Tuesday 22 August 2017

YANI NI MWENDO WAKUTUPA SHUKA NAKULIAMSHA DUDE TAIFA


Image result for simba vs yanga

SIMBA na Yanga zinaliamsha dude kesho Jumatano ndani ya Uwanja wa Taifa. Lakini Mwanaspoti pia tumeamua kuliamsha kwa kutoka kivingine katika mwonekano ambao umeboreshwa zaidi na wenye mambo mazuri na nyanja zote za michezo tumezigusa kwa kutumia wataalamu waliobobea. Kaa tayari.
Hapo Taifa kesho saa 11 jioni litaamshwa dude kuashiria mwanzo wa msimu mpya wa Ligi Kuu Bara. Simba baada ya kusota muda mrefu kwenye ligi ya ndani na kupachikwa majina kibao ya kejeli, safari hii imenunua wachezaji wa maana na wametangaza kiama cha Yanga kwenye Ngao ya JAamii.
Simba inaamini huu ni msimu wake kutokana na ilivyojipanga. Lakini taarifa zitakazoishtua Simba ni kwamba, Yanga haijawahi kupoteza mchezo wowote, Donald Ngoma, akiwamo uwanjani. Kwenye mechi tatu alizoichezea Yanga dhidi ya Mnyama, imeshinda mbili na ikatoa sare moja. Rekodi hiyo imeipa kiburi Yanga ambayo pia inatambia uzoefu wa kukaa pamoja muda mrefu.
Hata hivyo, Simba nayo imepata kiburi baada ya kubaini kwamba katika mechi mbili ilizocheza na Yanga mwaka huu wa 2017, Mnyama aliondoka kifua mbele mechi zote, kwa mikwaju ya penalti Kombe la Mapinduzi na nyingine ya Ligi Kuu kwa mabao 2-1 Februari.
Rekodi zinaonyesha mchezo huo utakaorushwa moja kwa moja na Azam TV, ni wa kwanza wa Ngao ya Jamii kwa Simba na Yanga tangu Mwaka 2011 walipovaana na Simba kushinda mabao 2-0 wafungaji wakiwa Haruna Moshi ‘Boban’ na Felix Sunzu.
Ofisa Habari wa Simba, Haji Manara, alisema wametumia zaidi ya Sh 1.3 bilioni kuimarisha kikosi hivyo wataifunga Yanga.
Nyota wanaotarajiwa kuleta mvuto zaidi kesho ni Ibrahim Ajib atakayeichezea Yanga mechi ya kwanza ya mashindano akitokea Simba sambamba na Haruna Niyonzima ambaye ataikabili klabu yake ya zamani kwa mara ya kwanza pia, sasa akiwa Simba.
Simba inaonekana kujiimarisha zaidi katika eneo la ulinzi na Salim Mbonde na Erasto Nyoni pamoja na Jamal Mwambeleko wanatarajiwa kuwa wachezaji wapya watakaoanza sambamba na nahodha Method Mwanjali.
Yanga imejiimarisha katika eneo la kiungo na Mkongomani, Kabamba Tshishimbi pamoja na Raphael Daudi wanatarajiwa kuanza katika eneo la katikati sambamba na nahodha, Thaban Kamusoko.
OKWI, KICHUYA NA  TAMBWE
Mchezo wa kesho umeshikwa na nyota watatu ambao ni Shiza Kichuya, Emmanuel Okwi na Amissi Tambwe ambao ndiyo wababe wa kufumania nyavu zinapokutana.
Kichuya ndiye shujaa wa sasa na katika mechi mbili za mwisho amefunga mabao mawili likiwamo la ushindi katika mchezo wa Februari 25, Simba ilishinda 2-1.
Tambwe na Okwi ndiyo vinara wa mabao wanaoendelea kucheza ambapo katika michezo hiyo ya watani wa jadi wamefunga mabao matatu kila mmoja.
Okwi ambaye amesaini mkataba mpya Simba anakumbukwa zaidi kwa bao lake murua la ushindi mwaka 2015 alipomfunga kipa Ally Mustapha ‘Barthez’ kwa umbali mrefu.
Tambwe ndiye alisababisha varangati Oktoba mwaka jana kwa kufunga bao baada ya kuushika mpira kwa mkono, bao lililowapa hasira mashabiki wa Simba na kuvunja viti vya Uwanja wa Taifa.
Hata hivyo Tambwe atakabiliwa na wakati mgumu wa kuvunja rekodi ya kutomfunga kipa, Aishi Manula tangu alipotua nchini mwaka 2013.
Kiufundi timu hizo zinaonekana kuwa imara katika maeneo tofauti ambapo Simba ipo vizuri zaidi katikati huku ikitegemea washambuliaji wa pembeni katika kufunga wakati Yanga iko vizuri mbele hasa kwa washambuliaji wa kati.
Safu ya kiungo ya Simba inayoundwa na nahodha wa zamani, Jonas Mkude, Mzamiru Yassin, Mghana James Kotei, Mnyarwanda Haruna Niyonzima, Said Ndemla na Mwinyi Kazimoto inatarajiwa kuwa nguvu kubwa ya timu hiyo kesho na kutawala mchezo. Mpaka sasa nafasi kubwa ya kuanza ipo kwa Mzamiru, Kotei na Niyonzima ambao wamekuwa katika kiwango cha juu tangu kuanza maandalizi ya msimu.
Kwa Yanga mastraika wake, Donald Ngoma, Ajib, Tambwe na Obrey Chirwa ambaye hata hivyo anaweza asicheze, na ndiyo silaha kubwa kwao.
Yanga inatarajiwa kuwatumia zaidi mabeki wa pembeni Juma Abdul na Gadiel Michael kujenga mashambulizi kwenda kwa washambuliaji wa kati. Kocha wa Simba, Joseph Omog anatarajiwa kuendelea kulinda rekodi yake dhidi ya Yanga ambapo msimu uliopita katika mechi zote tatu hakupoteza hata mara moja. Lwandamina naye atakuwa akipigania ushindi wake wa kwanza dhidi Simba.
Share:

0 comments:

Post a Comment

Ads

Blog Archive