KATIKA kuhakikisha kikosi cha Yanga kinamaliza tatizo la beki wa kati, mmoja wa wapenzi wa timu hiyo, Shabani Hussein ‘Papaa Ndama’,
jana alifika kwenye mazoezi ya timu hiyo na kufanya kikao cha siri
kilichokuwa na ulinzi mkali wa makomandoo na benchi la ufundi kufuatia
kutua kwa beki mpya, Fiston Kayembe raia wa DR Congo.
Bosi huyo inadaiwa ndiye aliyekuwa katika mipango ya kumleta kiungo kipenzi cha mashabiki wa timu hiyo, Papy Kabamba Tshishimbi, lakini pia amehusika kumleta Kayembe ambaye ni rafiki mkubwa wa Tshishimbi kwa ajili ya kufanya majaribio.
Ndama alifika kwenye mazoezi hayo
yaliyofanyika katika Uwanja wa Uhuru, Dar kwa usiri mkubwa kwa lengo la
kutaka kumuangalia beki huyo aliyeanza kufanya majaribio hayo ili kuziba
nafasi ya beki wa kati, Vincent Bossou raia wa Togo, akitokea katika
Klabu ya SM Sanga Balende.
Championi lilimshuhudia
bosi huyo aliyekuwa ameambatana na mtu mwingine wakiingia uwanjani hapo
kisha kukaa kwenye eneo la jukwaa kuu kufuatilia mazoezi hayo kabla ya
kufanya kikao cha siri na benchi la ufundi, ambacho kilikuwa na ulinzi
mkali wa makomandoo.
Chanzo cha kuaminika kutoka ndani ya uongozi wa timu hiyo, kililihakikishia Championi Jumatano:
“Ndama amekuja kwa ajili ya kumuangalia Kayembe kabla ya kuanza
harakati za kumsajili ili kuziba pengo la Bossou kwa sababu huyu
mchezaji ni rafiki yake na Tshishimbi.
“Unajua hata kuja kwa Tshishimbi jamaa
amehusika, sasa alimuuliza kuhusu beki, ndiyo Tshishimbi akamtaja
Kayembe kwa kuwa walikuwa pamoja DR Congo kabla ya kutimkia Mbabane
Swallows ambako aliuvunja mkataba wake kwa kuununua na kuja Yanga.”
Mara baada ya kumalizika kwa mazoezi hayo, Championi lilimshuhudia
bosi huyo akifanya kikao hicho na kocha George Lwandamina akiwa na
meneja wa timu, Hafidh Saleh katika eneo la kuegeshea magari nje ya
uwanja, kikao hicho kilitumia dakika kumi huku kukiwa na ulinzi mkali wa
baadhi ya makomandoo.
0 comments:
Post a Comment