoja jela kwa kosa la kumtongoza na kumtumia picha za utupu mwanafunzi
wake wa kiume mwenye umri wa miaka 17.
Kwa mujibu wa maelezo kutoka kwenye mtandao wa kituo cha runinga cha
Fox 5 DC Mwalimu huyo aliyetambulika kwa jina la LaToya Nicole Parker
(40) imeelezwa kuwa alikuwa anamtuma mwanafunzi huyo kwenye supermarket
kipindi cha mapumziko na kwenda nae nyumbani kwake.
Kisa hicho ambacho kiliripotiwa na wazazi wa mwanafunzi huyo mwezi machi
mwaka huu, 2017 kwenye kituo cha polisi kabla ya kupelekwa mahakamani
ambapo mshtakiwa alikiri kutenda kosa hilo jumatatu ya wiki iliyopita.
Upelelezi uliofanywa na polisi pamoja na ushahidi uliotolewa mahakamani
unaonesha kuwa mwalimu huyo alianza kumtongoza mwanafunzi huyo tangu
mwezi April mwaka huu , 2017 kwa kumuandikia barua za mahaba, kumtumia
picha zake za utupu na kumuahidi pesa mwanafunzi huyo kama angelikubali.
Kwa upande mwingine mwalimu mkuu wa shule ya St. Charles High School
Principal, Richard Conley amesema mwalimu huyo alikuwa anafundisha somo
la Mapishi shuleni hapo na alikuwa hajaajiriwa rasmi shuleni hapo bali
alikuwa anafanya kazi kwa muda (Temporary) tangu mwezi Machi mwaka huu
2017.
“Baada ya kupata malalamiko kutoka kwa wazazi wake mapema tulimsimamisha
kazi Ms. Parker kwani tayari walikuwa wameshatoa taarifa polisi ili
kupisha uchunguzi.“amesema Mwalimu Mkuu wa shule hiyo, Richard Conley.
Polisi mjini Maryland wamesema walikuta picha 5o za utupu za mwalimu
huyo na jumbe 303 zilizotumwa kwenye simu ya mwanafunzi huyo nyingi
zikiwa za mahaba.
Mahakama mjini Maryland inayoshughulikia kesi za watoto imetoa hukumu
kwa mwalimu huyo kwenda jela mwaka mmoja au kulipa faini ya dola $20,000
sawa na Tsh milioni 44 kwa kosa la kusambaza picha za utupu kwa watoto
na udhalilishaji.
Wabunge nchini Uganda wamepigana ndani ya ukumbi wa bunge wakiwa katika
siku ya pili ya kikao cha kujadili wa muswada wa kuondoa ukomo wa miaka
ya kugombea nafasi ya urais kwa mjibu wa katiba ya taifa hilo.
Katika ugomvi huo wabunge hao walirushiana viti, kuharibu vipaza sauti
na katika kikao hicho kilichoongozwa na Spika wa bunge, Bi.Rebecca
Kadaga.
Ugomvi huo ulianza pale Spika alipochukua hatua ya kuwafukuza wabunge
wapatao 25 wengi wao wakiwa ni wale wa upinzani kwa madai ya utovu wa
nidhamu pamoja na waziri wa serikali aliyeshtakiwa kwa kufyatua risasi
bungeni siku ya jumanne.
Wabunge hawa wanadai kuwa kama kikomo cha umri wa miaka 75 kitaondolewa
basi rais aliyepo kwa sasa atapata mwanya wa kugombea tena mwaka 2021.
Mkuu na mwanzilishi wa mtandao wa Facebook ,Mark Zuckerberg, amebeza
maoni ya rais Donald Trump dhidi ya mtandao huo kwamba umekuwa
ukimpinga.
Zuckerberg amesema pande zote mbili za kisiasa nchini Marekani zilikuwa
zikiutazama mtandao wa Facebook tofauti kutokana na kutofurahishwa na
maoni yanayotolewa na watumiaji.
