Sunday, 13 August 2017

BILL GATE SASA KUISAIDIA TANZANIA KIFEDHA

Bill Gate (kulia) akisalimiana na Gavana wa Benki Kuu, Benno Ndulu.
MWASISI wa Taasisi ya Bill and Melinda Gates Foundation, Bill Gate, aliyekuwa nchini wiki hii amesema ataisaidia Tanzania katika masuala ya huduma nyepesi na isiyo na gharama ya kifedha kwa njia ya mitandao katika mfumo wa kidijitali katika miradi iliyomo katika taasisi hiyo nchini kwa lengo la kusaidia na kuzifikia jamii maskini nchini.

Taarifa iliyotolewa na Financial Sector Deepening Trust (FSDT) jijini Dar es Salaam, imesema kwamba akiungana na viongozi wa serikali, watoa huduma za kifedha zenye kutembea (mobile) na za kidijitali, Gates alifanya mazungumzo nao kuhusu utafiti wa mchango mkubwa wa kuduma hizo katika kuendeleza maisha na uzalishaji wa nchini.
Bill Gate akiwa na wawakilishi wa taasisi mbalimbali za kifedha nchini.
Gates pia alihakiki maendeleo ya miradi inayogharimiwa na taasisi yake ili kuipatia nguvu ya kifedha. Chini ya mpango wa kutoa huduma kwa watu maskini ujulikanao kama ‘Financial Services for the Poor’, taasisi hiyo inalenga kuwasaidia watu katika maeneo maskini zaidi duniani ili kuendeleza maisha yao kwa kuwaunganisha na vyombo vya huduma za kidijitali katika masuala ya fedha.

Ubunifu na uwekezaji katika teknolojia kwa lengo la kuimarisha huduma za kifedha kwa mfumo wa kidijitali, ikiwa ni pamoja na misaada ya usimamizi wa kiserikali, vimezaa matokeo makubwa ya misaada ya kifedha kwa jamii maskini katika miaka ya karibuni.

Zaidi ya nusu ya watu wazima nchini Tanzania hivi sasa wanafikia huduma za kifedha kutokana na kuanzishwa kwa huduma hizo zinazotembea ambazo huduma zake hufika hata sehemu za ndani kabisa nchini.
Katika hali hii, taarifa hiyo imesema, huduma hiyo imeongezeka kwa kiwango kikubwa na hivyo kuchangia kuwafikia watu wengi maskini ambapo mnamo mwaka 2009 jamii hiyo ilikuwa haifiki kwa walengwa kwa asilimia 55.4 na sasa kiwango hicho kimeshuka na kuwa asilimia 27.4 tangu mwaka 2013.

Wakati wa mazungumzo hayo, Gate alielezea umuhimu wa kazi ya taasisi yake nchini Tanzania aliposema: “Moja ya sababu inayotufanya tuithamini Tanzania ni kwamba hii ni nchi muhimu ambamo pia uongozi wake unapigania kuunganisha ufanisi wa miundombinu kitaifa.”

Alisisitiza pia ulazima wa wafanyabiashara kupata malipo yao kwa njia ya kileletroniki na jinsi mfumo huo unavyoweza kuenezwa nchini kote na namna taasisi yake inayoweza kuuimarisha mfumo huo ukijumuisha malipo ya serikali.
Mazungumzo hayo yaliyoandaliwa na Innocent Ephraim, kiongozi wa FSDT, yalijadili pia nguvu ya taasisi na mashirika mbalimbali katika kufanya ubunifu na kuwekeza katika mfumo wa malipo ya fedha kidijitali na jukumu ya miundombinu ya umma na shiriki katika kutatua vikwazo vya masoko kwa kutumia mfumo huo.
Jopo la majadiliano hayo lilimjumuisha Bill Gate na wawakilishi waandamizi kutoka tasnia ya viwanda, mawasiliano na taasisi mbalimbali za fedha nchini.

Majadiliano ya duru la pili yalimhusisha Gavana wa Benki Kuu, Prof. Benno Ndulu, viongozi kutoka makampuni yanayohusiana na masuala ya fedha yenye lengo la kufungua fursa za kuwepo mfumo wa malipo kati ya serikali na watu binafsi na kupanua mfumo wa malipo kwa watu maskini.
Majadiliano hayo yalijumuisha Mamlaka ya Udhibiti wa Mawasiliano (TCRA), Mfuko wa Misaada ya Kijamii (TASAF), Mamlaka ya Vitambulisho nchini (NIDA) na wadau mbalimbali ikiwemo FSDT.
Share:

0 comments:

Post a Comment

Ads

Blog Archive