Yanga
wanafanya mambo mawili kwa wakati mmoja. Wanaendelea na Ligi na tayari
wameanza usajili wa dirisha dogo. Unavyosoma hapa dakika hii tayari beki
aliyeletwa na kiungo mpya wa Yanga, Papy Tshishimbi, yupo kwenye ardhi
ya Dar es Salaam. Mchezaji huyo aliyekuja kwa majaribio, ametua usiku
wa kuamkia leo Ijumaa na anaitwa Kayembe Kanku Fiston akitokea klabu ya
SM Sanga Balende yenye makazi yake nje ya Jiji la Kinshasa, Jamhuri ya
Kidemokrasia ya Congo.
Mchezaji huyo amepishana na
kocha aliyetakiwa kumfanyia majaribio George Lwandamina ambaye imeelezwa
kwamba amekwenda kwao kwa dharura baada ya kufiwa na baba yake mzazi na
kwamba atarejea Bongo Jumapili.
Tshishimbi
amewahakikishia Yanga kwamba mchezaji huyo ni fundi na wataona yake
kwenye majaribio ambayo atayaanza baada ya kocha kurejea. Amewaambia
viongozi kuwa akishirikiana na kina Kelvin Yondani, Yanga itakuwa imara
sana nyuma.
Kuondoka kwa Lwandamina kutamfanya Fiston
kuanza majaribio yake akiwa chini ya makocha watatu wasaidizi wa kikosi
hicho; Shadrack Nsajigwa,Noel Mwandila na Juma Pondamali, lakini bado
akisubiri kuthibitisha uwezo wake kwa Lwandamina ambaye usiku na mchana
anaomba Novemba ifike dirisha dogo lifunguliwe asajili beki.
Taarifa
kutoka ndani ya Yanga ni kwamba Fiston atajaribiwa kwa wiki mbili
ambapo endapo uwezo wake utakubalika, atasaini mkataba wa awali na Yanga
na kurejea klabuni kwake.
Imeelezwa kuwa atarejea tena
nchini kuja kujiunga na mabingwa watetezi hao wa Ligi Kuu Bara wakati
wa usajili wa dirisha dogo la usajili likalaofunguliwa Novemba.
Fiston
anamaliza mkataba wake na Sanga Balende mwezi huu ambapo tayari
Tshishimbi ameliambia Mwanaspoti kuwa beki huyo amezuia kuendelea na
mazungumzo ya kuongeza mkataba mpya na klabu yake hiyo akisubiri kujua
hatma yake na Yanga.
Yanga inamsaka mrithi wa Vincent
Bossou aliyenyimwa mkataba mpya, licha ya awali kuwajaribu mabeki
watatu katika dirisha lililopita, ilishindwa kukubaliana na uwezo wao.
Hali
hiyo ndiyo iliyowalazimisha mabosi wa Jangwani kiasi cha kumuuliza
Tshishimbi endapo anamjua beki yeyote shoka anayefaa na ndio wakapewa
jina la Fiston.
0 comments:
Post a Comment