Ofisi ya mawakili ya Prime Attorneys
imevamiwa usiku wa manane na watu wasiojulikana ambao wameiba kasiki
lenye fedha na nyaraka. Mmoja wa mawakili katika ofisi hiyo, Hudson
Ndusyepo amesema ofisi yao imevunjwa na tayari ameenda polisi kutoa
taarifa.
Ndusyepo ambaye ni miongoni mwa
mawakili wanaomtetea mfanyabiashara maarufu Yusuf Manji katika kesi ya
uhujumu uchumi, amesema kabla ya wizi huo, waliohusika walimfunga mlinzi
kwa kamba.
Kampuni ya Prime Attorneys katika
tovuti yake inaeleza ilianzishwa mwaka 2010. Ofisi za kampuni hiyo zipo
Jengo la Prime House lililopo Mtaa wa Tambaza, Upanga jijini Dar es Salaam.
Ofisi hizo zipo kwenye jengo la ghorofa
tano lililopo jirani na Taasisi ya Kuzuia na Kupambana na Rushwa
(Takukuru) wilayani Ilala.
Leo Asubuhi barabara ya kuingia eneo
hilo ilifungwa kwa muda na polisi ambao walitumia magari yao kuziba njia
na kuweka uzio wa utepe wa rangi ya njano.
Jengo la Prime House lina ofisi za kampuni mbalimbali, zikiwemo za mawakili, duka la dawa na sehemu ya kufanya mazoezi gym.
Kamanda wa Polisi Mkoa wa Ilala, Salum Hamduni amethibitisha tukio hilo akisema limetokea kati ya saa nane na saa tisa usiku wa kuamkia leo Jumanne.
“Kwa sasa siwezi kusema wahalifu hawa
walilenga ofisi gani maana zipo nyingi katika jengo lile. Naomba mtupe
nafasi tufanye uchunguzi kisha tutawapa taarifa,” amesema Kamanda Hamduni.
0 comments:
Post a Comment