Monday, 4 September 2017

MSUVA AISHANGAA YANGA

Simon Msuva
KUFUATIA kuitungua timu ya taifa ya Botswana mabao mawili, winga wa kimataifa wa Tanzania, Simon Msuva, ameshangazwa na mashabiki wa Yanga wanaodai kuwa ameacha pengo kubwa katika timu hiyo.

Juzi Jumamosi, Msuva akiwa na Taifa Stars alifanikiwa kufunga mabao mawili peke yake katika mchezo wa kirafiki dhidi ya Botswana uliopigwa kwenye Uwanja wa Uhuru, Dar.

Katika mchezo huo, Taifa Stars iliibuka na ushindi wa mabao 2-0 yaliofungwa na kiungo huyo aliyejiunga na Klabu ya Difaa El-Jadida kwa mkataba wa miaka mitatu akitokea Yanga.

Kelele za mashabiki wa Yanga zilianza katika mchezo wa Ngao ya Jamii dhidi ya Simba ambao ulimalizika kwa Yanga kufungwa kwa penalti 5-4 kabla ya kutoka sare ya bao 1-1 dhidi ya Lipuli ya Iringa ukiwa ni mchezo wa Ligi Kuu Bara.

Akizungumza na Championi Jumatatu, Msuva alisema kuwa kuondoka kwake katika timu hiyo hajaacha pengo lolote kwa kuwa timu yake imefanya usajili mkubwa ambao anaamini inaweza kufanya makubwa katika ligi ya msimu huu.

“Kweli nimeondoka mimi, Haruna Niyonzima, Vincent Bossou na Deus Kaseke lakini kwa upande wangu naona Yanga bado nzuri, kikubwa ni kuangalia ni sehemu gani wanakosea kama wachezaji au vipi kwa sababu mwalimu anaona makosa yapo sehemu gani ili waweze kufanya makubwa, maana ni kitu ambacho kinawezekana.

“Najua watu wanasema kuwa Yanga kuna pengo la nafasi yangu lakini kwa upande wangu siamini hilo, kwa sababu wapo wachezaji wengi ambao wana uwezo wa kuziba hilo pengo ambalo wao wanalisema kwani haitakuwa vyema kuchukulia kutokuwepo kwangu ndiyo timu ifanye vibaya maana naamini timu ipo sawa idara zote,” alisema Msuva.
Share:

0 comments:

Post a Comment

Ads

Blog Archive