Ameongeza wakati wa uchaguzi Democrats wamewahi tuhumu mtandao huo kwamba unamsaidia Trump.
Mwanzilishi huyo wa Facebook amebainisha kuwa wakati wote wa uchaguzi
mtandao wake ulifanya unachoweza kwa manufaa ya wapiga kura.
Wanafamilia 11 wameripotiwa
kufariki wakiwa kwenye ibada ya ubatizo wa mtoto baada ya paa la kanisa
walilokuwepo kuwaangukia kutokana na tetemeko kubwa lililokumba Mexico
juzi September 20, 2017.
Waliopona kwenye janga hilo ni baba wa mto aliyekua anabatizwa ambaye
alikua ni wa miezi miwili pamoja na wachungaji wawili ambao walikua
wakiongoza tukio hilo.
Mwanamke anayetajwa kuwa tajiri
zaidi duniani ambaye na mrithi wa Kampuni ya L’Oreal Ufaransa, Liliane
Betterncourt amefariki dunia akiwa na miaka 94.
Liliane ambaye utajiri wake ulitajwa na jarida Forbes na Orodha ya
Matajiri Duniani (Bloomberg Billionaire Index) kuwa ni wa Dola za
Marekani bilioni 44 sawa na Shilingi trilioni 105.6, amefariki nyumbani
kwake lakini kumekua na habari kwamba mwanamama huyu alikua na tatizo la
akili.
Akiwa na umri wa miaka 15 Liliane alijiunga na kampuni ya baba yake
ya L’Oreal ambayo ilijishughulisha na vipodozi ili kujifunza kuendesha
biashara hiyo na mwaka 1957 akiwa na 24 alirithi rasmi kampuni hiyo ya
baba yake ambayo aliiendesha mpaka alipoiacha akiwa na miaka 89 mwaka
2012 kutokana na matatizo hayo ya kiafya.
RAIS wa Ufilipino, Rodrigo Deterte,
amesema yuko tayari mwanawe auawe iwapo madai kwamba anahusika katika
biashara ya madawa ya kulevya yatakuwa ya kweli. Ameongeza kwamba polisi
ambao wataendesha mauaji hayo watalindwa dhidi ya kufunguliwa
mashitaka.
Paolo Duterte
mwenye umri wa miaka 42, alifikishwa mbele ya jopo la maseneta
alipokana madai yaliyotolewa na wabunge wa upande wa wapinzani kwamba
alikuwa mwanachama wa kundi la Wachina lililosaidia kuingiza ndani ya
nchi hiyo madawa ya kulevya aina ya ‘crystal methamphetamine’.
Mtoto wa Rais Deterte, Paolo Duterte (kushoto) akiwa mahakamani na mtuhumiwa mwenzake.
Rais Duterte
hakumaanisha hasa madai hayo dhidi ya mwanaye, lakini alisisitiza
maneno yake aliyoyasema wakati wa kampeni ya uchaguzi mwaka jana kwamba
hakuna mwanaye yeyote anayejihusisha na madawa ya kulevya, lakini
wangekabiliwa na adhabu ngumu zaidi iwapo wangefanya hivyo. “Kama nina
watoto wanaojihusisha na madawa ya kulevya, waueni ili watu wasiwe na la
kusema,” alisema Duterte katika hotuba yake aliyoitoa juzi (Jumatano)
usiku mbele ya wafanyakazi wa serikali katika ikulu ya Manila.
Paolo Duterte.
“Hivyo, nilimwambia
Pulong (jina la utani la Paolo) kwamba amri yangu ni kukuua iwapo
utakamatwa. Na nitawalinda polisi watakaokuua, kama ni kweli
ujajihusisha na mambo hayo,” alisema.
Duterte (72) alishinda
uchaguzi wa rais kwa kampeni kali aliyoendesha akiahidi kuyatokomeza
madawa katika jamii kwa kuua wauaji na watumiaji wa madawa hayo wapatao
100,000.
