Mgombea urais wa muungano wa
upinzani Nasa Raila Odinga amewaambia wanahabari kwamba wamepata habari
kwamba mitambo ya Tume ya Uchaguzi IEBC ilidukuliwa na matokeo halisi
kufanyiwa ukarabati.
IEBC imekuwa ikitangaza matokeo ya awali ya
urais mtandaoni, na kwa sasa matokeo hayo yalikuwa yanamuonyesha Rais
Uhuru Kenyatta wa chama cha Jubilee akiwa mbele na kura 7,795,083
(54.38%) naye Bw Odinga akiwa na kura 6,433,161 (44.76%).
Matokeo hayo ni ya kutoka vituo
38561 kati ya vituo 40883 nchini humo.
Kura zilizoharibika kufikia sasa ni 382,705
Bw
Odinga, akiandamana na mgombea mwenza wake Kalonzo Musyoka, na viongozi
wengine wakuu wa muungano huo, amesema wadukuzi walitumia taarifa
alizokuwa nazo meneja wa teknolojia wa IEBC Chris Msando aliyeuawa wiki
moja iliyopita kuingia katika mitambo ya IEBC.
Waziri huyo mkuu wa
zamani amesema baada ya kuingia, wadukuzi walitumia programu fulani
kuongeza matokeo ya Rais Kenyatta na kupunguza matokeo yake.
Amesema anaamini hilo lilifanyika katika kaunti zote na kwamba wagombea wa NASA katika nyadhifa nyingine waliathirika pia.
Bw Odinga, amesema huo ulikuwa "ulaghai wa hali ya juu".
Hata hivyo, ametoa wito kwa wafuasi wa muungano huo waendelee kuwa watulivu.
Bw
Musyoka amesema anawashauri wafuasi wa muungano huo waendelee na
shughuli zao za kawaida, ingawa huenda karibuni wakatakiwa kuchukua
hatua.
Bw Odinga na Kalonzo wamekataa kusema ni hatua gani zaidi
watachukua na badala yake wakasema wanasubiri kusikia ufafanuzi kutoka
kwa IEBC kuhusu yaliyotokea.
Mwenyekiti wa IEBC Wafula Chebukati
amewaambia wanahabari baadaye kwamba wamepata habari kuhusu tuhuma za
muungano huo wa upinzani kwamba mitambo yao ya uchaguzi ilidukuliwa.
Amesema
tume haiwezi kupuuza tuhuma kama hizo na kwamba maafisa wake watafanya
uchunguzi kubaini iwapo kuna ukweli wowote katika madai hayo.
Hata
hivyo alieleza imani yake kwamba mfumo wa uchaguzi unaotumiwa na tume
hiyo ni imara na kwamba ulitumiwa na shughuli zote za awali, na sasa
"imesalia shughuli ya mwisho" ya kupeperusha na kutangaza matokeo ya
kura.
0 comments:
Post a Comment