KADA mkubwa wa Chama cha Demokrasia na Maendeleo (Chadema), Dk.
Lawrence Masha amesema hana shida kabisa na Katiba ya Jamhuri ya
Muungano wa Tanzania iliyopo sasa huku akiwataka watu waache kupotosha
umma kuhusu jambo hilo. Akichangia mjadala kwenye Kongamano la Meza ya
Uzalendo, Jumamosi ya wiki iliyopita ndani ya Ukumbi wa Nkurumah uliopo
Chuo Kikuu cha Dar es Salaam, Masha ambaye kitaaluma ni mwanasheria,
alisema haoni ubaya wala kasoro za katiba hiyo na kwamba jambo muhimu la
kufanya ni kuhakikisha watu wanakuwa wazalendo kwa nchi yao kuanzia
viongozi na raia wa kawaida.
Akizungumza kwa kujiamini, mwanasiasa huyo aliyewahi kushika nafasi ya uwaziri
wa mambo ya ndani na ubunge wa Nyamagana, Mwanza aliweka wazi kuwa
endapo kila mwananchi atakuwa mzalendo kwa taifa lake, yaani
viongozi kutimiza majukumu yao kwa moyo wa kizalendo na wananchi
wanafanya yaliyo upande wao kwa kujitoa kikamilifu kwa taifa, hakuna
sababu za kulaumu na kukosoa katiba iliyopo na kwamba hata kama
itatungwa nyingine mpya yenye uzuri wa kila aina, kama hakuna uzalendo
wa kweli ni kazi bure.
“Binafsi sioni kabisa tatizo ya katiba iliyopo, unajua muhimu sana ni
kuwa na uzalendo wa kweli kwa taifa letu, mimi ni mwanasheria kitaaluma
na nyote hapa mnajua, naisoma katiba yetu vizuri sana na haina shida,
msisitizo ni kuwa na uzalendo kuanzia kwa viongozi na raia wa kada zote
kwa kuipenda sana nchi yetu, kujifunza mambo mengi yanayohusu taifa letu
leo.
“Ni aibu kama nyinyi nyote hapa hamumjui mtu kama Mti Mkavu au Black
Mamba, tatizo tulilonalo sisi Watanzania ni kukosa uzalendo na kutopenda
kujifunza kwa dhati mambo yanayohusu taifa letu, mtu asipotoshe kuwa
katiba ina ubaya,” alisema Masha.
Aidha, kwa upande mwingine, Masha alionesha hisia za wazi kukerwa na
kitendo cha baadhi ya watu kumuita mpinzani kwa sababu ya kutofautiana
kimawazo kuhusu namna ya kuijenga nchi na kwamba anamtambua na
kumheshimu Rais Dk. John Magufuli kama rais na kiongozi wa taifa.
“Hakuna kitu kinanikera kama kuitwa mpinzani, nakereka sana kwa
kweli, tofauti zetu za kivyama na mambo ya mtazamo wa namna ya kuijenga
nchi yetu hakumaanishi mimi ni mpinzani, namheshimu Rais Magufuli na
yeye ndiye kiongozi wa taifa langu kwa sasa, tuacheni kuvurugwa na
utofauti wa vyama, sisi sote ni Watanzania na tuwe na uzalendo kwa taifa
letu kwa kufanya yaliyo mema,” alisema Dk. Masha.
0 comments:
Post a Comment