Tangu ashike madaraka
katikati ya mwaka jana, polisi wameripoti kuua watu zaidi ya 3,800
katika oparesheni dhidi ya madawa ya kulevya wakati maelfu wameuawa
katika mazingira yasiyoelezeka. Maelfu ya wakosoaji na wafuasi wake,
walifanya mikutano mbalimbali jana (Alhamisi) kujadili vita hiyo kali ya
mauaji na vitisho vya kijeshi mitaani.
Rais wa Marekani Donald Trump ameonya vitisho kutoka kwa mataifa Korea
kaskazini na Iran katika hotuba yake katika umoja wa mataifa.
Katika hotuba yake ya kwanza katika mkutano wa umoja huo mjini New York,
ameonya kuwa Marekani itaangamiza Korea kaskazini iwapo italazimika
kujitetea ama kuwalinda washirika wake.
Alimkejeli kiongozi wa Korea kaskazinmi Kim Jong un akisema: Yuko katika harakati za ''kujitoa muhanga''.
Korea kaskazini imefanya makombora yake kinyuklia majaribio na kukiuka maamuzi ya Umoja wa mataifa.
Iran, bwana Trump alisema ni nchi ya kifisadi na inayoongozwa kidikteta
kwa lengo la kutaka kuyumbisha eneo la mashariki ya kati.
Ameitaka serikali mjini Tehran kukoma kuwasaidia ugaidi mbali na
kuukosoa utawala wa rais Obama kuhusu makubaliano ya mpango wa amani wa
nyuklia wa taifa hilo ambao ameutaja kuwa aibu.
Amesema kuwa marekani haitanyamaza ama kuingia mikataba inayopendelea upande mmoja.
Amesema kuwa mataifa mengine yanaelekea motoni lakini akasema kuwa UN utayasaidia.
Emir wa Kuwaiti, Sheikh Sabah al-Ahmad Al-Sabah, akizungumza na waandishi wa habari alipokutana na raisi wa Marekani, Donald Trump,katika ikulu ya nchi hiyo iliyopo Washington, DC, Septemba 7, 2017. (AFP photo)
Ripoti kutoka nchini Kuwait zinasema kuwa imemfukuza balozi wa Korea Kaskazini.
Hakuna
taarifa rasmi iliyotolewa lakini kuwait imewaambia waandishi wa habari
kuwa balozi wa Korea Kaskazini, amepewa mwezi mmoja kuondoka huku
wanadiplomaisa wa Korea Kaskazini wakipunguzwa.
Kuwait ndiyo nchi pekee katika ghuba iliyo na ubalozi wa Korea Kaskazini.
Maelfu ya raia wa Korea Kaskazini wanafanya kazi nchini kuwait na nchi zingine za ghuba kama vibarua.
Hatua hiyo inachukuliwa wiki mbili baada ya kiongozi wa kuwait kuzuru Washington.
Marekani imetaka hatua za kimataifa kuchukuliwa dhidi ya Korea Kaskazini kufuatia mipango yake ya nyuklia.
Gavana wa Florida amekuwa akitoa maelezo ya operesheni ya kazi ya
misaada inavyofanyika kutokana na hali inayoikabili Marekani baada ya
kukumbwa na kimbuga na dhoruba maruufu Irma.
Rick Scott , asema kwamba vipaumbele vya haraka vimeelekezwa katika
kusaidia hospitali na kuokoa maisha. Zaidi ya theluthi mbili ya taifa
hilo haina nishati ya umeme na bwana Scott amearifu kuwa itachukua wiki
kadhaa kurejeshwa kwa ukamilifu wake nishati hiyo.
Moja ya maeneo yaliyoathiriwa vibaya na kimbunga hicho ni maeneo ya
pwani ya mji wa Florida yajulikanayo kama vitovu vya Florida na
imearifiwa kuwa itachukua muda kwa wakaazi wa maeneo hayo kurejea katika
makaazi yao.
