BAADA ya Wakili Joseph Makandege anayemtetea mtuhumiwa wa uhujumu
uchumi, Harbinder Singh Seth kuiambia Mahakama ya Hakimu Mkazi Kisutu
kuwa mteja wake huyo yupo hatarini kufa kutokana na maputo aliyowekewa
tumboni, siri nzito imefichuka, UWAZI linakupasha.
Wakili Makandege alidai mahakamani
hapo wiki iliyopita kuwa mahakama ilitoa amri mara mbili ili mteja wake
apelekwe Hospitali ya Taifa ya Muhimbili ili akatibiwe lakini magereza
hawajatekeleza amri hiyo. Gazeti hili lilimtafuta Dk. Godfrey Chale
ambaye amewahi kuhudumu katika hospitali mbalimbali jijini ikiwemo ya
Muhimbili na Temeke na kumuuliza maswali kadhaa kuhusiana na tatizo
linalosababisha mtu kuwekewa maputo tumboni, faida yake na athari zake,
na kwa nini yanawekwa?
Akitoboa siri hiyo Dk Chale alisema maputo hayo yanawekwa tumboni
kama tiba na yanaweza kukaa humo kwa muda mrefu, akafafanua kuwa maputo
hayo yaitwayo kitaalamu intra-gastric balloon, ni laini sana na yanaweza
kupasuka kirahisi kama mgonjwa hatafuatilia utaratibu wa uchunguzi wa
mara kwa mara kuona kama bado yapo sawa na yametengenezwa kwa kutumia
madini ya Silicon.
“Maputo huwekwa ndani ya tumbo la chakula na ndani yake huwekwa maji
safi ya chumvi yaitwayo sterile salt au saline solution. Puto
linapowekwa tumboni, hujaza nusu ya tumbo na muda wote aliyewekewa
huhisi tumbo lake limejaa.
Kazi ya maputo haya husaidia kudhibiti hamu ya kula na kujikuta
unakula kiasi kidogo sana cha chakula hivyo inakusaidia kudhibiti tatizo
la kuongezeka unene kwa kasi,” alisema. Ili kupata undani wa maputo
yanayowekwa tumboni, fuatana nasi katika maswali na majibu na Dk. Chale:
KWA NINI MTU ANAWEKEWA PUTO TUMBONI?
“Tiba ya kuwekewa puto inasaidia sana kudhibiti unene, ni njia ambayo
siyo ya upasuaji, inapotumika pia husaidia kumuepusha mhusika kupata
matatizo ya ini na figo. “Sababu za kuwekewa puto tumboni ni endapo mtu
yupo katika hatari ya kupata magonjwa makubwa yanayohusiana na unene
ambapo kitaalamu tunasema body mass index (BMI) yake inazidi 35 ambapo
inaweza kumsababishia apate kisukari, ini kujaa mafuta, kupanda kwa
shinikizo la damu, matatizo ya miguu na kwa mwanamke anapata vivimbe
katika vifuko vya mayai au polycystic ovary syndrome.
“Mtu mwenye BMI zaidi ya 35 huwa ni mfupi na mnene sana. Mtu anaweza
kuwekewa puto endapo tiba nyingine za kupunguza uzito au unene
zimeshindikana, iwe kudhibiti ulaji au matumizi ya dawa za kupunguza
unene kushindikana, na hawako tayari kupunguza unene kwa njia ya
upasuaji.
PUTO LINAFANYAJE KAZI TUMBONI?
“Puto linapunguza nafasi tumboni hivyo inakusaidia ukila kidogo
unahisi umeshiba. Mtu aliyewekewa puto anatakiwa ale chakula maalumu
chenye kiwango kidogo cha nishati, awe mara kwa mara karibu na daktari
wake, wauguzi na wataalamu wa lishe ili
kuhakikisha puto hilo linaendelea kuwepo bila tatizo.
kuhakikisha puto hilo linaendelea kuwepo bila tatizo.
NINI ATHARI YA KUWA NA PUTO TUMBONI?
“Mara nyingi watu wote waliowekewa puto huwa hawapati athari zozote
na wanaendelea na maisha yao kama kawaida ila ni muhumu kuwa karibu na
daktari wako kwa mawasiliano na endapo utahisi tatizo lolote basi toa
taarifa kwa daktari wako, muuguzi wako au mtaalamu wa lishe.
