Monday, 14 August 2017

JULIO ASHITUKIA MBINU YA YANGA AISHITUA SIMBA

 
JAMHURI Kihwelo ‘Julio’ ambaye ni mnazi mkubwa wa Simba, amesema  mabeki wa Yanga, Nadir Haroub ‘Cannavaro’ na Kelvin Yondani, watashangaza wadau siku ya  mechi ya Ngao ya Jamii, Agosti 23, itakayochezwa Uwanja wa Taifa, Dar es Salaam.
“Simba, wasije wakajibweteka wakidhani, beki ya Yanga ni mbovu, ninachokiona ni kocha George Lwandamina, anakiandaa kikosi chake, kujifunga dhidi ya Ruvu, siyo sababu hayo ni  maandalizi tu, wapo kina Cannavaro na Yondani, wana uwezo wa juu na wazoefu.
“Huwezi kukibeza kikosi cha Yanga, wakati kipo kwenye maandalizi kwa sababu kocha anakuwa anampima kila mchezaji ili  kujua ubora na madhaifu yake, kujifunga ni mambo ya kawaida na hilo atalifanyia marekebisho ndani ya siku 10 zilizosalia,”alisema kocha huyo wa Dodoma FC.
Julio alisema  Simba , ndiyo ipo kwenye hatari zaidi tofauti na majina makubwa wanayoyaamini mashabiki kwa maana ya kikosi ni kipya kinatakiwa kukaa  kwa pamoja kwa muda mrefu, ili kutengeneza kombinesheni ya wachezaji.
“Simba ni timu mpya, kocha atakuwa na kazi ngumu kuliko Yanga, ambao wengi ni wazamani wameongezeka wachache, wageni, wajipange vilivyo kuendana na uhalisia wa uwanjani na si kishabiki,”alisema Julio ambaye ni mchezaji wa zamani wa Simba.
MSIKIE CANNAVARO
Naye nahodha wa Yanga, Cannavaro, alisema anaiamini beki yao kwani kujifunga dhidi ya Ruvu ni jambo la kawaida akitolea mfano kwamba hata Ulaya, inatokea “Ni kawaida na ujue haya ni maandalizi siyo kwamba tupo kwenye ligi.”
“Kocha anampa nafasi kila mchezaji, kujua anaweza akafiti wapi ni mapema sana kujaji mtu kwa sasa, ila kuhusu Ngao ya Jamii, tumejipanga na tunacheza mechi za kirafiki kujiweka sawa,”alisema mchezaji huyo mzoefu.
Kwa upande wa katibu mkuu wa Yanga, Boniface Mkwasa, alizungumzia maandalizi kwa ujumla kwamba yanaenda vizuri, wakitambua kwamba ni mechi ya ushindani wa hali ya juu, ila matarajio yao ni ushindi.
‘Tupo kwa ajili ya kushindana naamini tutafanikiwa kushinda mechi hiyo, najua Simba wanajipanga ila watakutana na muziki mnene wa wachezaji wa Yanga, kama kiongozi naona maandalizi yapo imara,”alisema
Emmanuel Martin ni straika wa timu hiyo, alisema kufungwa na Ruvu inasaidia kujifunza na kujua mapema mapungufu yapo wapi “Simba wakidhani kwa sababu Yanga, walijifunga na Ruvu ni mbovu, basi tutakutana Agosti 23, pale taifa ndipo watajua tupo vipi,”alisema.
Yanga, wamecheza mechi mbili za kirafiki jijini Dar es Salaam,  dhidi ya Singada United na kufanikiwa kuibuka na ushindi wa mabao 3-2, Uwanja wa Uhuru, huku wakijifunga  bao 1-0, dhidi ya Ruvu Shooting ya Masau Bwile, Uwanja wa Chamazi.
KOTEI ACHEKELEA
Kiungo wa Simba, Mghana James Kotei amezinasa kuwa beki wa Yanga, Abdallah Shaibu ‘Ninja’ amejifunga mwenyewe kwenye mechi ya kirafiki, akacheka na kumwonea huruma, lakini akasisitiza kwenye mchezo wao wa Ngao ya Jamii dhidi yao, watawachapa mengi tu.
Kotei amesema: “Ninachokiamini kwa Simba yetu hii, mbali na kushinda, Yanga tutawafunga mabao mengi tu na tuna kila sababu ya kufanya  hivyo. Ukiangalia timu yao kuanzia beki, kiungo na ushambuliaji, tunawazi.”
“Tena kwa beki yao ile. Nimesikia mechi ya kirafiki  waliyocheza beki kajifunga, ni huruma naona linapokukuta hili ni shida, lakini jambo kama hili watu wanatakiwa kuelewa inatokea tu,”alisema Kotei.
Share:

0 comments:

Post a Comment

Ads

Blog Archive