MTIKISIKO mkubwa umetokea kufuatia bomoabomoa inayoendelea jijini
hapa ambayo imeacha vilio kwa baadhi ya watu, huku ikibainika kuwa
makanisa 20 na misikiti 11, ni miongoni mwa majengo yaliyowekewa alama
za X kuashiria kuwa yatabomolewa na Wakala wa Barabara Tanzania (Tanroads) kupisha ujenzi wa Barabara ya Morogoro-Dar.
Uwazi lilifanya uchunguzi kuanzia eneo la
Ubungo, Kimara, Mbezi Luis hadi Kiluvya jijini hapa mwishoni mwa wiki
iliyopita na jana na kubaini kuwa licha ya watu wa kawaida, waumini wa
makanisa na misikiti hiyo wamejawa na simanzi kutokana na kukumbwa na
bomoabomoa hiyo.
TANESCO WAKATALIWA KUKATA UMEME
Jana waandishi wetu walishuhudia baadhi ya wananchi wakiwakataza
mafundi wa Tanesco kukata umeme kwenye baadhi ya nyumba ambazo
zimewekewa alama X eneo la Kimara Stop Over, hata hivyo, hakuna
aliyekuwa tayari kusema sababu za kufanya hivyo.
MAKANISA YENYE ALAMA YA X
Kanisa la Ufufuo na Uzima linaloongozwa na Askofu Josephat Gwajima lililopo Ubungo Maji, ni miongoni mwa nyumba za ibada zilizowekewa alama ya X, hivyo kiongozi huyo kukutwa na dhahma nyingine.
Kiongozi huyo amekuwa akikumbwa na matukio mengi huku akifikishwa polisi na mahakamani mara kadhaa.
Katika uchunguzi wa gazeti hili, imebainika kuwa makanisa mengine yatakayokumbwa na bomoabomoa hiyo ni Kanisa
la Anglikana Stop Over, Kanisa la Kiinjili la Kilutheri Tanzania (KKKT)
Usharika wa Kibamba, KKKT Usharika wa Mbezi Luis, Kanisa Katoliki
Kimara litakalobomolewa nusu, Kanisa Katoliki la Mbezi Luis,
The River Healing Ministry of Tanzania la Kibamba na Kanisa la Calvary
Salvation lililopo Kibamba.
Makanisa mengine ni Kanisa la TAG Rejoice Center la Mbezi, Kanisa la
Kaprenan lililopo Kibamba, TAG – Suka, Pentekoste of Tanzania Kiluvya,
Nayoth Church Kiluvya, KLPT la Bwawani, Kapernan Centre Mbezi, TAG
Calvary Temple Mbezi Inn na GRC Mbezi Inn.
MENGINE YAMEBOMOLEWA
Katika uchunguzi wetu, baadhi ya makanisa yameshabomolewa kutii agizo
la kubomoa kwa hiyari likiwemo la Moravian Kimara Stop Over na KKKT
Kibamba.
Askofu wa Dayosisi ya Dar es Salaam wa Kanisa la Kiinjili la
Kilutheri Tanzania, Dk. Alex Malasusa, Jumamosi iliyopita alikwenda
kuwafariji na kuwatia moyo waumini wa kanisa lake ambao wamepatwa na
simanzi kutokana na uamuzi huo wa serikali.
“Najua mna huzuni, majengo mengi yatabomolewa na serikali ili kupisha
ujenzi wa barabara, kwa hili hamna budi kukubali na kuamini kuwa hiyo
ni baraka kwa Mungu, zaidi kuweni na amani, ombeni baraka na kumshukuru
Mungu,” alisema Dk. Malasusa.
Kwa upande wake, Mchungaji wa KKKT Kibamba, Mshiu Wilness alisema
kanisa limepokea agizo la kutakiwa kuhama na kubomoa jengo hilo na
kwamba, tayari wameshapata eneo jingine ambalo wanatarajia kuhamia.
“Tumepokea, tunatarajia kuondoka na tutavunja kama tulivyoelekezwa,” alisisitiza kiongozi huyo.
MISIKITI NAYO YAKUMBWA
Licha ya makanisa hayo, kuna misikiti itakayokumbwa na bomoabomoa
hiyo ambayo ni Masjid Kilumbi Islamic Center – Kimara Mwisho, Dalul
Mustafah wa Kimara Stop Over, Masjid Baitul Maamur, Masjid Jaaria, Al
Masjid Nuur uliopo Kiluvya, Masjid Jaalia Gogan, Masjid Nuur Kibamba CCM
na misikiti mingine mitatu ya Mbezi Inn, Mbezi Luis na Temboni.
