Mshambuliaji wa Simba, Emmanuel Okwi amewajibu kwa vitendo wanaomwita
'mhenga' kwa kufunga mabao manne akiongoza Simba kuisambaratisha Ruvu
Shooting kwa magoli 7-0 katika mchezo wa ufunguzi wa Ligi Kuu Bara
uliofanyika kwenye Uwanja wa Uhuru jijini Dar es Salaam.
Ushindi
huo unaifanya Simba kuongoza ligi kwa tofauti ya mabao kabla ya
mabingwa watetezi Yanga kesho Jumapili kucheza na Lipuli kwenye Uwanja
wa Uhuru.
Okwi aliyejiunga na Simba msimu ameanza
kuonyesha ubora wake kwa kufunga mabao yake matatu katika dakika 45 za
kwanza akimalizia pasi nzuri za kiungo Muzamiru Yassin kabla ya kuongeza
moja katika kipindi cha pili akiunganisha pasi ya Said Ndemla. Mabao
mengine ya Simba yalifunga na Shizza Kichuya, Juma Luizio na Erasto
Nyoni.
Akizungumzia mabao yake Okwi alisema magoli hayo
anayatoa kwa mke wake ambaye ni mjamzito na ndio maana alijituma sana
katika mchezo huo ili kumpa zawadi nzuri mke wake kipenzi.
Okwi
alianza kufungua karamu ya mabao ya Simba dakika ya 18 akifunga kwa
shuti kali akimalizia pasi ya Mzamiru kabla ya kufunga la pili dakika ya
22 baada ya kumpiga chenga beki wa Ruvu Shooting,Shaibu Nayopa na
kutumbukiza mpira nyavuni, na kisha kufunga tena la tatu dakika ya 35
kabla ya kuhitimisha siku yake nzuri ya jana kwa kufunga bao la nne
dakika ya 53 akimalizia pasi ya Said Ndemla.
Mabao
mengine ya Simba katika mchezo huo yalifungwa na Shiza Kichuya dakika ya
41 akimalizia pasi ya Erasto Nyoni kabla Juma Liuzio kufunga lingine
dakika ya 45 na bao la saba likifungwa na Nyoni dakika ya 81 akimalizia
pasi safi ya Said Ndemla.
Simba
ilitawala mchezo huo katika vipindi vyote viwili huku Ruvu Shooting
ikishindwa kupiga hata shuti moja la maana golini kwa Simba huku kocha
wa maafande hao,Abdulmatic Haji Kiduu akijitetea kuwa wamefungwa kwa
sababu ya kuwakosa wachezaji wake sita wa kikosi cha kwanza walio katika
mashindano ya Majeshi nchini Burundi.
Kama Simba
ingekuwa makini ingeweza kufunga mabao mengi zaidi katika mchezo huo
kwani dakika ya 21,Liuzio alishindwa kuipatia timu yake bao akipokea
pasi safi ya mpira wa faulo kutoka kwa Haruna Niyonzima lakini akashikwa
na kitete akishindwa kujua afunge au ampe pasi Okwi na kujikuta mpira
wake ukiwahiwa na kipa wa Ruvu Shooting,Bidii Abdallah.
Pia
Niyonzima alikosa bao dakika ya 36 akipokea pasi safi ya Liuzio lakini
baade akatolewa kabla ya kipindi cha kwanza kumalizika baada ya kuumia
na nafasi yake kuchukuliwa na Mohammed Ibrahim.
Katika
mchezo huo wachezaji Mangasini Mangasini na Ishara Juma wa Ruvu Shooting
walionyeshwa kadi za njano kwa kuwafanyia faulo Okwi na Niyonzima.
Kwenye
Uwanja wa Nangwanda Sijaona Mtwara, Azam iliichapa Ndanda bao 1-0
lililofungwa dakika ya 34 na mshambuliaji Yahaya Mohammed.
Singida
United pamoja na kufanya usajili mkubwa bado wamekalibishwa katika Ligi
Kuu kwa kipigo cha mabao 2-1 kutoka kwa Mwadui kwenye Uwanja wa Mwadui
Complex Shinyanga.
Paulo Nonga alianza kuipatia Mwadui
bao dakika ya 30 baada ya kumchambua kipa wa Singida United,Manyika
Peter na kutumbukiza mpira nyavuni kabla ya Kenny Ally kuisawazishia
Singida United dakika ya 53 akimalizia pasi ya Atupele Greeen.
Salim
Hamis aliipatia Mwadui bao la pili na la ushindi kwa kichwa dakika ya
64 akimalizia pasi ya Hassan Kabunda na kumuacha kocha wa Singida
United, Hans Pluijm ambaye aliushuhudia mchezo huo akiwa jukwaani
kutokana na kutumikia adhabu ya kufungiwa mechi tatu na Shirikisho la
Soka Tanzania (TFF) wakati akiwa Yanga.
Kwenye Uwanja
wa Manungu Turiani Morogoro,Mtibwa Sugar iliichapa Stand United bao 1-0,
shukrani kwa goli la Hussein Javu alilolifunga dakika ya 76, akimalizia
krosi ya Issa Rashid'Baba Ubaya'.
Uwanja wa Sabasaba
Njombe,Prisons iliibuka na ushindi wa mabao 2-1 dhidi ya wenyeji Njombe
Mji.Mabao ya Prisons yalifungwa na Kassim Hamis na Nurdin Chona.
Kwenye
Uwanja wa Uwanja wa Sokoine Mbeya wenyeji Mbeya City iliichapa
Majimaji bao 1-0,bao la washindi likifungwa kiufundi na Eliud Ambokile
dakika ya 32 baada ya kupokea mpira wa kurushwa kutoka kwa Hassan
Mwasapili kisha kuutuliza kifuani na kuachia shuti kali nje kidogo ya 18
na mpira kumshinda kipa wa Majimaji Hushimu Mussa.
Kwenye
Uwanja wa Kaitaba Bukoba,wenyeji Kagera Sugar walilala kwa bao 1-0
dhidi ya Mbao, bao la washindi likifungwa dakika ya sita na Boniface
Maganga.
Msimamo wa Ligi Kuu Bara
P W D L F A Pts
1.Simba 1 1 0 0 7 0 3
2. Prisons 1 1 0 0 2 1 3
3.Mwadui 1 1 0 0 2 1 3
4.Azam 1 1 0 0 1 0 3
5. Mbao 1 1 0 0 1 0 3
6. Mbeya City 1 1 0 0 1 0 3
7. Mtibwa 1 1 0 0 1 0 3
8. Kagera 1 0 0 1 0 1 0
9. Ndanda 1 0 0 1 0 1 0
10. Stand 1 0 0 1 0 1 0
11. Majimaji 1 0 0 1 0 1 0
12. Njombe 1 0 0 1 1 2 0
13. Singida United 1 0 0 1 1 2 0
14. Ruvu Shooting 1 0 0 1 0 7 0
15. Lipuli 0 0 0 0 0 0 0
16. Yanga 0 0 0 0 0 0 0
0 comments:
Post a Comment