Scott anasema Kuna uharibifu mkubwa , nina matumaini kila mtu alinusurika, ni mambo ya kutisha tuliyoyaona.
Ninajua hali ya taifa letu lakini hasa vitovu vya Florida itachukua muda
kurejea katika hali yake ya kawaida, kwakweli kuna uharibifu mkubwa .
''Naelewa kuwa watu walio wengi wanataka kurejea katika maisha yao ya
kawaida, najua kila mmoja anataka kuanza upya, nawasihi kuwa na subra,
mnapaswa kupata msaada wa haraka katika maeneo yenu, tunapaswa kupata
maji tena, tunahitaji huduma zote za kijamii zirejee kama kawaida lakini
nasema, itachukua muda Mrefu!''
Abiria tisa wamezua taharuki kwenye kiwanja cha ndege cha kimataifa cha Zaventem, nchini Ubelgiji baada ya mmoja wao kutamka matamshi yaliyosikika ‘Allah Akbar’ kwa sauti kubwa mara kadhaa.
Watu hao tisa walitolewa na maaskari kwenye ndege ya shirika la Ryanair, na kuamriwa mizigo yao kutolewa kwenye ndege ili kukaguliwa zikiwa zimebakia dakika 10 kabla ya ndegehiyo kuondoka.
Ndege hiyo ililazimika kuchelewa kwa masaa manne ikipisha ukaguzi wa mizigo ya watu hao, ambao walitambuliwa kuwa ni raia wa Ubelgiji.
Polisi mjini Brussels wamethibitisha taarifa hizo kupitia kituo cha Runinga cha VTM Nieuws kwa kusema kuwa ni kweli tukio hilo limetokea siku ya Jumamosi Tarehe 2 Septemba ambapo wavulana hao tisa walikuwa wanasafiri kutoka Mjini Brussels kwenda Madrid, Hispania.
“Tumepokea taarifa hizo za wanaume tisa waliokuwa wakisafiri kutoka Ubelgiji kwenda Madrid, Hispania lakini walipoingia kwenye ndege mmoja wao akaanza kutamka kwa sauti ‘Allah Akbar’ akimaanisha ‘Mungu mkubwa’ kama mara sita hivi ndipo askari wa usalama wakamtoa kwenye ndege pamoja na wenzake wote kwa ukaguzi”,amesema Peter De Waele msemaji wa jeshi la Polisi mjini Brussels .
Kwa mujibu wa taarifa kutoka gazeti la Top 24 abiria walioshuhudia tukio hilo wamesema lilitokea baada ya ndege hiyo kuchelewa masaa matatu kuruka na ndipo mtu huyo akaanza utani akitamka ‘Allah Akbar’ huku akicheka.
Hata hivyo abiria hao nane walirudishwa kwenye ndege baada ya ukaguzi kufanyika na ndege kuendelea na safari yake, ingawaje mpaka sasa bado haijawekwa wazi sababu za kupekuliwa kwa watu hao kwa mara ya mbili huku mitandao mingi duniani ikiandika kuwa ni hofu ya ugaidi iliyotanda nchini Ubelgiji.
Balozi wa Marekani kwenye Umoja wa Mataifa ameilaumu Korea ya Kaskazini kwa kulazimisha vita kutokana na majaribio yake ya makombora ya mara kwa mara.
Nikki Haley ametaka kuwepo kwa muda wa dharura wa Baraza la Umoja wa Mataifa utakao jibu majaribio hayo kwa hatua kali.
"Vita sio kitu ambacho Marekani ingetaka," alisema. "Hatutaki vita kwa sasa lakini uvumilivu wa nchi yetu hautuzuii."
Baadae, kupitia mazungumzo ya simu na Rais Trump, Kansela wa Ujerumani Angela Merkel amesema atahimiza kuwepo kwa vikwazo vikali kutoka umoja wa nchi za ulaya dhidi ya Pyongyang.
