Mshambuliaji
wa Simba ya Dar es Salaam, Emmanuel Okwi amechaguliwa kuwa Mchezaji
Bora wa Agosti wa Ligi Kuu ya Vodacom Tanzania Bara msimu wa 2017/2018.
Okwi
alitwaa tuzo hiyo baada ya kuwashinda wenzake wawili katika uchambuzi
uliofanywa Dar es Salaam jana (Jumatano) na Kamati ya Tuzo ya Shirikisho
la Mpira wa Miguu Tanzania (TFF), kutokana na mapendekezo kutoka kwa
makocha wa viwanja mbalimbali ambavyo ligi hiyo inachezwa. Wachezaji
wote hao timu zao zilishinda.
Walioshindana
na Okwi katika hatua hiyo ya mwisho ni kiungo wa Mtibwa Sugar, Mohammed
Issa ambaye alisaidia timu yake kupata pointi tatu kwa ushindi wa bao
1-0 katika mchezo dhidi ya Stand United uliofanyika Uwanja wa Manungu,
Turiani, ambapo alikuwa nyota wa mchezo huo. Mwingine aliyeshindana na
Okwi ni Boniface Maganga wa Mbao FC.
Maganga
alitoa mchango mkubwa katika ushindi wa ugenini wa bao 1-0, ambao timu
yake iliupata dhidi ya Kagera Sugar kwenye Uwanja wa Kaitaba, Bukoba
ikiwa ni pamoja na kufunga bao hilo.
Ushindi
wa Okwi unatokana na kutoa mchango mkubwa katika mchezo wa Simba dhidi
ya Ruvu Shooting uliofanyika Uwanja wa Uhuru, Dar es Salaam na timu yake
kuibuka na ushindi wa mabao 7-0, huku Okwi akifunga mabao manne.
Pia
Okwi amekuwa mchezaji wa kwanza msimu huu kufunga hattrick (mabao
matatu katika mchezo mmoja) katika Ligi Kuu ya Vodacom inayoshirikisha
timu 16, ambapo hat trick hiyo alifunga ndani ya dakika 45 za kipindi
cha kwanza.
Mwezi huo ulikuwa na raundi moja tu iliyochezwa Agosti 26 na 27 mwaka huu ambapo kila timu ilicheza mechi moja.
Kutokana
na kutwaa tuzo hiyo, Okwi ambaye pia ni mchezaji wa timu ya Taifa ya
Uganda (The Cranes) atazawadiwa kitita cha Sh. 1,000,000 (milioni moja)
na Kampuni ya Vodacom Tanzania Plc.
0 comments:
Post a Comment