Mbunge wa Jimbo la Arusha Mjini, Godbless Lema jana alihojiwa na polisi kwa zaidi ya saa tatu, kutokana na kauli alizotoa kwenye mikutano ya hadhara iliyomalizika hivi karibuni.
Moja ya sababu za kuhojiwa kwake ni kutamka kwamba Mkuu wa Wilaya ya Hai, Gelasius Byakanwa na wa Wilaya ya Chemba, Saimon Odunga “ni wajinga na wapumbavu” kutokana na kufanya matendo ambayo ni kinyume na ubinadamu ambayo yanamvunjia heshma Rais John Magufuli aliyewateua.
Lema alikuwa kituo kikuu cha polisi cha Arusha kuanzia saa 7:14 mchana hadi saa 10:00 jioni kwa mahojiano katika ofisi ya Mkuu wa Upelelezi wa Mkoa (RCO).
Akizungumza na waandishi wa habari mara baada ya kuachiwa kwa dhamana hadi Septemba 19, Lema alisema ni kweli kitendo alichofanya mkuu huyo wa wilaya ya Hai cha kumuweka rumande mwalimu aliyeshindwa kumtaja jina lake, ni cha udhalilishaji na hakiendani na hadhi ya mkuu wa wilaya.
Lema pia alisema kitendo cha mkuu mwingine wa wilaya ya Chemba, Odunga kumchapa viboko mzazi ambaye mtoto wake alirusha jiwe kwenye gari, ni cha ajabu na udhalilishaji mkubwa na hakuna jina jingine la kumuita zaidi ya “mjinga”.
“Nimewaeleza polisi ni kweli nilisema na nikawaambia nina imani na Rais John Magufuli kuwa hataendelea kuwaacha salama wakuu hawa wa wilaya hizo kwa kuwa walifanya matendo ambayo ni ya kipumbavu na kijinga licha ya kuomba msamaha,” alisema mbunge huyo anayeongoza Jimbo la Arusha Mjini kwa kipindi cha pili.
Lema alisema anakumbuka alimshauri Rais katioka mikutano yake awachukulie hatua viongozi hao kwa kuwa wanafifisha jitihada zake.
“Matendo haya ni ya kinyama na udhalilishaji na hayana lugha nyingine ya kuyakemea zaidi ya kuyaita ni ya kipumbavu na kijinga,” alisema.
Kamanda wa polisi mkoa wa Arusha, Charles Mkumbo hakupatikana jana kueleza sakata hilo.
Hata hivyo, ofisa mmoja wa polisi mkoani hapa alithibitisha kuhojiwa kwa Lema na kueleza kuwa ameachiwa kwa dhamana ya polisi kwa kuwa uchunguzi unaendelea.
0 comments:
Post a Comment