BAADA ya ukimya wa muda mrefu wa kutoachia ngoma mpya, staa wa Bongo
Fleva, Ali Saleh Kiba ‘King Kiba’ aliwaweka kwenye ‘kimuhemuhe’
mashabiki wake kwa kuonesha dalili za kuachia wimbo mpya ambao
ulishakuwa maarufu kabla hata haujatoka.
Mkali huyu ambaye alikimbiza na wimbo wa Aje alioutoa mwaka jana, kwa
kipindi chote hicho alikaa kimya na sasa ‘ameuvuruga’ ulimwengu wa
burudani kwa ‘kubipu’ na posti zinazoashiria wimbo wake mpya uitwao
Kipusa. Kupitia ukurasa wake wa Instagram wenye mashabiki zaidi ya
milioni mbili, Kiba alianza kutupia picha zilizoandikwa Kipusa na
kuwafanya mashabiki wake wapagawe kwa kumtaka autoe wimbo huo haraka
iwezekanavyo.
“I cant wait Kiba, achia bwana hiyo Kipusa iwakimbize wote wenye
nyimbo mbovumbovu mjini,” aliandika mmoja wa wafuasi wa Instagram. KING
NI KING Kiba ana historia ya kutoa wimbo au nyimbo kadhaa na zikakaa
kwenye soko kwa muda mrefu tofauti hata na yule msanii anayejidai kuwa
ni mpinzani wake wa jadi ambaye kila siku anatoa nyimbo lakini hazikai
muda mrefu kwenye soko, zinaotea.
USHAHIDI NI HUU
Kabla ya Kiba hajatoa Chekecha Cheketua mwaka 2015, alikuwa kimya kwa
muda mrefu lakini mashabiki wake waliendelea kusikiliza ngoma za
kitambo kama Cindelera na Kidela. Alipoibuka mwaka huo, kila mmoja
alikubaliana na ujio wake wa Chekecha Cheketua kabla hajachagiza na Aje
kisha Mwana. Hapo ndipo kila mtu alimjua Kiba ni nani. Kila mtaa, kila
nyumba watu walisikika wakicheza nyimbo hizo za Kiba ambapo
alidhihirisha ule usemi wake wa ‘nimepangusa kiti changu kilichokuwa na
vumbi kisha nakikalia tena’.
UTOFAUTI WA KIBA
Tofauti na wasanii wengine, Kiba ni mwanamuziki.
Namaanisha msingi wake umejengeka katika muziki. Anajua kuimba na
vyombo, tofauti na wasanii wengi wa Bongo Fleva ambao ukiwaambia waimbe
kwa vyombo, wataingia mitini.
HADI SASA HAKUPOA
Baada ya kuachia ngoma hizo, Kiba alikaa tena kimya hadi jana
alipoaamua kuachia ngoma yake ya Kipusa (video na audio) na tayari
imekuwa gumzo kila kona ya jiji.
SHOO KIBAO NJE YA NCHI
Kuonesha kwamba Kiba yupo vizuri, kwa wakati wote huo amekuwa akifanya shoo nyingi nje ya nchi.
AMEPIGA SHOO NEW YORK, MAREKANI
Huyo ndiye Kiba ambaye hata mwishoni mwa wiki iliyopita, aliandika historia kwa kufanya shoo matata sana pande za Marekani.
KOLABO KALI
Moja kati ya sifa nyingine kubwa ambayo Kiba anayo, amefanya kolabo
nyingi sana ambazo kimsingi, hazijawaacha salama wenye nyimbo zao.
Amefanya balaa kwenye kolabo kama Kiboko Yangu ya MwanaFA, amefunika
mbaya katika Nisamehe ya Baraka The Prince na nyingine nyingi. Ana sauti
kali ambayo anajua kuipangilia. Anapanda, anashuka.
Ni wasanii wachache sana wenye sifa ya namna hiyo duniani na ndiyo
maana Kiba ameendelea kuwa Kiba miaka yote Bongo. Hata anayejiita
mpinzani wake, anasifika kwa kutoa nyimbo nyingi ambazo mara nyingi
zimegeuka kuwa kama big G lakini Kiba hata sasa akiimba Cindelera, bado
mashabiki wataifurahia.
0 comments:
Post a Comment