VIONGOZI WA DINI WANENA
Wakizungumzia bomoabomoa hiyo, baadhi ya mashehe na wachungaji
wametaharuki, wakisema wamepokea maagizo ya serikali ya kutakiwa kuvunja
majengo yao huku wengine wakimuomba Rais Dk. John Pombe Magufuli
kuwatazama kwa jicho la huruma.
Imamu wa Msikiti wa Jamsjid Jaria wa Kiluvya, Haidary Masenga alisema
waumini wameathirika kisaikolojia kwa kutojua msikiti huo
utakakohamishiwa kwa kuwa hakuna eneo walilopata.
“Wote tunataka maendeleo na sisi hatupingi, lakini tunaomba tutazamwe
kwa jicho la huruma tuachwe tuendelee kuabudu hapa. Mpaka sasa hatujui
chochote tunasubiri tu hatima ya serikali kama watavunja au la,” alisema
Imamu Masenga.
Imamu Msaidizi wa Msikiti wa Kilumbi Islamic Center, Halfan Malima
alimuomba Rais Magufuli kuwahurumia kwa kuwapa eneo lingine la ibada kwa
kuwa bado hawajapata.
Mchungaji wa Kanisa la The River Healing Ministry of Tanzania, John
Kyashama alisema anaunga mkono agizo la serikali la kubomoa nyumba,
makanisa na misikiti ili kupisha upanuzi wa barabara.
Kyashama alisema hana kinyongo na rais na anaunga mkono mipango ya
maendeleo anayoifanya na anawashauri wachungaji wenzake waliokumbwa na
bomoabomoa kukubaliana na hali hiyo kwa kuwa kinachofanywa na serikali
ni kwa nia njema.
“Si vizuri kuwa na kinyongo wala kuzozana na utawala, kila mtu atii mamlaka za nchi,” aliasa mchungaji huyo.
MALALAMIKO YA WANANCHI
Licha ya nyumba hizo za ibada, baadhi ya majengo ya wananchi pia
yamewekwa alama ya X ambapo wengi wameitupia lawama serikali kwa madai
kwamba wakati wanajenga nyumba hizo, walikuwa hawajavunja sheria yoyote.
Mzee John Mlangi (74), mkazi wa Kimara Stop Over alisema amejenga
nyumba yake miaka 35 iliyopita na wakati huo hakukuwa na sheria ya ardhi
aliyoivunja kwa kuwa alikuwa nje ya mita 60 kutoka kwenye barabara na
kiwanja hicho alikuwa akikilipia kodi kwa miaka yote hiyo.
“Kutokana na kuwekewa alama ya X nimekuwa nikiishi kwa wasiwasi na nimepata ugonjwa wa shinikizo la damu,” alisema.
Mwenyekiti wa Serikali ya Mtaa wa Stop Over, Kimara, Magreth Msabuso
alisema katika mtaa wake, wapo wazee wengi waliostaafu ambao ikiwa
nyumba zao zitabomolewa bila fidia, hali zao zitakuwa mbaya.
Alisema wananchi wote waliowekewa alama za X nyumba zao walipaswa
kushirikishwa tangu hatua ya kwanza kabla ya kuweka alama hizo.
POLISI NAO WAKUMBWA
Mbali na nyumba hizo za kiraia na za kidini, pia Kituo cha Polisi
Mbezi Luis kitabomolewa huku Kamanda wa Polisi wa Mkoa wa Kipolisi wa
Kinondoni, ACP Muliro Jumanne akisema kilijengwa kwa nguvu za wananchi
kutokana na mahitaji ya eneo hilo.
Alisema kutokana na kuwekwa alama ya X, kituo hicho kitahamishiwa
eneo la Gogoni kwa kuwa licha ya kuwa barabarani, bado eneo lake ni
dogo.
“Kituo hiki kitaondolewa hapa na kupelekwa kwenye kituo kingine cha
Gogoni kilichojengwa chini ya mradi wa Matokeo Makubwa Sasa (BRN) na
ujenzi wake umeshirikisha nguvu za wananchi na ni kikubwa kwa Wilaya ya
Ubungo,” alisema.
VITUO VYA MAFUTA NAVYO BALAA
Vituo vya mafuta navyo vimekumbwa na balaa hilo na vilivyowekewa
alama ya X kwa ajili ya kubomolewa ni Camel Oil-Kimara Stop Over, Henry
Filling Station-Mbezi kwa Yusuph, Camel Oil – Kibamba, Uduru Oil Station
– Kibamba na Total-Stop Over.
HUDUMA ZA AFYA ZAKUMBWA
Vipo pia vituo vya huduma za afya vitakavyoguswa na bomoabomoa hiyo
ambavyo ni Hospitali ya Boch na Kituo cha Afya cha Kimara
vitakavyobomolewa nusu, Hospitali ya Neema iliyopo Kimara Stop Over,
Kimara Centre Dispensary na Zahanati ya Arafa.
0 comments:
Post a Comment