AMA kweli hakuna ufalme unaodumu milele! Beki Mohammed Hussein ‘Tshabalala’
alikuwa kama mfalme wa nafasi ya kushoto msimu uliopita pale Simba na
aliweka rekodi ya kucheza mechi zote za ligi, lakini mambo yamebadilika
msimu huu, amepata mpinzani na amepigwa benchi mechi mbili mfululizo
kwenye ligi.
Juzi Simba ilicheza dhidi ya Azam FC kwenye Uwanja wa Azam Complex, Chamazi jijini Dar na kutoka suluhu. Tshabalala alikuwa benchi.
Tshabalala hadi sasa ameshindwa kufua dafu mbele ya beki mpya wa timu hiyo, Erasto Nyoni ambaye amejiunga na klabu hiyo hivi karibuni akitokea Azam FC.
Kocha Mkuu wa Simba, Mcameroon, Joseph Omog amekuwa akimpatia Nyoni nafasi ya kucheza kila wakati kutokana na kuonyesha uwezo mkubwa tangu alipojiunga na timu hiyo.
Akimzungumzia mchezaji huyo, Omog alisema:
“Nyoni ni mchezaji mwenye faida kubwa anapokuwa uwanjani, mbali ya
kucheza nafasi ya beki wa kushoto lakini pia ana msaada mkubwa kwa
mabeki wa kati na pindi tunapokuwa tunashambuliwa.
“Anajua kukaba vizuri lakini pia anajua kuanzisha mashambulizi, kwa hiyo ni mtu muhimu sana katika kikosi changu.
“Kuhusu Tshabalala ni mchezaji mzuri lakini siwezi kuwatumia wote kwa pamoja ila atacheza tu, mechi bado ni nyingi.”
0 comments:
Post a Comment