WAKATI machungu ya kupoteza shamba lake lenye ukubwa wa ekari 33
lililokuwa Mabwepande yakiwa hayajatuliwa, aliyekuwa Waziri Mkuu Katika
serikali ya awamu ya tatu, Frederick Sumaye amepoteza shamba jingine
mkoani Morogoro baada ya serikali kulichukua.
Halmashauri ya Wilaya ya Mvomero imelitwaa shamba la Sumaye lenye
ukubwa wa ekari 326 baada ya kupata kibali kutoka kwa Rais Magufuli kwa
madai kuwa hajaliendeza licha ya kupewa notisi ya kufanya hivyo.
Shamba la Sumaye la Mabwepande lilichukuliwa Novemba mwaka jana na
Mkuu wa Wilaya ya Kinondoni, Ally Hapi akifikia uamuzi huo baada ya
mmiliki wa shamba hilo kutoliendeleza kama notisi ya siku 90 aliyopewa
ilivyokuwa ikimtaka. Oktoba 28 Rais Magufuli alibatilisha umiliki wa
shamba hilo namba 3,074 lililopo Mabwepande. Shamba hilo lilikuwa na
hati namba 53086 na jina la umiliki lilikuwa ni Frankline Sumaye.
Mkurugenzi wa Halmashauri ya Wilaya ya Mvomero, Florent Kyombo jana
alisema kuwa Rais Magufuli amekubali kufutwa kwa umiliki wa shamba hilo
kupitia ilani ya ubatilisho ya Mei mwaka huu.
Kabla ya kutangaza uamuzi huo jana, Mkurugenzi huyo alisema kwamba
Sumaye alipewa notisi ya siku 30 ya kueleza sababu za kutoendeleza
shamba hilo kwa shughuli za kilimo kama lilivyosajiliwa, lakini maelezo
aliyetoa yalielezwa kuwa hayakuwa na mashiko kiasi cha kuweza kubadili
uamuzi huo.
Imeeleza kwa licha ya Sumaye ambaye ni Mwenyekiti wa CHADEMA Kanda ya
Pwani kuendeleza sehemu ndogo ya shamba hilo lakini amekiuka Sheria ya
Mipango Miji Namba 8 ya mwaka 2007 pamoja na Sheria ya Ardhi namba 4 ya
1999.
Kwa mujibu wa sheria hizo, Sumaye alitakiwa kulitumia shamba hilo kwa shughuli za kilim0 na si ufugaji.
Kyombo alisema kwamba, ndani ya miezi minne watakuwa wamemaliza
taratibu za kuligawa shamba hilo kwa wananchi ili waweze kufanya
shughuli za kilimo.
Kwa mujibu wa taarifa iliyoanza kusambaa kwenye mitandao ya kijamii
jana asubuhi ikionyesha kuandikwa na Sumaye, ilieleza tukio hilo la
kunyang’anywa shamba, akisema kuwa ni kutokana na sababu za kisiasa.
“Kwangu mambo siyo mazuri, mtakumbuka baada tu ya kuingia upinzani
serikali ilitishia muda mrefu kuchukua mashamba yangu bila sababu za
msingi, hata wakati wa kampeni baadhi ya viongozi wa CCM walitamka
hadharani kuwa huyu dawa yake ni kumnyang’anya mashamba yake. Shamba la
Mabwepande ekari 33 wameagiza wiki hii halmashauri iligawe kwa wavamizi
na wengineo.”
Aidha, Sumaye katika taarifa hiyo alionyesha kusikitishwa na madai
kuwa shamba hilo la mvomero hajaliendeleza ambapo alisema katika shamba
hilo kuna mifugo yake, mashine mbalimbali, visima vya maji pamoja na
mazao.
“Jana nimepokea barua kuwa shamba la Mvomero ekari 326 limetwaliwa na
Rais na sitakiwa kukanyaga hapo. Shamba hilo lina majengo, mazao,
mashine mbali mbali, visima virefu vya maji, umeme na mifugo
mchanganyiko zaidi ya 200. Kisingizio shamba halijaendelezwa! Shamba
lenye vitu vyote hivyo halijaendelezwa?? “
Sumaye alieleza kwamba tayari alishafungua kesi katika Mahakama
Kuu kwa mashamba yote na mahakama imeweka zuio la kutokuingiliwa
mashamba hayo mapaka mashauri ya msingi yatakapoamuliwa lakini serikali
imeamua kukaidia uamuzi huo.
0 comments:
Post a Comment