Hata hivyo, China imesisitiza wito wake wa kutaka pande zote zirudi katika meza ya mazungumzo.
Ripoti zinasema kuwa Korea Kaskazini inajiandaa kwa majiribio mengie ya makombora.
Siku ya Jumapili ilifanya jaribio la bomu la chini ya ardhi lililoaminika kuwa na nguvu ya kati ya kilotani 20 na 120.
Kifaa hicho hicho kinaweza kuwa na nguvu mara tatu zaidi ya bomu lililotumiwa kuharibu mji wa Hiroshima mwaka 1945.
China haitaki kuwepo nchi yenye silaha za nyuklia ya Korea Kaskazini na mara kwa mara imeeleza msimamo wake kwa nchi hiyo.
Lakini pia haitaki kuona utawala wa Korea Kaskazini ukiondolewa madarakani. Hii itasababisha mamilioni ya wakimbizi kukimbia kwenda China na kuchangia kuungana kwa Korea ambayo itakuwa chini ya ushawishi wa Marekani.
Waziri wa ulinzi nchini Marekani James Mattis amesema kuwa Marekani itaendelea na mazungumzo ya kidiplomasia na Korea Kaskazini.
Matamshi hayo yanajiri baada ya rais Donald Trump kusema katika mtandao wake wa Twitter kwamba mazungumzo sio suluhu kwa mipango ya kijeshi ya Korea Kaskazini.
Urusi pia imeionya Marekani dhidi ya kuchukua hatua za kijeshi akisema madhara yake yatakuwa makubwa.
Korea Kaskazini ilizuwa wasiwasi baada ya kurusha kombora kupitia anga ya Japan siku ya Jumanne.
Kombora hilo ambalo Japan limelitaja kuwa tishio lisilo la kawaida , lilivuka katika anga ya kaskazini ya kisiwa cha Japana cha Hokkaido mapema siku ya Jumanne, na kusababisha raia kujificha kabla ya kombora hilo kuanguka baharini yapata kilomita 1,180 .
Korea Kaskzini baadaye ilisema kuwa ni hatua mojawapo ya operesheni zake za kijeshi katika eneo la pacific na kurejelea tishio lake la kushambulia kisiwa cha pacific cha Guam.
Siku chache zilizopita, bwana Trump alikuwa amenukuliwa akisema anaamini kiongozi wa Korea Kaskazini Kim Jong un alikuwa ameanza kuheshimu Marekani.
Lakini katika chapisho lake la siku ya Jumatano , alisema: Marekani imekuwa ikizungumza na Korea Kaskazini na kuwalipa fedha kwa miaka 25.
''Kuzungumza nao sio suluhisho''.lakini alipoulizwa iwapo ni kweli kwamba Marekani imepoteza matumaini ya kidiplomasia , bwana Mattis alitofautiana wazi na rais Trump akisema: Hapana. Sisi hatujapoteza matumaini kupitia kutatua maswala kidiplomasia .
Alikuwa akizungumza alipokutana na mwenzake wa Korea Kusini Song, Young-moo katika Pentagon.
''Tunaendelea kufanya kazi pamoja na waziri na mimi tunagawana majukumu ili kulinda mataifa yetu, idadi yetu na maslahi yetu''.
Baraza la usalama la Umoja wa Mataifa limelaani kitendo cha Korea Kaskazini kwa kurusha kombora kupitia anga la japan, huku nchi hiyo ikithibitisha kutekeleza.
Taarifa iliyoandikwa na Marekani, haikutishia kuiwekea vikwazo vipya Korea kaskazini.
Lakini Baraza la Usalama limeitaka Korea Kaskazini kusitisha majaribio zaidi na kusitisha mpango wake wa nuklia.
