SIMBA
iliyorejea katika anga za kimataifa baada ya kukaa pembeni muda mrefu,
huenda ikawa na kibarua kizito katika mashindano ya Kombe la Shirikisho
Afrika mwakani, kwani licha ya kuikwepa TP Mazembe ya DR Congo, iko
mikononi mwa timu 10 vigogo Afrika.
Simba iliyotwaa
tiketi ya kushiriki mashindano hayo ya CAF kwa mara ya kwanza tangu
mwaka 2013, italazimika kuchuana na timu hizo huku Difaa el Jadida ya
Simon Msuva ikitarajiwa kuzengea kukutana na Yanga katika Ligi ya
Mabingwa.
Timu ambazo tayari zimefuzu na ambazo Simba
itahitaji kutumia akili ya ziada endapo itakumbana nazo ni Zamalek na El
Masry kutoka Misri pamoja na Club Africans na Ben Guerdane za Tunisia.
Sio
hizo tu, ipo USM Algers na CR Belouizdad za Algeria ambazo tayari
zimepata tiketi ya kushiriki mashindano hayo ya pili kwa ukubwa Afrika
katika ngazi ya klabu.
Timu nyingine ambayo tayari
imetwaa tiketi hiyo ni Cape Town City na Super Sports United za Afrika
Kusini na timu ya zamani ya Joseph Omog, AC Leopards ya Congo na Raja
Casablanca ya Morocco.
Katika mashindano hayo ya CAF
timu zitakazofuzu hatua ya makundi zitakuwa zimejihakikishia kupata dola
150,000 (Sh331 milioni) hadi Dola 239,000 (Sh527 milioni).
Kwa
upande mwingine, watani zao Yanga watakuwa na kibarua kigumu zaidi
katika Ligi ya Mabingwa Afrika kwani kuna uwezekano wakakutana na Msuva
akiwa na El Jadida yake waliokata tiketi sambamba na Wydad Casablanca.
Nyingine
ni Al Ahly na Misr Lel Makkasa za Misri, Esperance na Etoile Du Sahel
za Tunisia, TP Mazembe na AS Vita za DR Congo, ES Setif na MC Alger
iliyoitoa Yanga kwa jumla ya mabao 4-1 kwenye play-off za Kombe la
Shirikisho Afrika.
Nyingine zitazoikabili Yanga ni
Mamelodi Sundowns na Bidvest Wits za Afrika Kusini, ASEC Memosas na
Mbabane Swallows aliyoichezea kiungo wake mpya, Kabamba Tshishimbi.
0 comments:
Post a Comment