Haruna Niyonzima.
KIUNGO wa Simba, Haruna Nyiyonzima, amekiri ugumu wa mechi yao ya leo
Jumamosi dhidi ya Ruvu Shooting, lakini anaamini timu nyingi ikiwemo
Yanga zipo vizuri na wao watapambana nazo ili watwae ubingwa.
Simba inaanza Ligi Kuu Bara kwa kucheza na Ruvu Shooting
kwenye Uwanja wa Taifa halafu kesho Jumapili Yanga itacheza na Lipuli
FC ya Iringa uwanjani hapo katika muendelezo wa ligi hiyo.
Niyonzima ambaye leo ataichezea Simba
mchezo wake wa kwanza wa ligi kuu tangu ajiunge nao akitokea Yanga,
amesema mbali na timu zote kujiandaa vizuri, watapambana kuhakikisha
wanatwaa ubingwa.
Akizungumza na Championi Jumamosi, Niyonzima alisema kikosi chao kina
mastaa wengi wanaoweza kuamua matokeo mazuri, lakini watatakiwa
kupambana kwa kila hali katika kila mchezo ulio mbele yao ili wapate
ushindi.
“Kila timu ipo vizuri, Yanga wapo vizuri na wanautaka ubingwa, hivyo
na sisi tumejipanga kuhakikisha tunashinda mechi zetu zote japokuwa
nyingi ni ngumu ikiwemo hii ya kesho (leo).
“Hatuna njia rahisi ya kutwaa ubingwa bila kupambana kwa juhudi zote,
sisi ni wazuri kila upande jambo ambalo naamini litazifanya timu
pinzani kutukamia ili tusiweze kupata matokeo, ila tutapambana,” alisema
Niyonzima raia wa Rwanda.
0 comments:
Post a Comment