MSHAMBULIAJI wa Yanga, Obrey Chirwa na kiungo wa Singida United, Deus
Kaseke wameruhusiwa kucheza mechi za Ligi Kuu Bara kufuatia kutokutwa
na hatia katika tuhuma iliyokuwa ikiwakabili ya kumwangusha mwamuzi
Charles Ludovic katika msimu uliopita dhidi ya Mbao FC.
Kamati ya Nidhamu ya Shirikisho la Soka Tanzania (TFF) ambayo
imepitia shauri hilo imemkuta na hatia aliyekuwa kiungo mshambuliaji wa
Yanga, Simon Msuva ambaye kwa sasa anacheza katika Klabu ya Diffa Al
Jadida ya Morocco baada ya ushahidi kuonyesha kuwa ndiye aliyemsukuma
mwamuzi hivyo kupewa onyo kali.
Makamu Mwenyekiti wa Kamati ya Nidhamu ya TFF, Peter Hellar amesema
kamati yake haikuwakuta na hatia wachezaji Chirwa na Kaseke katika
shitaka hilo kupitia ushahidi mbalimbali walioutazama na badala yake
Msuva ndiye aliyekutwa na kosa ambapo kwa mujibu wa sheria alitakiwa
kukosa mechi tatu lakini kwa sasa amepewa onyo.
“Kamati ilitoa nafasi kwa walalamikiwa na walalamikaji kutoa ushahidi
ambapo ushahidi mwingine uliotumika ni video na kamati na ripoti ya
kamisaa na mwamuzi na kwa baadhi ya wachezaji aliyekuwa ni Chirwa na
Kaseke lakini Msuva hakuwepo kutokana na kutokuwepo nchini.
“Kamati ilipopitia shauri hilo ilimkuta Msuva ndiye mwenye hatia
ambapo alionekana akimwangusha mwamuzi, hivyo anatiwa hatiani kwa ibara
ya (49) (1) B ambapo chini ya kifungu hiki anatakiwa kukosa si chini ya
mechi tatu, lakini kwa upande wa wachezaji waliobakia kamati haikuwakuta
na hatia.
“Hata hivyo kamati ya ligi ilitoa adhabu kabla ya kamati ya nidhamu
kinyume na taratibu hivyo ni vyema TFF kupitia kamati zake ikafanya
maamuzi haraka mara baada ya tukio kutokea ili kuepuka jambo kama hili,”
alisema Peter.
Aidha, Ofisa Habari wa TFF, Alfred Lucas alisema Msuva aliwasili
nchini jana baada ya kufanikiwa kupata viza, tayari ameshajiunga na
wenzake wa Taifa Stars kuivaa Botswana.
0 comments:
Post a Comment