Wachezaji wa Kitanzania wanaocheza mpira wa kulipwa nje ya nchi ameanza
kutikisa barani Ulaya mwishoni mwa wiki katika michezo ya ligi pamoja
na mechi za kirafiki za kujiandaa na msimu mpya wa ligi mbalimbali.
Ubelgiji
Nahodha
wa Taifa Stars, Mbwana Samatta ameanza kufungua kapu lake la mabao
baada ya kufunga goli mbili na kuiongoza Genk kushinda 5-3 dhidi ya
Royal Antwerp FC katika mchezo wa Ligi Kuu ya Ubelgiji ‘Jupiler Pro’.
Katika
mchezo huo Samatta alifunga mabao yake katika dakika 8 na 41 na
kuifanya Genk kupata ushindi wake wa kwanza tangu kuanza kwa ligi hiyo
ikiwa imecheza mechi tatu ikifungwa moja kutoka sare moja na kushindi
moja.
Hispania
Mshambuliaji Simon Msuva ni kama amejibu mapigo ya Samatta kwa kufunga juzi nchini Hispania katika mchezo wa kirafiki.
Msuva yupo Hispania na timu yake ya Difaa Hassani El Jadidi akijiandaa na Ligi Kuu Morocco ‘Batola Pro’.
Msuva
amedai licha ya kupoteza mchezo huo kwa mabao 2-1 na USMO, timu yake
ilicheza vizuri lakini haikuwa na bahati ya kushinda mchezo huo.
“Ni
vikosi viwili vilitumika kama ilivyokuwa kawaida yetu, kila kikosi
kilipata dakika 45, nimefunga bao ambalo halikutosha kutufanya
tusipoteze” alisema Msuva.
Naye Mtanzania Farid Mussa
anayecheza CD Tenerife alishindwa kuisaidia timu yake isiepuke kipigo
cha mabao 3-0 kutoka kwa Deportivo La Coruna katika mchezo wa kirafiki.
Kiwango
alichoonyesha Farid katika michezo ya kirafiki msimu huu kinafungua
milango kwake kucheza kikosi cha kwanza cha Tenerife katika ligi ya
Segunda watafungua dhidi ya Real Zaragoza, Agosti 18.
Ureno
Mtanzania
Orgenes Mollel ilicheza timu yake Famalicao ikilazimishwa sare 1-1 na
Penafiel katika mchezo wa Ligi daraja la pili nchini Ureno ‘Segunda
Liga’ya uliofanyika Agosti 13 ugenini kwenye Uwanja wa Municipal.
Mollel
mwenye miaka 19 amekuwa na changamoto ya kuanza katika kikosi cha
kwanza cha timu hiyo ambayo inashika nafasi ya tatu ikiwa na pointi nne
(4) katika msimamo wa Ligi hiyo.
Ujerumani
Beki
wa kushoto Emily Mgeta aliingoza VfB Eppingen kupata ushindi mnono wa
mabao 4-1 dhidi ya Oeffingen katika mchezo wa kirafiki nchini Ujerumani.
“Huo
ndiyo mchezo wetu wa mwisho maana wiki ijayo tunaanza ligi, kikubwa
tulichopanga ni kupanda daraja, tumefanya maandalazi ya kutosha na hata
tulivyoweka kambi nchini Italia kulikuwa na sababu.” alisema beki huyo
wa zamani wa Simba.
Austria
Kinda
la Kitanzania, Michael Lema anayeichezea SK Sturm Graz ya Austria
amepata majeraha ya kifundo cha mguu yatayomweka nje kwa wiki mbili au
zaidi.
Lema alisema hajui ni lini atarejea uwanjani,
lakini amekuwa akitajwa kuwa huenda akaanza mazoezi mepesi ndani ya wiki
tatu zijazo.
“Niliumia mazoezini naendelea vizuri maana mwanzo ilidhaniwa kuwa ni majeraha makubwa, lakini imekuwa tofauti,” alisema Lema.
0 comments:
Post a Comment