MBUNGE wa Jimbo la Kigoma Mjini, Zitto Kabwe amesema hayuko tayari kushiriki siasa za vurugu za kupinga mipango ya Serikali ya Rais John Magufuli katika kuwaletea maendeleo wananchi.
Akizungumza kwenye Viwanja vya Stendi ya zamani Ujiji mjini hapa, mbunge huyo akawashangaa baadhi ya wanasiasa nchini wanaomtaka ashiriki vurugu za kupinga juhudi za Serikali kwa kisingizio cha kupinga Chama Cha Mapinduzi (CCM) ili kujipambanua kama wapinzani. Kabwe alisema kuwa siasa hizo kwa sasa hazina nafasi kwake wala kwenye chama chake na kwamba anaunga mkono juhudi za Rais Magufuli na kwamba binafsi na chama chake wamejielekeza katika kuleta maendeleo kwa wananchi.
Kabwe alisema kuwa Mkoa wa Kigoma umekuwa nyuma kimaendeleo kwa miaka mingi hivyo kwa sasa utashirikiana na mtu yeyote mwenye mwelekeo wa kutetea maslahi mapana ya kiuchumi bila kujali itikadi yake. Kauli ya mbunge huyo wa jimbo la Kigoma mjini inakuja, ikiwa ni siku chache tangu Rais John Magufuli kufanya ziara mkoani hapa na kumsifia mbunge huyo kuwa ni kiongozi anayependa kuleta maendeleo kwa watu wake.
Hata hivyo, Zitto ambaye pia ni Kiongozi wa Chama cha ACT -Wazalendo alikiri demokrasia kwa sasa kuwa imefinywa tofauti na huko nyuma. Kwa upande wake, Mstahiki Meya wa Manispaa ya Kigoma, Hussein Ruhava akizugumzia halmashauri yake kupata hati chafu alikiri kuwepo kwa dosari mbalimbali za kiutendaji na kwamba kwa sasa halmashauri yake kwa kushirikiana na wadau mbalimbali imeanza kuziondoa dosari hizo.
Alisema kuwa halmashauri iko kwenye mkakati wa kutekeleza miradi mbalimbali ya maendeleo ukiwemo mradi wa maduka 3,000 maarufu kama Ujiji City unaotekelezwa kwa ufadhili wa Serikali ya China.
0 comments:
Post a Comment