Wanachama 15 wa Baraza hilo la Usalama wameitaka korea kaskazini kuchukua hatua za haraka kupunguza hali ya wasiwasi uliyopo.
Majeshi ya Korea kusini na Marekani yamekuwa yakifanya mazoezi ya pamoja karibu na mpaka wa Korea kaskazini, jambo ambalo Pyongyang inasema ni mazoezi yenye kulenga uvamizi wa kijeshi.
Korea kaskazini imerusha makombora yake ambayo yalipita Japan kabla ya kudondokea baharini.
Makombora hayo yalisafiri kuelekea mashariki karibu kilomita elfu moja juu ya kisiwa cha Japan cha Hokkaido.
Tukio hilo limechochea tahadhari ya hatari ambayo watu walielekezwa kujificha katika maeneo yaliyo chini ya ardhi ama kwenye majengo yaliyo imara.
Waziri mkuu wa Japan Shinzo Abe amesema urushwaji huo wa makombora ambao haujawahi kutokea , umeleta kitisho kikubwa kwa taifa lake.
Hakuna juhudi zilizofanywa na Japan kulitengua kombora hilo lakini ilitoa onyo la kiusalama ikiwaambia raia wake katika eneo la Hokkaido kujificha chini ya majumba yaliojengwa ardhini.
Wanajeshi wa Marekani na Japan wanafanya zoezi la pamoja katika eneo hilo la Hokkado, rais wa Korea Kusini Moon Jae-in aliagiza uwezo wa utumiaji wa nguvu ili kujibu shambulio hilo.
Ndege nne za Korea Kusini zilifanya zoezi la kurusha makombora siku ya Tuesday.
Bwana Abe alisema kuwa amezungumza na rais wa Marekani Donald Trump na kwamba wote wamekubaliana kuiongezea shinikizo Korea Kaskazini.
Katika mfululizo wa majaribio yake ya makombora ya hivi karibuni Korea kaskazini haijawahi kurusha makombora yaliyopita juu ya ardhi ya nchi hiyo, hivyo tukio hili la sasa limeleta wasiwasi mkubwa.
Haki miliki ya picha
Katika siku za hivi karibuni Pyongyang ilijaribu kombora lake lililopata mafanikio kutokana na uwezo wake wa kuweza kuifikia Marekani na kuonyoa kuwa inasimamia mipango yake ya kushambulia kwa makombora eneo la Marekani la Guam, kilomita elfu mbiili kusini mashariki mwa Japan.
Mahakama Kuu nchini Kenya imeanza kusikiliza kesi ya kupinga ushindi wa Rais wa Kenya,Uhuru Kenyata, iliyotakiwa kuanza kusikilizwa jana.
Kesi hiyo ilitakiwa kuanza jana
jioni baada ya kumalizika kwa hatua ya kwanza iliyofanyika juzi kwa
pande zote tatu yaani upande wa NASA, Jubilee na Tume ya Taifa ya
Uchaguzi na Mipaka nchini humo(IEBC) kuwasilisha mahakamani hoja zao za
maandishi.
Msajili wa Mahakama hiyo, Esther
Nyaiyaki akinukuliwa na gazeti la Kiingereza la Standard nchini humo
bila kueleza mabadiliko hayo alisema itasikilizwa leo.
Kesi hiyo inatokana na uamuzi wa
Muungano wa vyama vya upinzani NASA chini ya mgombea wake Raila Odinga
kupinga matokeo ya uchaguzi wa urais wa Agosti 8, wakidai kuwa haukuwa
wa haki na huru.
Odinga akiwa kwenye viunga vya mahakama.
Odinga amepinga matokeo
yaliyotangazwa Agosti 11, mwaka huu na Tume hiyo yakimtambua Rais Uhuru
Kenyatta wa Muungano wa Jubilee kuwa mshindi wa kiti cha urais katika
ungwe ya pili akipata kura 8, 203, 290 sawa na asilimia 54.27 huku
mpinzani wake mkuu, mgombea wa Muungano wa upinzani wa NASA, Raila
Odinga akIpata kura milioni 6,762,224 sawa na asilimia 44.74.
