Thursday, 27 July 2017

SERIKALI YAPIGILIA MSUMARI UDAHILI







BAADHI ya vyuo vilivyosimamishwa kufanya udahili katika baadhi ya programu zake, vimebainisha kuwa vimeanza kuchukua hatua ya kuondoa dosari hizo, na viko tayari kufanyiwa uhakiki tena

Hayo yamebainishwa jana kwa nyakati tofauti jijini Dar es Salaam kwenye maonesho ya 12 ya Taasisi za Elimu ya Juu nchini yanayoendelea katika viwanja vya Mnazi Mmoja. Kwa upande wake, Makamu Mkuu wa Chuo cha Mtakatifu Augustine (SAUT), Padri, Thadeus Mkamwa alikiri kuwa baadhi ya matawi ya chuo chake, yamesimamishiwa udahili katika baadhi ya programu zake, lakini ni kutokana na tatizo la mawasiliano baina ya chuo hicho na TCU.
“Ni kweli walituletea notisi ya siku 14 tujibu kuhusu upungufu waliobaini, tumewajibu mapema tu, lakini wakati tunasubiria matokeo, tukasikia kwenye vyombo vya habari kuwa, baadhi ya programu zetu zimesimamishwa zisifanyiwe udahili, lakini tunalifanyia kazi,” alisema Mkamwa ambaye pia ni Mwenyekiti wa Umoja wa Wakuu wa Vyuo Vikuu nchini. Kwa upande wake, Ofisa Uhusiano wa Vyuo Vikuu vya Kanisa Katoliki, Atunus Simwambi, alikiri kuwa programu iliyosimamishiwa udahili ilikuwa kwa muda wa miaka mitatu angu ianzishwe haijawahi kuwa na wanafunzi na hivyo kutofundishwa chuoni hapo.
“Programu hii ilianzishwa kwa ajili ya watu wanaotakiwa kuwa mapadri au wanaokwenda kufanya kazi za utume katika maeneo mbalimbali. Kwa kuwa kuna mchakato wa kuunganisha chuo chetu na Chuo cha Filosofia cha Kibosho, tulitarajia programu hii itarejea,” alisema. Chuo hicho kimesitishiwa programu moja ya Bachelor of Arts in Philosophy with Ethics. Naye Makamu wa Chuo cha Waislamu cha Morogoro (MUM), Profesa Hamza Njozi, pamoja na kukiri kuwa katika baadhi ya programu zilizosimamishwa udahili zilikuwa na changamoto ya walimu, alieleza kuwa dosari hizo zimefanyiwa kazi kama ambavyo Tume ya Vyuo Vikuu Tanzania (TCU) ilivyoagiza katika notisi yake ya siku 14.
Alisema chuo hicho kilipatiwa notisi ya siku hizo 14 inayoanzia Julai Mosi hadi 14, mwaka huu, kufanyia marekebisho dosari hizo, lakini hata baada ya kutoa majibu, walishtukia kupitia vyombo vya habari, kuwa programu hizo zimesimamishiwa udahili. Akizungumzia taarifa ya TCU, Ofisa Mtendaji Mkuu wa Shirikisho la Watoa Elimu Wasiotegemea Serikali Kusini mwa Jangwa la Sahara(CIEPSSA), Benjamin Nkonya alisema uamuzi huo wa serikali ni nzuri kwani una nia njema ya kurudisha heshima ya elimu nchini.
Nkonya alisema hatua hiyo inapaswa kuungwa mkono na wadau wa elimu nchini kwa sababu yapo baadhi ya mambo ambayo yamechangia kiwango cha elimu kushuka wakiwemo baadhi ya wasomi ambao wameonesha udhaifu kwenye utendaji wao. “Kwanza kabisa tunaona jinsi rais anavyokerwa na baadhi ya wasomi ambao wanavuruga nchi badala ya kuwa kioo, ameona hakuna mwelekeo nah ii inawezekana ikatokana na mfumo wa elimu ambao wakati mwingine baadhi ya shule au vyuo vimetoa elimu isiyokidhi, sasa tunapojisahihisha ni vizuri ili tuwe na mfumo thabiti kwa manufaa ya taifa,” alisema Nkonya.
Alisema kwa bahati nzuri sekta ya elimu nchini kwa sasa imepata mtu sahihi kwenye wizara hiyo inayoongozwa na Profesa Joyce Ndalichako ambaye hata wao wana imani ataendelea kuiboresha zaidi kwa sababu utendaji kazi wake unatambulika. “Profesa Ndalichako ni mtu makini, nakumbuka nilipokuwa Shirikisho la Wamiliki na Mameneja wa Shule na Vyuo Visivyo Vya Serikali (TAMANGSCO) zaidi ya miaka 10, Profesa Ndalichako alipokuwa NECTA, aliadhibu shule au vyuo vilivyokosea, na alitoa adhabu kali hata wakati mwingine kufutia matokeo shule nzima alipobaini udanganyifu, alifanya hivyo kulinda heshima ya elimu,” alisema Nkonya. Hivyo akashauri kuwa uamuzi uliofikiwa na serikali kupitia TCU ni uamuzi sahihi na kuvishauri vyuo husika kufuata maelekezo ili kuhakikisha kiwango cha elimu kitolewacho kina ubora unaotakiwa.
Share:

0 comments:

Post a Comment

Ads

Blog Archive