Kwa mara ya kwanza kikosi cha timu ya taifa ya Tanzania
‘Taifa Stars’ kitakuwa na wachezaji saba wanaocheza soka la kulipwa nje
kitakachocheza mechi ya kirafiki ya kimataifa Septemba 2, dhidi ya
Botswana kwenye Uwanja Uhuru, Dar es Salaam.
Wachezaji
hao saba wanaungana na wenzao 14 wanaocheza soka nchini kuunda kikosi
cha wachezaji 21 kitakachoingia kambini wiki ijayo kujiandaa na mechi
hiyo ya kirafiki iliyokuwa katika kalenda ya Fifa.
Kocha
wa Taifa Stars, Salum Mayanga amewaita kwa mara ya kwanza Mtanzania
Orgenes Mollel anayecheza FC Famalicao, Ureno na kiungo wa Sony Sugar ya
Kenya, Hamis Abdallah.
Wengine wanaocheza nje
waliotwaa ni pamoja na nahodha wa Stars, Mbwana Samatta (Genk,
Ubelgiji), Simon Msuva (Difaa EL Jadidiy, Morocco), Farid Mussa (CD
Tenerife, Hispania), Elias Maguli (Dhofar SC, Oman), na beki Abdi Banda
(Baroka FC, Afrika Kusini).
Pia, Mayanga amewarudishwa kundini kipa wa Azam, Mwadini Ally na beki wa Yanga, Kelvin Yondani.
Mayanga alisema Mwadini amefanya vizuri kwenye mechi za majaribio za timu yake na ameona ni wakati muafaka kumrejesha kundini.
"Said
Mohammed na Beno Kakolanya wameumia sasa nimeona Mwadin atatufa kwa
sababu amefanya vizuri kwenye klabu yake katika mechi za maandalizi ya
msimu huu,"alisema Mayanga, aliyewahi kuifundisha Mtibwa Sugar.
Katika kikosi kilichoitwa Mayanga pia amemrudisha kundini beki Yondani.
"Kelvin
alinieleza kuwa ana maandalizi ya ndoa ndio tukamweka pembeni. Kabla ya
kutangaza kikosi niliongea naye na akanambia yuko tayari kurudi,"
alisema Mayanga.
Wachezaji walioitwa ni makipa Aishi
Manula (Simba), Mwadin Ally (Azam) na Ramadhan Kabwili (Yanga), mabeki
ni Gadiel Michael, Kelvin Yondani (wote Yanga), Boniface Maganga (Mbao),
Abdi Banda (Baroka FC, Afrika Kusini), Salim Mbonde na Erasto Nyoni
(wote Simba).
Viungo walioitwa kikosini ni Said Ndemla,
Mzamiru Yassin, Shiza Kichuya (wote Simba), Himid Mao (Azam), Simon
Msuva (Difaa EL Jadidiy, Morocco), Farid Mussa (CD Tenerife, Hispania),
Raphael Daud (Yanga) na Mollel (FC Famalicao, Ureno) na Hamis Abdallah
(Sony Sugar, Kenya).
Washambuliaji walioitwa ni Kelvin
Sabato (Mtibwa Sugar), Elias Maguli (Dhofar SC, Oman), na nahodha Mbwana
Samatta (Genk, Ubelgiji).
Wakati huohuo, Ofisa Habari wa TFF, Alfred Lucas alisema ratiba ya mchezo inaweza kuathiri ratiba ya Ligi Kuu Tanzania Bara.
"Wiki
ya Fifa kwa mujibu wa ratiba ya awali ilitakiwa kuanzia Septemba 5
lakini imerudishwa nyuma, tutaona ratiba ya ligi lakini inaweza
kuathirika,"alisema.
Endapo ratiba ya ligi
itabadilishwa itaziathiri klabu za Simba na Yanga zenye zaidi ya
wachezaji wanne kwenye kikosi kilichoitwa.
0 comments:
Post a Comment