Ikiwa
ni siku chache tangu atue Yanga, beki mpya wa timu hiyo, Gadiel Michael
amefunguka kuwa atahakikisha anawazima washambuliaji wa Simba, Emmanuel
Okwi na Shiza Kichuya watakapokutana wiki ijayo.
Simba
na Yanga zinatarajiwa kukutana katika mchezo wa Ngao ya Jamii, Agosti
23, mwaka huu, ambapo tayari presha imekuwa kubwa, Yanga wamefunga
safari kutoka Dar es Salaam hadi Unguja kwa ajili ya kambi kujiandaa na
mchezo huo.
Beki
huyo wa kushoto amejiunga na Yanga kwa mkataba wa miaka miwili akitokea
Azam FC ambapo juzi Jumamosi katika mchezo wa kirafiki uliopigwa kwenye
Uwanja wa Chamazi dhidi ya Ruvu Shooting alionyesha uwezo mkubwa wa
kukaba na kupandisha mashambulizi.
Gadiel alisema kuwa kwake
mchezo huo utakuwa ni wa kawaida na amejipanga kuwadhibiti wachezaji
hao watakaocheza kwenye eneo lake hadi kusahauliwa na mashabiki wa timu
yao.
“Nadhani
hiyo ndiyo mechi ambayo nitajitambulisha rasmi Yanga maana katika
kucheza kwangu mpira sijawahi kuogopa mechi kubwa hata siku moja wala
kuwahofia wachezaji, na hao ambao watakuwa wanafika kwenye eneo langu
wajue kabisa nitawazima kabisa siku hiyo.
“Lakini
hata wakati nacheza Azam, mechi za Simba na Yanga nilikuwa nikiaminiwa
kupewa nafasi kwa sababu kuna kitu ninachokionyesha, sasa Yanga nahitaji
kuaminika zaidi pia naamini Mungu ataniongoza kwa kila kitu katika
maisha yangu mapya,” alisema Gadiel.
Katika
siku za hivi karibuni, beki huyo amekuwa akionyesha uwezo wa juu hasa
alipokuwa akiichezea timu ya Taifa ya Tanzania, Taifa Stars, kiasi cha
kuaminiwa na kuwa na uhakika katika kikosi cha kwanza cha timu hiyo
licha ya kuwa ni chipukizi.
Usajili
wake kutua Yanga uliambatana na ugumu baada ya awali Azam FC kugoma
kumuachia kutokana na kuwa na mkataba ambao ulitarajiwa kumalizika
Desemba, mwaka huu, lakini baada ya mazungumzo baina ya klabu hizo,
akaachiwa kwa ada ya uhamisho wa shilingi milioni 10.
SOURCE: CHAMPIONI
0 comments:
Post a Comment