“Hata hivyo, matatizo yanaweza kutokea mara chache sana inaweza
kuumiza njia ya chakula kuanzia kinywani hasa wakati wa kuupitisha
lakini ni jambo linalotibika wakati huohuo. Siku za mwanzo baada ya
kuwekewa puto tumboni unaweza kujihisi vibaya tumboni, kichefuchefu na
kutapika lakini haiendelei kwa muda mrefu.
“Kwa kuwa ni kitu kigeni tumboni, mwanzoni utahisi tumbo linakuwa
zito, unacheua asidi mara kwa mara, maumivu ya mgongo na tumbo kujaa
gesi lakini baadaye hali hiyo inapotea.
JE PUTO LIKIPASUKA TUMBONI INAKUWAJE?
“Athari mbaya inayoweza kutokea ni endapo puto hilo litanywea lote au
kupasuka tumboni kwani husababisha puto hilo liende mbele na kuziba
utumbo na tiba yake ni upasuaji wa dharura wa tumbo.
“Kama katika ufanyaji uchunguzi wa mara kwa mara itaonekana puto
linaanza kunywea, au tunasema kitaalamu defleted, inamaanisha yale maji
ya chumvi yanapungua taratibu, basi puto hilo itabidi litolewe kama
lilivyowekwa.
“Kama umewekewa puto, basi hauruhusiwi kusafiri mbali na sehemu
walipo wataalamu wako waliokuwekea na endapo itakulazimu usafiri, basi
ni vizuri daktari wako akuruhusu na likitokea tatizo wasiliana naye mara
moja ili afanye mawasiliano na daktari wa mahali ulipo.
JE PUTO LINAWEZA KUKAA TUMBONI KWA MUDA GANI?
“Muda wa puto kukaa tumboni na kuendelea kufanya kazi ni miezi sita
hadi mwaka mmoja kutegemea na aina ya puto lililowekwa, maputo mengi
hukaa kwa miezi sita halafu yananywea. “Endapo puto ni la miezi sita,
basi lifuatiliwe na kutolewa kwa njia inayoitwa kitaalamu endoscopy.
Njia ya kuyaweka huitwa Endoscopic Intragastric Balloon Insertion, na
huwekwa tumboni puto moja hadi matatu na kama nilivyosema hukaa si chini
ya miezi sita tumboni.
KUNA AINA NGAPI ZA MAPUTO HAYO YA TUMBONI?
“Aina za maputo haya ni nyingi kama vile Spatz, Orbera na Bio
Enterics Intra-Gastric Balloon. NINI USHAURI WAKO? “Inashauriwa maputo
haya yasikae tumboni kwa zaidi ya miezi sita ili kuepusha kunywea na
kuleta madhara makubwa ikiwa ni pamoja na kupoteza maisha kama mgonjwa
atachelewa tiba.”
YAPO MADAI KUWA KUNA UVIMBE MWINGINE TUMBONI KAMA PUTO, JE NI KWELI?
“Ni kweli tatizo hilo kitaalamu huitwa spasmodic pains, ni aina ya
maumivu makali yanayohusisha mishipa ya fahamu na misuli. Maumivu haya
yana tabia ya kuja kwa ukali na kupotea , ni maumivu ya kukata,
yakitokea sehemu yeyote ya mwili lazima ukae na ushike sehemu hiyo.
“Spasmodic pains hutokea kwenye misuli ya miguu, ini, moyo, bandama,
kongosho na tumbo. Ni maumivu yanayowatokea watoto na watu wazima. Zaidi
maumivu haya hutokea tumboni sehemu yoyote lakini wengi hutokea upande
wa juu wa tumbo na wanawake hutokea upande wa juu na hata upande
wa chini kwenye kizazi hasa pale mwanamke anapokuwa kwenye siku zake,
mimba kutishia kutoka na wakati mwingine anapokuwa katika kipindi cha
upevushaji mayai au ovulation.
NINI TIBA YA TATIZO HILO?
“Tatizo la maumivu haya huchunguzwa hospitali kutegemea na sehemu
yanapojitokeza. Pamoja na kutibu chanzo dawa za kutuliza maumivu haya
zinaitwa Antispasmodic, pia zipo dawa za kupaka, kunywa na sindano,”
alisema Dk Chale. Seth na James Rugemalira wanakabiliwa na mashitaka 12
ya uhujumu uchumi kwa kula njama, kujihusisha na mtandao wa uhalifu,
kughushi nyaraka, kujipatia fedha kwa njia ya udanganyifu kutakatisha
fedha na kuisababishia serikali hasara ya dola za Marekani 22,198, 544.
60 na Sh. 309, 461,300, 158.27. Wote wapo rumande Gereza la Segerea.
0 comments:
Post a Comment