BONDIA Floyd Mayweather amefunguka mengi kuhusu maisha yake ya ndondi
na binafsi ikiwemo kuhusu kama atarejea kwenye ndondi au ndiyo
amestaafu ukweli.
Mayweather ambaye alitangaza kustaafu kupigana mwaka 2016 kisha
kuamua kurejea mwaka huu na kupigana pambano dhidi ya Conor McGregor
likiwa ni pambano lake 50, inaaminika ndiye bondia mwenye mafanikio
makubwa kifedha kuliko wote kuwahi kutokea.
Katika pambano hilo lililopewa jina la pambano la fedha, Mayweather
alishinda na hivyo kujiandikia rekodi ya kucheza mapambano 50 akishinda
yote, huku akiingiza kiasi kikubwa cha fedha kutokana na mikataba
mbalimbali.
Akifanya mahojiano na mtangazaji Diego wa kwenye mtandao wa YouTube
ambaye amekuwa ni maarufu kwa kutumia kuhoji kupitia katuni (yaani
katuni ndiyo inakuwa kama inazungumza na mgeni), Mayweather amedai kuwa
hadi sasa ana wapenzi saba na ana magari 25 ya kifahari ambayo yote yapo
Las Vegas.
Magari hayo ni yale ambayo anayo kwenye jiji hilo tu, yakiwemo
Bugatti na Ferrari ambayo thamani yake ni zaidi ya shilingi bilioni 1
kila moja.
Mayweather amesisitiza kuwa, pambano lake na McGregor lililofanyika
mwezi uliopita ndilo lilikuwa la mwisho kwake na hana mpango wa kurejea
ulingoni kupigana.
“Hilo lilikuwa pambano la mwisho kwangu kupigana, uhakika hilo
lilikuwa la mwisho, pambano lijalo labda nitapigana katika dunia
nyingine,” anasema Mayweather ambaye elimu yake ya dunia ni ya kawaida
kwa kuwa aliacha shule mapema na kujiingiza kwenye ndondi.
Mahojiano hayo yalifanyika mbele ya ukumbi wa usiku wa Mayweather
unaojulikana kwa jina la Girl Collection unaopatikana Las Vegas.
Alipoulizwa kuhusu mpenzi wake, alisema yeye ni mwanaume ambaye hawezi kuwa mwaminifu kwa mwanamke mmoja.
“Nina wanawake wangapi? Nafikiri ni kama saba hivi ambao wana bahati kuwa na mimi.
“Huwa nikiamua ninatoka na mmoja wao kwenda kula, mwingine tunasafiri
pamoja, kuwa na mwanamke mmoja ni sawa na kutokuwa na mpenzi kwa kuwa
muda wowote unaweza kumkosa,” anasema.
Alipoulizwa juu ya kiasi cha fedha ambacho anacho kwenye akaunti
zake, Mayweather alisema anazo akaunti kadhaa za benki na hakumbuki hasa
salio lake katika kila akaunti.
“Nina zaidi ya dola milioni 200 nyingine dola milioni 300,” anasema
bondia huyo ambaye licha ya kujulikana kupenda kuonyeshea fedha zake
lakini pia ni hodari katika kupambana kutafuta mafanikio hasa kwenye
suala la ndondi.
Ikumbukwe kuwa katika pambano lake la mwisho dhidi ya McGregor,
bondia huyo Mmarekani inaelezwa kuwa aliingiza zaidi ya pauni milioni
100 ndani ya usiku mmoja tu.
Alipoulizwa juu ya ushauri anaoweza kutoa kwa mwanaume aliyeoa, akashauri huku akicheka kwa kusema: “Mpe talaka mkeo.”
“Ukitaka kumwambia au kutafuta njia ya kumuacha mkeo, mlete kwenye
hii klabu yangu (ni klabu ya wanawake wanaocheza wakiwa nusu utupu)
kisha mwambie ni sehemu pekee ambayo huwa unapenda kuitembelea. Ukifanya
hivyo hutakuwa na haja ya kumpa talaka, ataondoka mwenyewe.”
Kutokana na kauli yake ya kuwa na uhusiano na wanawake saba,
tujikumbushe baadhi ya wanawake maarufu aliowahi kuwa na uhusiano nao na
baadhi bado yupo kwenye uhusiano nao wa kimapenzi:
Abi Clarke
Huyu ni mtangazaji wa runinga na staa wa showbiz ambaye inaelezwa
kuwa amekuwa na uhusiano na Mayweather, hawajawahi kuweka wazi lakini
taarifa zimekuwa zikijulikana wawili hao wana uhusiano. Uhusiano wao
ulianza mwaka jana wakati Abi alipokuwa Las Vegas kwa ajili ya
mapumziko.
Rmarni Ellis
Binti huyu ni raia wa Uingereza ambaye ana umri wa miaka 20,
alikutana na Mayweather wakati bondia huyo alipotembelea nchini mwake.
Inadaiwa uhusiano wao uliisha kimyakimya lakini hakuna taarifa zaidi.
Mara baada ya kukutana Uingereza, Mayweather akamsafirisha Rmarni hadi Marekani ili waweze kuwa pamoja.
Licha ya ubilionea wake alionao lakini Mayweather alianguka kwenye
penzi la mrembo huyu ambaye kazi yake ni kuuza dukani na ambaye alikuwa
akilipwa pauni 6.50 kwa saa.
Binti huyo ambaye naye ana umri wa miaka 20 alikutana na bondia huyo kwenye mishe zake hizohizo za dukani.
Yahaira Vianne Ochoa
Huyu ni mwanamitindo ambaye hata baada ya pambano lake la mwisho,
wawili hao walionekana kuwa pamoja na walipiga picha wakiwa pamoja
Doralie Medina
Huyu amedumu muda mrefu kidogo na Mayweather na mara kadhaa aliwahi kuonekana hadharani akiwa na bondia huyo.
Medina anajulikana kwa kuwa na umaarufu mkubwa kwenye mitandao ya
kijamii. Inaelezwa kuwa mrembo huyu anajua vizuri kuzitumia fedha za
Mayweather. Mwaka 2014 katika tuzo za BET, mrembo huo aliingia ukumbini
akiwa ametupia nguo za dola 70,000.
Alikuwa ametupia vitu vingi vya thamani kubwa ikiwemo cheni na viatu.
Pia Mayweather aliwahi kumnunulia gari aina ya Rolls Royce wakati wa
siku yake ya kuzaliwa Julai 2014.
Melissa Brim
Huyu ni mama wa mtoto wake wa kike, waliachana na kama ilivyo kawaida
ya mastaa wengi, amekuwa na migogoro ya mara kwa mara na mzazi mwenza
huyu.
Josie Harris
Huyu pia ni mzazi mwenza wa bondia huyo, hawapo pamoja lakini mara
kadhaa aliwahi kutofautiana na Melissa Brim, walishambuliana mitandaoni
kisa kikiwa ni wivu wao kwa Mayweather.
Alidumu na Mayweather kwa miaka mingi tangu akiwa anachipukia kwenye
ndondi lakini anakiri kuwa uhusiano wao ulivurugika na wakatofautina kwa
kuwa maisha yake hayakuwa mazuri pindi akiwa ndani ya penzi la bondia
huyo.
0 comments:
Post a Comment