Tuesday 12 September 2017

OMOG ATETEWA SIMBA

Dar es Salaam. Kiungo wa zamani wa Simba, Shekhan Rashid amewataka mashabiki wa klabu ya Simba kumpa muda Kocha Joseph Omog badala ya kumhukumu mapema.
Mashabiki wa Simba wamekuwa wakipaza sauti kushinikiza uongozi kumfukuza Omog kwa madai ameshindwa kuiongoza timu hiyo iliyofanya usajili mkubwa uliogharimu zaidi ya Sh13 bilioni.
Akizungumza na gazeti hili jana, Shekhana alisema ni vigumu kwa kocha yeyote kutengeneza timu imara kwa haraka, hususani anapokuwa na kikosi chenye wachezaji wengi wapya.
“Ni mazoea ya mashabiki kutaka vitu vizuri kwa haraka, Simba imesajili wachezaji wengi wanahitaji muda kuzoeana kuliko kuanza kuwalaumu mapema,” alisema Shekhan, aliyewahi kuitumikia Azam.
Simba imewasajili wachezaji wenye majina makubwa; Emanuel Okwi, John Bocco, Erasto Nyoni, Juma Luizio, Haruna Niyonzima, Shomari Kapombe, Aishi Manula, Ally Shomari na Jamal Mwambeleko lakini mashabiki bado hawaridhishwi na kiwango kinachoonyeshwa na timu yao licha ya kufunga mabao saba katika mechi mbili za Ligi Kuu.
“Simba haijaanza vibaya Ligi Kuu, kinachotakiwa ni mwalimu kuangalia wachezaji gani watakaomfaa kwenye ushambuliaji. Pia wachezaji wenyewe wasichezee majina, wajitoe na kujituma,” alisema Shekhan ambaye kwa sasa anaishi nchini Sweden.
Simba inajiandaa na mchezo ujao wa Ligi Kuu dhidi ya Mwadui utakaochezwa Jumamosi ijayo kwenye Uwanja wa Taifa, jijini Dar es Salaam.
Share:

0 comments:

Post a Comment

Ads

Blog Archive