Odinga hakukubaliana na matokeo hayo
hadharani na aliamua kuwasilisha stakabadhi zake mahakamani hapo ikiwa
ni saa nane kabla ya tarehe ya mwisho. Baadaye, Agosti 24, mwaka huu,
Rais Uhuru Kenyatta na Naibu wake William Ruto kwa upande wao, pia
waliwasilisha stakabadhi zao kuhusiana na kesi hiyo.
Odinga ambaye alikuwa ni miongoni mwa
wagombea nane wa kiti hicho cha urais, alilalamika pia kuwapo hujuma za
Rais Uhuru Kenyatta kutumia mamlaka yake vibaya katika kuingilia mfumo
wa tume hiyo.
Mahakama ya Juu imeipa idhini NASA na Rais Kenyatta kukagua mitambo
ya tume ya uchaguzi kufuatia madai ya mitambo kudukuliwa. Idhini
iliyotolewa na mahakama ni ya kusoma taarifa zilizopo kwenye mitambo
hiyo bila kurekebisha chochote.
Mahakama ya Juu nchini Kenya imeukubalia muungano wa upinzani nchini humo National Super Alliance (Nasa) kupekua sava zilizotumiwa na tume ya uchaguzi nchini humo wakati wa uchaguzi uliofanyika tarehe 8 Agosti.
Mahakama hiyo imesema muungano huo utaweza kusoma data kwenye sava hizo chini ya uangalizi kuhakikisha usalama wa mitambo ya IEBC hauhujumiwi.
Mgombea wa Nasa Raila Odinga amewasilisha kesi mahakamani kupinga ushindi wa Rais Uhuru Kenyatta wa chama cha Jubilee.
Mawakili wa Bw Odinga wameruhusiwa na mahakama kunakili data kutoka kwenye sava hizo kwa ajili ya kufanya uchunguzi kuhusu uchaguzi huo.
Miongoni mwa mengine, upinzani utapata utambulisho wa sava zilizotumiwa wakati wa uchaguzi, ukuta wa kinga uliotumiwa kulinda sava hizo pamoja na mitambo ya dijitali ya uchaguzi wa Kenya (KIEMS) dhidi ya wadukuzi na mfumo endeshi wa mitambo hiyo pamoja na nywila zilizotumiwa kuingia katika mitambo hiyo.
Kadhalika, wataweza kupata taarifa kuhusu yaliyojiri katika mitambo hiyo ya uchaguzi kuanzia Agosti tano hadi leo.
Aidha, wataruhusiwa kusoma nakala za Fomu 34A na 34B (fomu za matokeo katika vituo vya kupigia kura na ngazi ya maeneo bunge) ambazo zilitumiwa kutangaza matokeo.
Taarifa kuhusu mchakato wa upinzani kupekua sava na mitambo hiyo ya IEBC itawasilishwa kwa mahakama hiyo kesho jioni.
Majaji saba wa mahakama hiyo ya juu wameanza kusikiliza kesi hiyo iliyowasilishwa na Bw Odinga leo.
Kwa mujibu wa matokeo ya IEBC, Rais Kenyatta alipata kura 8,203,290 huku naye Raila Odinga akipata kura 6,762,224.
Gavana wa jimbo la Texas, Greg Abbott, anasema kuwa, mafuriko ya kutisha ndio swala lake kuu la msingi, huku mvua kubwa inayoandamana na kimbunga kiitwacho Harvey, ikiendelea kutatiza mambo katika jimbo hilo.
Bwana Abbott anasema kwamba, miji miwili katika barabara inakopitia kimbunga hicho, Houston na Corpus Christi, tayari imepokea mvua zaidi ya Sentimita 50 na kiwango kinatarajiwa kuongezeka kwa mita moja zaidi, kabla ya kimbunga hicho kupungua, ifikiapo katikati ya wiki hii.
