Shirika la Umeme nchini (Tanesco) limedaiwa kugomea zoezi la ukataji
umeme kwenye nyumba zinazotakiwa kuvunjwa eneo la Kimara na Kiluvya ili
kupisha upanuzi wa barabara ya Morogoro leo Jumatatu, Julai 31 kwa kile
kinachoelezwa na shirika hilo kuwa Tanroads hawajajipanga.
Mratibu wa bomoabomoa, Ephrahim Kinyafu amesema Tanroads wameweka
kambi eneo hilo tangu saa nne asubuhi wakiwasubiri Tanesco kuendelea na
zoezi la kukata umeme lakini hawajafika, walipompigia simu Meneja wa
Tanesco Kimara, Christopher Nguma akadai hawawezi kuwakatia umeme wateja
wao.
“Kwanza asubuhi ya saa mbili nilikuwa ofisini kwa Meneja wa Tanesco
nikamweleza kuhusu ukataji wa umeme meneja alichonieleza ni kwamba
Tanroads hawajajipanga hawawezi kuja kukata umeme leo alafu waje kuvunja
nyumba baada ya miezi, “alimnukuu alivyo mweleza meneja huyo Kinyafu.
Kinyafu amesema sababu nyingine waliyoieleza Tanesco ni kuwa
utaratibu wa kuwakatia umeme unaambatana na kutoa notsi ya saa 48,
lakini hawajatoa na badala yake Tanroads wanawataka wakakate umeme kitu
ambacho hakiwezekani.
“Tanesco pia wamegoma baada ya kutoa taarifa yetu jana kwamba suala
letu la bomoabomoa liko mahakamani kwahiyo wanasema kama tunakesi
mahakamani basi hawatakata umeme, “amesema Kinyafu.
Meneja wa Tanesco Kimara, Christopher Ndono alipotafutwa kuzungumzia
suala la kugomea kukata umeme amesema taarifa zote wanazo Tanroads.
“Sina cha kuzungumzia juu ya hilo, taarifa zote wanazo Tanroads maana wao ndiyo wenye eneo,” amesema Ndono.
Hata hivyo, alipotafutwa injinia wa Barabara ya Tanroads eneo la
Kimara na Kiluvya, Jonhson Rutechura ambaye pia ndiye msimamizi wa
bomoabomoa amesema atafutwe baadaye.
0 comments:
Post a Comment