Huku mabingwa wa Soka Tanzania Bara, Yanga wakitarajiwa kujitupa uwanjani leo Jumamosi kuvaana na Ndanda FC, beki wao wa pembeni Hassan Kessy anaweza kuukosa mchezo huo baada ya kupata ajali ya bodaboda.
Yanga wanacheza na Ndanda mechi ya Ligi Kuu Bara leo saa 10:00 jioni kwenye Uwanja wa Uhuru jijini Dar es Salaam.
Kessy alisema ajali hiyo aliipata jana mchana akiwa kwenye mizunguko yake binafsi.
Kessy alisema, aliikodi bodaboda hiyo alipoitwa Makao Makuu ya Yanga yaliyopo katika makutano ya Mitaa ya Jangwani na Twiga lakini kabla ya kufika alipata ajali eneo la Magomeni.
Alisema katika ajali hiyo amepata majeraha mbalimbali kwenye mwili wake ikiwemo sehemu ya kisigino na kwenye goti ambako amechubuka.
“Leo (jana) nimeshindwa kumaliza mazoezi ya asubuhi tuliyofanya kwenye Uwanja wa Polisi baada ya kusikia maumivu makali, yalikuwa maumivu
makali mno.
“Sidhani kama nitakuwepo katika mchezo wa kesho (leo) Jumamosi kwani licha ya kutomaliza mazoezi, bado nina maumivu labda itategemea na
nitakavyoamka kesho (leo).
“Ajali nimepata pale Magomeni bondeni kabla ya kufika klabuni Jangwani ambako nilikuwa nimeitwa na uongozi,” alisema Kessy.
Meneja wa Yanga, Hafidh Saleh, alisema ni kweli beki huyo alipata ajali wakati akielekea klabuni na kuongeza: “Kessy amepata ajali ya bodaboda na ameumia kisigino na goti, leo (jana) ameshindwa kuendelea na mazoezi kutokana na maumivu kuwa makali."
SOURCE: CHAMPIONI
0 comments:
Post a Comment