WABUNGE wanane wa Chama cha Wananchi (CUF) waliovuliwa uanachama na chama hicho wamepinga hatua hiyo na kutishia kwenda mahakamani kutafuta haki yao.
Wakati wabunge hao wakisema hayo, Wakili wa siku nyingi, Tamila Makene alisema uamuzi wa chama cha siasa kuwavua uanachama wabunge ni uamuzi sahihi kwa mujibu wa Katiba ya nchi Ibara ya 71 kifungo kidogo 1(f). Tamila alisema hayo jana Dar es Salaam, wakati akizungumzia jambo hilo kisheria na kusema chama cha siasa ndicho kina mtambua mwanachama wake na kwamba chama hicho hicho ndicho kinachoweza kumvua uachama pia.
“Kama chama kimetoa taarifa kuthibitisha kuwavua uanachama wabunge hao ni sahihi kwa sababu hata Katiba inatambua na inaelezea ukomo wa mbunge kwenye Ibara ya 71 kifungu kidogo cha kwanza (f), sasa kama wataamua kwenda mahakamani ni jambo jingine,” alisema Makene.
Wakizungumzia kuvuliwa kwao uanachama, Kiongozi wa Wabunge wa CUF, bungeni ambaye naye amevuliwa uanachama, Riziki Ngwali alisema hadi sasa hawajapokea barua rasmi ya kuvuliwa uanachama wao na kusisitiza kwamba walichaguliwa kwa barua na lazima watenguliwe kwa barua.
“Hatujapokea barua hadi sasa, lakini pamoja na hilo, sisi hatukubali uamuzi huo kwa sababu haujatolewa na mamlaka sahihi, tumeamua kwenda mahakamani kutafuta haki yetu,” alisema Ngwali. Kaimu Naibu Katibu Mkuu wa CUF-Bara, Jafar Mneke alisema kati ya wabunge 10 wa viti maalumu wa chama hicho, wawili ndio wamesamehewa baada ya kutoa ushirikiano na Baraza la Maadili la chama hicho, lilipowahitaji wabunge wote hao kuwahoji.
0 comments:
Post a Comment