WAKATI Yanga
ikiwa katika usingizi wa pono, watani zao Simba wapo mbioni kutengeneza
mamilioni ya fedha kupitia mtaji wa mashabiki wao ndani na nje ya nchi.
Simba
iliyopo katika hatua nzuri ya kuhama kutoka mfumo wa wanachama kwenda
katika Hisa, inatarajia kuingiza fedha za maana kutokana na uwekezaji
wake katika digitali.
Mpaka sasa, Simba inayoongoza kwa
mapato ya nje ya uwanja ikiwa inaingiza Sh351 milioni kutoka katika
majengo yake pale Kariakoo, Sh100 milioni ya kipindi cha Simba TV
kinachorushwa moja kwa moja na Azam TV.
Simba
inayoongoza kwa kutwaa mataji ya Afrika Mashariki na Kati (Kagame Cup)
ikifanya hivyo mara sita, inaingiza pia zaidi ya Sh36 milioni kwa mauzo
ya jezi zake, pia ikipanga kuboresha zaidi biashara hiyo ili ivune
maradufu tofauti na sasa.
Ukiachana na fedha hizo za
mboga hapo juu, Simba iliingia mkataba wa biashara na kampuni ya EAG
Group ambayo sasa iko mbioni kufanya biashara ya digitali ambayo itaipa
klabuni hiyo mamilioni na kuifanya kuwa kwenye anga za kimataifa.
Uwekezaji Simba App
Simba
inatarajiwa kupiga mkwanja wa maana kupitia Simba APP ambayo inatoa
taarifa rasmi za klabu hiyo kwa gharama nafuu ukilinganisha na vyanzo
vingine vya habari.
App hiyo ambayo ipo chini ya EAG Group tayari imepakuliwa na watu 121,000, ikiwa ni miezi mitano tu tangu kuzinduliwa.
Mkurugenzi
wa kampuni hiyo, Imani Kajula anasema kwa siku kati ya watu 1,000-2,000
wanapakua App hiyo jambo ambalo linawapa imani kwamba huenda wakafikia
watu 200,000 mwakani.
“Sio uwekezaji mdogo, mpaka sasa
tumetumia zaidi ya Sh 400 milioni kuifikisha App hapo ilipo. Imefanyiwa
kazi na watu kutoka Afrika Kusini na Israel, inahitaji uvumilivu na
subiri kufanya hii biashara,” anasema Kajula.
“Tunatazamia
idadi ya watu itaongezeka zaidi. Kwa sasa tunapatikana kwenye simu za
Android, lakini tumeanza pia mchakato wa kuitengeneza App itakayotumika
pia kwenye simu za Apple na nyingine za Kimarekani,” anaeleza.
Kuonyesha mechi
Kajula
anasema tayari kampuni yake imeingia makubaliano na Azam TV, ili kuweza
kuonyesha mechi za Simba za Ligi Kuu Bara pamoja na zile za hatua za
awali za mashindano ya kimataifa na kwa kila mechi mtu atalipia Sh1,000.
“Tayari
tumenunua vifaa vya kurusha mechi moja kwa moja na kwa wiki sasa
tumekuwa tukivifanyia majaribio. Vilichelewa kidogo, tulipanga kuanza
navyo wakati wa Simba Day,” anaeleza.
“Tunatazamia kama
robo ya watu waliopakua App yetu watatazama mechi basi tutakuwa
tunaingiza hadi Sh40 milioni kwa mechi moja,” anasema.
Kutokana
na makadirio hayo, huenda App hiyo ikaingiza hadi kiasi cha Sh600
milioni kwa mwaka kutokana na kazi hiyo ya kuonyesha mechi, endapo robo
tu ya watu waliopakua App hiyo watalipia kuona mechi.
Malipo ya Kawaida
Mbali
na kuonyesha mechi, Simba APP kwa sasa inatoa taarifa rasmi za Simba,
picha za mnato na video za mahojiano na wachezaji pamoja na watu wa
Simba, habari ambazo kwa mwezi zitakuwa zikilipiwa Sh2,000 tu.
“Kama nusu tu ya watu waliopakua App watalipia, basi tutapata zaidi ya Sh120 milioni kwa mwezi,” anasema.
Kwa
sasa App ya Simba ina kurasa nne ambazo ni Simba News inayotoa taarifa
za maandishi na picha za mnato, Simba Live inayotoa matukio ya video ya
timu hiyo ambapo, wameunganisha na mtandao wa Youtube.
Ukurasa
mwingine ni Simba Exclusive na huwekwa video za mahojiano maalumu na
wachezaji na viongozi wa klabu hiyo. Kwa makadirio huenda App hiyo ikawa
inaipatia Simba zaidi ya fedha za udhamini wa SportPesa sasa ambao kwa
mwaka wamewapa Sh950 milioni.
Simba Day
Kampuni
hiyo ya EAG ndiyo imekuwa ikisimamia tamasha la Simba Day ambapo, mwaka
huu limeweka rekodi ya kupata watazamaji 52,000, idadi kubwa kuliko
wanaojitokeza kutazama mechi za Simba na Yanga sasa.
“Ukitazama
kwa nje unaweza kuona kawaida, lakini tumeweka fedha nyingi katika
matangazo na kuitangaza Simba Day. Mwaka jana tulikuwa na watazamaji
46,000 lakini namba imeongezeka sana mwaka huu.
“Gharama
zilikuwa ni nyingi, tumetangaza kwenye redio na televisheni,
tuliwatumia pia mastaa kadhaa. Pia kuwaleta Rayon Sports hapa ilikuwa
gharama kubwa,” anaeleza.
Mauzo ya jezi
“Tunashukuru
Simba imeanza kupata faida kutokana na jezi zake. Changamoto ni nyingi
na bado hatujaweza kufikia juu sana, lakini tunakwenda vizuri. Mfano
sasa jezi ya Simba inavutia, inapendwa sana na mashabiki.
“Tunazidi
kuimarisha maeneo kadhaa, lakini hata hivyo natazama zaidi hili soko la
kwenye mtandao, App itatupa fedha nyingi. Tunataka kuuza tiketi za
mechi za Simba kwenye App yetu pia, tunatengeneza viza kwa watu wa nje
waweze kulipia,” anaeleza.
SOURCE; MWANASPOT
0 comments:
Post a Comment