Haki miliki ya picha
Zaidi ya wafungwa 4,500 katika gereza moja kusini mwa Houston wamehamishiwa hadi gereza lingine mashariki mwa Texas kwa sababu ya kuongezeka kwa maji ya mto Brazos ulioko karibu. Maafisa wakuu wa jimbo hilo wamesema.
Juhudi za uokoaji, zinatatizwa na upepo mkali.
Haki miliki ya picha
Mamia kwa maelfu ya watu wamekatikiwa na guvu ya umeme.
Kufikia sasa kifo cha mtu mmoja tu kimethibitishwa kutokea katika mji wa Rockport, huku wakuu wakionya kuwepo kwa mafuriko zaidi ya maji.
Gari lililokuwa na mikebe ya gesi ya kutoa machozi limepatikana katika ukumbi ambapo kulipangiwa kufanyika tamasha ya muziki mjini Rotterdam nchini Uholanzi, saa chache baada ya tahadhari kutoka kwa polisi wa Uhispania kusababisha kufutiliwa mbali kwa tamasha hilo la muziki.
Dereva wa gari hilo lililosajiliwa nchini Uhispani amekamatwa na kuziliwa na polisi, meya wa mji wa Rotterdam Ahmed Aboutaleb amewaambia wanahabari.
Bendi kutoka Marekani ya Allah-Las, ambayo mara nyingi hupokeza vitisho kutokana na jina lake, ilikuwa imepangiwa kutumbuiza katika ukumbi wa The Maassilo.
Lakini tahadhari kutoka kwa polisi lilisababisha kufutiliwa mbali kwa tamasha hiyo dakika za mwisho.
Hata hivyo Bw Aboutaleb amesema haijabainika iwapo gari hilo lina uhusiano na tishio la shambulio la kigaidi.
Lakini tahadhari hiyo ya polisi wa Uhispania ilitolewa kukiwa na hali ya juu ya tahadhari baada ya mashambulio kadha kutekelezwa Uhispania wiki iliyopita.
Lakini maafisa wa mahakama wameambia shirika la habari la Reuters kwamba hakuna uhusiano wowote kati ya mashambulio hayo ya Uhispania na onyo kutoka kwa polisi wa Uhispania, ambalo inadaiwa limetokana na uchunguzi wa muda mrefu.
Polisi wa Uholanzi pia wamemkamata dereva wa gari hilo kutoka Uhispania na anahojiwa.
Kikosi cha kuchunguza na kutegua mabomu kimetumwa eneo hilo, taarifa zinasema.
Polisi waliovalia fulana zisizopenya risasi wamefika eneo hilo, baada ya watu wote kuamrishwa kuondoka.
Haki miliki ya picha
"Polisi walikuwa wamezingira eneo la ukumbi huo na hilo lilisaidia kupatikana kwa mikebe hiyo ya gesi," Bw Aboutaleb amesema.
Katika mashambulio ya wiki iliyopita katika jimbo la Catalonia nchini Uhispania, watu 15 waliuawa katika mashambulio Barcelona na katika mji wa Cambrils.
Mashambulio hayo yalitekelezwa baada ya mlipuko katika nyumba iliyokuwa imejaa mikebe ya gesi ambapo washambuliaji inadaiwa walikuwa wanaandaa vilipuzi zaidi.
Katika mahojiano mwaka jana, kundi hilo la muziki aina ya Rock la Allah-Las liliambia gazeti la Guardian la Uingereza kwamba huwa linapokea vitisho mara kwa mara kutoka kwa Waislamu ambao hukerwa na kutumiwa na neno Allah - Mungu kwa Kiarabu - kama jina lake.
Kundi hilo lilisema lilitaka kuwa na jina lenye sifa za kidini baada ya kuhamasishwa na kundi jingine liitwalo Jesus and Mary Chain.